Waridi wa BBC: ‘Nilipopata hedhi kwa mara ya kwanza sikujua wa kumwambia ‘

September 9, 2020

Dakika 2 zilizopita

Jaki Maya

Maelezo ya picha,

Jaki Maya alizaliwa eneo la Mombasa na akapewa jina Jackline Njeri.

Kwa muda murefu, Jaki Maya alikuwa anaogopa sana kuwakaribia wanaume au kutangamana nao.

Hii ni kutokana na tukio alilokumbana nalo usiku mmoja akielekea chuoni kutafuta mahala pa kulala.

Ni tukio lililoendeleza msururu wa matukio ya kumvunja moyo katika maisha yake ambayo mara kwa mara yalikuwa yakimkosesha matumaini kiasi cha kujaribu kujitoa uhai.

Lakini baada ya muda, alifanikiwa kujikwamua na kuyadhibiti maisha yake.

Changamoto za kulelewa na baba

Jaki Maya alizaliwa eneo la Mombasa na akapewa jina Jackline Njeri.

Alipofika darasa la sita, mamake aliondoka nyumbani kufuatia ugomvi wa kinyumbani hivyo akasalia mikononi mwa babake.

Maisha yalibadilika ghafla kwani baba mzazi hakuwa na uzoefu wa kuwazungumzia au kuwa na muda na wao.

Baada ya muda mfupi aliamua kuwapeleka mashambani waishi na bibi yao.

“Maisha ya mashambani hayakuwa rahisi,” anaeleza Maya. “Umri wa bibi yangu tayari umesonga hivyo hakuwa na nguvu za kutuangalia sote kwani tulikuwa na binamu zangu wengine. Ilibidi kujichunga mwenyewe na kujisismamia.”

Jaki Maya

Maelezo ya picha,

Alipofika darasa la sita, mamake aliondoka nyumbani kufuatia ugomvi wa kinyumbani hivyo akasalia mikononi mwa babake.

“Changamoto nyingine ilinipata pale nilipopata hedhi mara ya kwanza. Sikujua nimwambie nani,” anasema.

Masaibu hayakumwacha kwani baada ya muda mfupi, babake alipoteza ajira huko Mombasa, na kwa hivyo ikawa hatumi hela za matumizi kama awali.

“Nilianza kutafuta vibarua ili nipate hela za matumizi yangu na dada yangu mdogo nikiwa na umri mdogo sana,” Maya anakumbuka.

Anasema kuwa tangu utotoni mwake, hajawahi kujifikiria kama mtu asiyefanikiwa hivyo hilo lilianza kumsukuma mapema sana kufanya bidii shuleni na kutafuta hela za kuwasitiri.

Alifanikiwa na kuhitimu shule ya upili lakini deni la karo ya shule lilimfanya afukuzwe na kuwa nyumbani kwa muda mrefu huku wenzake wakiendelea na masomo.

Jaki Maya

Maelezo ya picha,

Akiwa kidato cha nne alifukuzwa na kurudi nyumbani kwa sababu deni la karo ya shule lilikuwa kubwa sana

“Muda nikiwa shuleni, nilikuwa nakosa vitu vya matumizi kama vile sabuni, dawa ya meno na hata sodo,” anakumbuka Maya.

“Bahati njema kulikuwa na kundi la ushauri nasaha ambalo lilikuwa linakusanya bidhaa hizo na kuziweka kwa madhumuni ya kuwasaidia watoto wasiojiweza.”

Akiwa kidato cha nne alifukuzwa na kurudi nyumbani kwa sababu deni la karo ya shule lilikuwa kubwa sana.

Nilikaa muda mrefu hadi walimu wengine wakanitafuta na kusema, walidhani nimeolewa, kwani walikuwa wamenikosa kwa muda mrefu.

“Walizungumza na mwalimu mkuu, nikarudi shuleni kufanya mtihani wa kidato cha nne.”

Baada ya muda, babake mzazi alihamia Nairobi na akamuoa mwanamke mwingine.

Baada ya kumaliza mtihani wake Maya alijiunga nao Nairobi lakini familia mpya ya babake haikumpokea vyema.

Babake akamtafutia malazi kwa mwanadada tofauti kwani Maya hangeweza kamwe kuishi na mamake wa kambo.

“Kila mtu aliyekuwa katika nyumba hiyo alikuwa anatoka mapema kujitafutia riziki. Wengine walikuwa wanauza matunda, nguo za mitumba na kadhalika. Nilipata motisha pia na nikaanza kutafuta kazi. Nikapata kazi ya kufanya usafi kwa hoteli moja ndogo.”

Baada ya hapo Maya alijitafutia nyumba iliyojengwa kwa mabati akawa analipa kodi ya shilingi 1600 pesa za Kenya (dola 16 za Marekani).

Akaamua kuwa kazi moja haitamsitiri hivyo akatafuta kazi ya usiku ambayo ilikuwa ni kwenye kilabu cha burudani.

Tukio la kuogofya

Jaki Maya

Maelezo ya picha,

Maya alipata habari njema za kujiunga na chuo kikuu cha Kenyatta kusomea filamu na uanahabari.

Maya alipata habari njema za kujiunga na chuo kikuu cha Kenyatta kusomea filamu na uanahabari.

“Muda huo pia baba na kakangu mkubwa wakapata kibarua cha muda mfupi mjini Mombasa.

Walinilipia karo na nikaanza masomo yangu’. Nilikuwa nafanya kazi ya kuzungusha chai mchana nikipata muda na usiku bado nafanya kazi ya kilabuni.”

“Kasi ya masomo iliongezeka hivyo nikapunguza muda wa kufanya vibarua. Baada ya miezi kadhaa bila kulipa kodi nikafungiwa nyumba.”

Maya anasema anakumbuka siku hio vyema sana.

“Kulikuwa kunanyesha sana usiku huo nilipotoka kazini na kupata nimefungiwa nyumba. Niliamua kurudi chuoni baada ya kupigia watu kadhaa simu na kushindwa kufanikiwa kuwapata. Niliona chuoni nitapata usalama kwani kuna ulinzi mkali,” anasema.

Alipokuwa anatembea ghafla wanaume wawili walimvamia na kumpora na kuanza kumtishia kumbaka.

“Walininyang’anya begi langu la mkononi na simu wakanisukuma chini na kutaka kunivua nguo. Nilichukua mchanga chini na kuwarushia na bahati ukawaingia wote kwenye macho. Katika hali hio wakiwa kama wamechanganyikiwa nikakimbia mguu niponye hadi shuleni.”

Maya alipata majeraha kwenye mkono uso na miguu yake.

Tukio hili lilimtikisa sana Maya akawa anaogopa wanaume na makundi madogo madogo ya watu.

Pia masomo yake aliyakatiza muda huo kwani kibarua cha baba na kaka yake kilikuwa kimeisha.

“Kwa bahati njema, mwakilishi wa darasa letu akaniona na kunieleza kuwa anashangaa kwani anaskia ninaonekana chuoni ila simo darasani. Niliamua kumweleza ninayopitia na akaahidi kunisaidia,” anasema.

Jaki Maya

Maelezo ya picha,

Maya alitoa kibao chake cha kwanza cha muziki mwaka uliopita na sasa anazidi kushughulikia safari yake hii ya kuwa mwanamuziki wa nyimbo za injili.

“Nikiwa kwake, rafiki yake alinielekeza jinsi ya kupata kazi kwa kampuni ya kusafirisha chakula jijini na nilipotuma maombi yangu wakaniandika kazi.”

Kujitosa kwenye muziki

Maya alijikakamua toka muda huo, huku akiweka akiba ya anachopata na kujisitiri na hata kuisaidia familia yake.

Katika pita pita zake, alipatana na rafiki yake waliyekuwa shule naye ambaye anafanya shughuli za muziki. Baada ya kutazama kwa muda jinsi muziki unavyoundwa akapata msukumo wa kujaribu.

Alitoa kibao chake cha kwanza mwaka uliopita na sasa anazidi kushughulikia safari yake hii ya kuwa mwanamuziki wa nyimbo za injili.

“Ingawa wazazi wangu hawako pamoja, uhusiano wao sio mbaya sasa na hata dada yangu mdogo sasa anaishi na mama yangu mjini Mombasa,” anasema.

Msongo wa mawazo

“Mara ya kwanza nilitaka kujitoa uhai baada ya mamangu kutuacha peke yetu. Nilijihisi kuwa peke yangu na nikaingia tu chumbani nikilia kama nimeshikilia kisu cha jikoni tayari kujidunga. Niliitwa na baba ambaye hakujuwa nilipokuwa na nikashtuka nikaangusha kisu hicho na kutoka chumbani ,” anaeleza.

Alipofukuzwa kwa kukosa karo akiwa kidato cha nne na kukaa muda mrefu bila masomo, alihisi kama dunia imemgeukia, akaingia chumbani na kufunga kamba kwa mbao za paa.

Jaki Maya

Maelezo ya picha,

Anamshauri mtu yeyote yule ambaye huenda amepitia kisa kama hiki kutoogopa kukizungumzia.

Lakini akiwa kaika harakati ya kujitoa uhai alimkumbuka dadake mdogo na jinsi atakavyomuacha na shida nyingi.

“Tukio la wanaume wawili kutaka kunibaka liliniacha na hofu moyoni kiasi kwamba ninapoona mtu tu wa kawaida, naona kama yuko karibu nami sana na anataka kunifanyia tendo baya,” anasema.

“Bado siamini marafiki ninaowapata pia kwani nahisi tu huenda wakanigeuka na kutaka kunifanyia uovu.”

Anamshauri mtu yeyote yule ambaye huenda amepitia kisa kama hiki kutoogopa kukizungumzia.

“Unapopata mtu ambaye unamwamini, unamueleza na kuhisi kama mzigo mkubwa ulio kwa mabega yako umeondolewa.”

Source link

,Dakika 2 zilizopita Chanzo cha picha, Jaki Maya Maelezo ya picha, Jaki Maya alizaliwa eneo la Mombasa na akapewa jina…

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *