Waridi wa BBC: ‘Nilivyoporomoka kutoka kuwa meneja hadi kuwa mfungwa’

October 14, 2020

Dakika 15 zilizopita

Teresa Njoroge

Maelezo ya picha,

Kabla ya kufungwa Teresa Njoroge alikuwa mfanyikazi mashuhuri katika benki moja jijini Nairobi

Teresa Njoroge alipatwa na mshtuko alipoambiwa avue nguo zake na kuvalia sare za gereza kuashiria kwamba amekuwa mfungwa.

“Wakati huo nilihisi kana kwamba ubongo wangu umekufa ganzi. Haukuweza kung’amua yote yaliyokuwa yanatokea,” anakumbuka.

Ni maisha ambayo yangekuwa tofauti sana kwa mwanamke aliyekuwa amezoea madaraka na pesa.

Ilikuwaje hadi akafungwa jela?

Teresa alihukumiwa kufungwa jela mwaka mmoja baada ya kupatikana na hatia ya wizi na njama ya kulaghai.

Kabla ya hapo, alikuwa mfanyikazi mashuhuri katika benki moja jijini Nairobi na alikuwa amepata mafanikio makubwa.

Alikuwa anaishi maisha mazuri na alikuwa amehakikisha pia kwamba mwanawe aliyekuwa amezaliwa miezi mitatu kabla ya matukio haya alikuwa hakosi chochote.

Lakini matukio yaliokuwa yanatokea mbele ya macho yake yalikuwa tofauti kabisa na matarajio yake. Mwanadada huyu alihisi kana kwamba alikuwa kwenye ndoto .

“Nilionyeshwa sehemu ambapo ningelala kwa mwaka mmoja uliofuata. Nilipewa chombo cha chuma ambacho ningekitumia kama sahani. Hali kadhalika niligundua kuwa gerezani bafu zisizo na mlango na vyoo ambavyo vilikuwa vinatumika na makumi ya wafungwa wenzangu ilikuwa kawaida,” anasema Teresia.

“Haya ni mambo ambayo sikuwa nimezoea. Pia niligundua kuwa mfungwa kupata mwangaza wa mchana tu, ni kama kupata dhahabu. Mwangaza ulitoka kwa matundu madogo juu juu ya ukuta. Hakukuwa na kwenda nje bila ruhusa.”

Wafungwa gerezani

Maelezo ya picha,

Wafungwa wanawake wakiwa katika moja ya magereza nchini Kenya

Mwanadada huyu anasema licha ya yote aliyoshuhudia gerezani, alikuwa ahudumie kifungo na mtoto wake alikuwa amejifungua miezi mitatu iliyopita .

Kama mama alihisi kana kwamba amefeli katika majukumu yake kwa kumlea mwanawe katika mazingira ambayo hakuchagua yeye.

“Ilikuwa vigumu kwasababu sikuweza kumpatia malezi niliyokuwa nimempangia kwa uangalifu – kuanzia chakula, makao, huduma ya afya, vitu vya kuchezea na kadhalika,” Teresa anasema

Kwa muda baada ya kuanza kutumikia kifungo chake, Teresa alijihurumia mno na hakuwa anaona mwisho mzuri baada ya kuwa gerezani kwa miezi mitatu.

Mwanga akiwa gerezani

Akiwa gerezani Teresa alianza kuona hali ya kukata tamaa ya wafungwa wenzake. Baadhi yao walikuwa hawajui kusoma na kuandika. Wengine wao walikuwa na uwezo mdogo wa hata kuandika majina yao.

Na hapo ndipo alianza kujiuliza ni kwanini anasononeka na kujihurumia wakati amepata nafasi ya kuwa mtu tofauti .

“Sikuamini. Nilikuwa nikilalamikia nini? Nilikuwa nimefurahia maisha mazuri yaliyojaa fursa nzuri lakini hapa kulikuwa na wanawake ambao hawajawahi kuonja hata sehemu ya kile nilichokuwa nacho. Huo ndio ulikuwa mwamko wangu, “anasema Teresa.

Teresa akiwa na mfungwa

Maelezo ya picha,

”Wanawake waliokungwa jela wanakabiliwa na unyanyapaa” anasema Teresa

Kuanzia hapo alianza kuwafundisha wafungwa wenzake jinsi ya kusoma na kuandika, kupanga bajeti, kuhifadhi pesa na kuandika mapendekezo ya biashara.

Teresa aliondoka gerezani mnamo Novemba 2011, baada ya kuachiliwa huru miezi minne kabla ya kumaliza kifungo chake baada ya kuonesha mwenendo mzuri.

Mashtaka ya wizi yalikuwa yameondolewa mahakamani lakini hadi mwezi Februari 2013 ndipo ilipothibitishwa na Mahakama ya Rufaa, ambayo ilisema kuhukumiwa kwake hakukuwa sahihi.

“Nilifikiri kufugwa jela ndio jambo baya zaidi ambalo lingeweza kunisibu lakini nilipoachiliwa, niligundua aina nyingine ya mateso iitwayo unyanyapaa,” anasema Teresa

Kulingana na Teresa, ile hali ya mtu anayetoka kuhudumia kifungo kujaribu kurejea na kutangamana katika jamii ambayo tayari imeunda mtazamo fulani juu yake huwa ni ngumu sana. Anasema kuwa sio wengi wanaotaka kuhusishwa au kuhusiana na mtu aliyetoka kutumikia kifungo gerezani.

Jamii yake ilimpokeaje?

Kwa bahati nzuri, Teresa anaweza kutegemea familia yake lakini anasema wanawake wengi wakiondoka gerezani hukataliwa na wazazi, ndugu na jamaa wengine.

“Unakuwa kama mzigo wa ziada kwa sababu hukutoka na kitu. Wewe unakuwa wa kutegemea na, kwa hivyo, ni dhima. Tayari unaporudi kwa familia yako wao pia wana shida zao wanazojaribu kutatua . Je wataweza ya kwako wewe uliyotoka gerezani?” Teresa anasema

Japo pia mwanadada huyu alipata changamoto ya kupata ajira – hakuweza kupata kazi licha ya kuhitaji sana kipato cha kumuwezesha kuhudumia mahitaji yake ya kimsingi.

Wafungwa

Maelezo ya picha,

Teresa alitaka jamii ifahamu kuwa wanawake wanaotoka gerezani bado watahitaji kushikwa mkono

Jambo jingine ni kuwa pia ilikuwa vigumu kurudi kwenye mambo aliyokuwa anayafanya hapo zamani kabla ya kufuingwa jela.

Mara kwa mara alipojaribu kuwapigia simu marafiki wa zamani simu haikujibiwa na wala ujumbe wake kurejeshwa .

Mwanamke huyu anasema kuwa jamii isipohamasihswa vya kutosha inakuwa kana kwamba mfungwa alisahaulika na jamii inakuwa haina wakati na yeye.

Mwanzo mpya

Teresa alijikuta akivutiwa na wale ambao walijua na kufahamu kutengwa ni nini. Anakiri kuwa aligundua kwa haraka kuwa mkondo mpya wa maisha uliashiria kuwa anaanza kufanya kazi na wanawake wanaotoka gerezani na hawajui waanzie wapi.

“Niligundua haraka kuwa kwa uzoefu wangu wa elimu na ushirika, ningeweza kuwasaidia wanawake hawa. Niliichukua hali hii kama mwito wangu mpya wa maisha,”Teresa anasema.

Teresa alianza kutembelea makanisa na vikundi vya wanawake kuelezea matatizo ambayo yanawakabili wanawake gerezani.

Teresa Njoroge

Maelezo ya picha,

Teresa anahamasisha jamii kuhusu changamoto zinazowakabili wanawake gerezani

Alitamani jamii ifahamu kuwa wanawake wanaotoka gerezani bado watahitaji kushikwa mkono.

Anaamini kuwa ukosefu wa nafasi ya pili ndio unaowapeleka tena gerezani baadhi ya wanawake hawa kwani wanakuwa katika pilkapilka za kutafuta jinsi ya kukidhi mahitaji yao na hawana wa kuwasaidia .

Hali hii Teresa anaiona kama mtego mbaya wa umaskini, unaojirudia.Uhalifu unaowapelekea wanawake wasiokuwa na namna kufungwa tena na tena.

Wanawake hawa watajikuta wakifanya uhalifu mdogo wa wizi na hata ukahaba.

Hii ndio ilimfanya Teresa aanze shirika la SMIMS, (Support Me In My Shoes).

Hii ni katika hali ya kujaza hitaji la programu za huduma kwa wanawake katika magereza ya Kenya. Pia alianzisha mpango wa kuwapa wanawake fursa za kuanza maisha upya ili kuwawezesha wanawake kujimudu kwa kupitia ujasiriamali, ajira na mabadiliko ya mawazo.

Kwa msaada kutoka kwa wataalam wa kujitolea, makanisa, mashirika na wafadhili, wafungwa wa zamani wanaweza kuanzisha biashara na kupata msukumo wa kuendelea na kozi. Wanapata pia elimu ya afya na huduma.

Ndoto iliyojengewa gerezani

“Kuwa gerezani kulikuwa na mabaya yake lakini ilinipa kusudi mpya ya maisha,” Teresa anasema. “Hapo awali, nilikuwa kwenye mbio za panya kutosheleza malengo ambayo sasa ninayatambua kama ambayo yalikosa urithi. Malengo yangu yalilenga ubinafsi tu,” Teresa anaongezea

Mwanamke huyu anasema kuwa asingeingia gerezani na kuvaa viatu hivyo vya kuwa mfungwa – asingeweza kuelewa changamoto za wafungwa.

Lakini kwa sasa ndoto yake kuu ni kuona kila mwanamke anayetoka gerezani anapewa nafasi ya pili kuanza maisha yake tena iwe alikuwa mhuni au la.

Teresa pia anafanya kazi kwa pamoja na idara ya magereza nchini Kenya. Anahudumu kwenye Bodi ya Utekelezaji na anahusika katika Idara ya Urekebishaji Tabia na Ustawi.

Kutokana na juhudi zake Teresa amepokea tuzo mbalimbali.

Source link

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *