Waridi wa BBC : Milicent Kagonga azungumzia alivyotorokwa na mume wake kutokana na harufu mbaya mwilini

October 7, 2020

Saa 5 zilizopita

Milicent Kagonga azungumzia alivyotorokwa na mume wake kutokana na harufu mbaya mwilini

Maelezo ya picha,

Milicent Kagonga azungumzia alivyotorokwa na mume wake kutokana na harufu mbaya mwilini

Onyo: Simulizi hii ina maneno makali ambayo yanaweza kushtua baadhi ya wasomaji

Milicent Kagonga alianza kutokwa na damu kuliko kawaida kwenye sehemu zake za siri akiwa na miaka 20. Damu ilikuwa inamtiririka kutoka mwilini mwake kila siku.

Haikuwa hedhi ya kawaida ya wanawake, ila damu iliyoandamana na uchungu mwingi. Damu hii iliandamana na uvundo wa aina yake na kufanya chumba chao kidogo kutokalika.

Alivumilia hali hii kwa muda mrefu.

“Nakumbuka siku nyingi nilikuwa ninaketi juu ya ndoo kubwa kwani ndiyo tu ingeweza kuhimili kiasi cha damu iliyokuwa inanitoka” Milicent anasema .

Alipotafuta matibabu, alielezwa tu ni maambukizi ya kawaida ambayo huathiri wanawake katika sehemu zao za uzazi.

Mwanzoni alipewa dawa za kupunguza maumivu, lakini hali yake ya kutokwa na damu ilizidi kuwa baya zaidi.

Wakati mmoja, alikumbuka kuwa aliwahi kumsikia daktari mmoja akizungumza kuhusu dalili za saratani ya njia ya kizazi kwa wanawake. Alidadisi jinsi dalili alizozisikia zilivyoshabihiana na dalili alizokuwa nazo.

Alikwenda hospitalini kwanza, mwaka wa sita tangu kuanza kupata dalili.

Alipofanyiwa uchunguzi aligunduliwa kuwa na saratani ya mlango wa kizazi.

Badala ya kupata afueni, masaibu ya Millicent yalizidi.

Mumewe alikuwa tayari amemuacha. Milicent anasema pengine mumewe alikata tamaa kutokana na uvundo mbaya uliokuwa unamtoka. Alimuoa mwanamke mwingine.

Milicent Kagonga akitabasamu

Machungu, kero na hali ya mahangaiko ilimzingira Millicent asijue la kufanya.

Wakati mmoja, alifikiria kuwa uhai wake ungemtoka.

Kurudi kijijini

Wakati mume wake alipoamua kujitenga na jamii yake, Millicent alionelea ni vyema arejee kwao kijijini kutoka kwenye mtaa wa mabanda alikokuwa anaishi.

Alihisi pengine kule angepata afueni ya maisha ya kijiji yalivyo mepesi.

Millicent na wanawe walipowasili kijijini mwao, mambo yalikwenda kinyume 
cha alivyotarajia.

Hakukuwa na wa kumlaki yeye na wanawe. Jamaa zake wengi walijitenga naye. Ugonjwa wake nao ulikuwa unamzidi nguvu, damu ikimtoka kama maji.

“Kule kijijini habari zilienea kuwa ningefariki 
kutokana na ugonjwa wangu. Tetesi zilienea kuwa nilikuwa nimerogwa,” anasema

“Hakukuwa na mtu hata mmoja aliyejitolea kunisaida na pale ndipo nilipoamua kurejea tena mjini angalau kutafuta namna ya kuendeleza maisha yangu na ya wanangu.”

Milicent Kagonga wakati alipokuwa akiugua

Aliporudi mjini maisha yakawa ni ya kuomba omba angalau aweze kuwalisha watoto pamoja na kukidhi mahitaji yake ya kila siku.

Lakini maisha yaliendelea kuwa magumu zaidi. Majirani zake walikuwa na hofu kuhusu ugonjwa wake.

Mara nyingi walifunga choo na bafu ili Milicent asiitumie wakiogopa kuambukizwa.

Mara nyingi ilimlazimu mwanadada huyu kutumia choo cha karatasi kisha kutupa nje baadaye.

Kupata mfadhili wa matibabu

Katika pilkapilka zake za kuomba usaidizi hapa na pale, alikutana na msamaria mwema aliyemsaidia na kufanikisha maombi yake ya kupata matibabu.

Matibabu yenyewe yalihusu awamu tatu za tiba ya kemikali, awamu 25 za matibabu ya tibaredio na awamu nyengine za matibabu ya kuwekwa miali nururishi ndani ya mwili.

Kulingana na Millicent mara ya mwisho alipofanyiwa uchunguzi , matokeo yalionyesha kuwa seli za saratani zilikuwa zimepungua na alikuwa hayupo hatarini tena.

Milicent Kagonga anafurahia kuwa uchungu mwingi ulioandamana na kutokwa na damu ulimuondokea .

Maelezo ya picha,

Milicent Kagonga anafurahia kuwa uchungu mwingi ulioandamana na kutokwa na damu ulimuondokea .

Anafurahia kuwa uchungu mwingi ulioandamana na kutokwa na damu ulimuondokea .

Kutokana na matibabu yaliokuwa na kasi mno mwilini mwake, aliachwa akiwa tasa. Aidha, hawezi kupata hedhi.

Bado Milicent anameza dawa za kudhibiti hali ya saratani, japo hatokwi na damu wala hana uvundo pia .

Miilicent anasema kuwa ni mwanamke mmoja ambaye alikuwa anamfanyia kazi ya usafi ndiye aliyemsaidia kuchangisha fedha za kumwezesha kupata matibabu na pia kumsaidia kupeleka wanawe shuleni.

Millicent anasema amejifunza mengi kutokana na aliyoyapitia. Kama sio hatua ya mwanamke mmoja kujitolea kumsaidia pengine hangelikuwa hai.

Aliamua kuanza shirika ambalo linawaleta pamoja wagonjwa wa saratani katika maeneo ya mabanda mtaa wa Kariobangi, Nairobi. Shirika lake hufahamika kama Symbol of Hope Warriors kwa maana ya mashujaa ishara ya amani.

Milicent Kagonga

Kupitia shirika hilo Milicent na wanawake wengine hutembelea wagonjwa ambao wamezidiwa na kulemewa vitandani.

Mbali na kuwafariji, huhakikisha kuwa wanameza dawa, wanakula na pia kuwa kwenye mazingira safi.

“Niliamua kuwasaidia wagonjwa waliopo mitaa ya mabanda kwa kuwa ninaelewa jinsi ilivyo ngumu, nikikumbuka nilivyotengwa na kuachwa na watu waliokuwa muhimu katika maisha yangu. Huhisi kuwa ninaweza kuwa msaada kwa wenye wanapitia niliyoyapitia hapo nyuma,” Milicent anasema

Saratani ya mlango wa kizazi ni nini?

Kulingana na Daktari wa saratani Catherine Nyongesa Watta :

Mlango wa uzazi ‘cervix’ ni sehemu ya kizazi kati ya uke na mji wa mimba. Sehemu hii ina kazi nyingi ikiwemo kupitisha mbegu za kiume kuelekea katika mji wa uzazi na hatimaye mirija ya uzazi ili kupevusha yai. Pia, hupitisha damu ya hedhi. Ndio mlango anaopitia mtoto wakati wa kuzaliwa.

Millicent Kagonga

Maelezo ya picha,

Millicent Kagonga alikwea Mlima Kenya kama ishara ya kukwea saratani yake

Saratani ya shingo ya kizazi ni saratani inayotokea katika sehemu ya shingo ya uke ambapo seli za kansa hujiunda na kusababisha kizazi kupata madhara katika afya ya uzazi. Saratani ya shingo ya kizazi inaongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi duniani.

Wanawake wengi wanaopata ugonjwa huu huwa na chanzo kimoja au zaidi kinachojulikana kuwa na uwezo wa kuongeza hatari ya kuupata. Baadhi ni:

1.Kuanza vitendo vya ngono katika umri mdogo (chini ya miaka 16)

2.Kuwa na mahusiano ya kimwili na zaidi ya mwanaume mmoja

3.Maambukizi ya virusi vya HPV (Human papilloma virus)

4.Maambukizi ya magonjwa ya zinaa

Dalili

1.Kutokwa na damu katika tupu ya mwanamke ambayo sio ya kawaida. Damu hii inaweza kuwa matone, au damu inayotoka katikati ya mzunguko wa hedhi (yaani baada ya hedhi kabla ya hedhi inayofuata) au damu itokayo kwa mwanamke ambae ameacha kupata hedhi.

2.Kutokwa na damu baada ya kujamiana baada ya tendo la ndoa.

3.Maumivu wakati wa kujamiana.

Dalili za saratani iliyosambaa ni kama zifuatavyo

1.Kutokwa na majimaji yenye harufu ukeni kusiko kwa kawaida na maumivu ya tumbo chini ya kitovu.

2.Kupungua kwa hamu ya kula

5.Kutokwa na damu nyingi zilizozidi hedhi

Daktari anasema kuwa matibabu yatalingana na kasi ya ugonjwa lakini kuna aina za matibabu :

•Kufanyiwa upasuaji na kuondoa mji wa mimba na viungo vingine kama ovari na mirija ya uzazi

•Matibabu ya tibakemikali ili kuongeza muda wa kuishi

•Matibabu kwa njia ya mionzi ili kuua seli za saratani.

•Kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu mara kwa mara.

•Kupata chanjo dhidi ya virusi vya HPV kabla ya kuanza vitendo vya ngono.

Source link

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *