Wanawake wa Dalit ni miongoni mwa watu wanaokumbwa na unyanyasaji zaidi duniani

October 11, 2020

Dakika 4 zilizopita

Dalit women

Maelezo ya picha,

Wanawake wa Dalit wanaonyanyaswa zaidi duniani

“Sisi ni waathirika wa ghasia kwasababu ni masikini, wanawake wa daraja la chini, kwahiyo tunadunishwa na wote,” Mwanamke wa Dalit alimwambia mtafiti Jayshree Mangubhai miaka kadhaa iliyopita.”

“Hakuna wa kutusaidia au kuzumnguza nasi. Tunakabiliana zaidi na dhuluma za kingono kwasababu hatuna nguvu yoyote.”

Wiki iliyopita, inasemekana kwamba mwanamke wa Dalit, 19, alibakwa na genge la wahalifu na kushambuliwa na kundi la wanaume wa tabaka la juu kutoka jimbo la Uttar Pradesh kwa mara nyingine tena.

Taarifa hizo zinaonesha tena kusambaa kwa dhuluma za kingono kunakowakabili karibu wanawake milioni 80 wa Dalit nchini India na kama tu waume zao ambao nao pia wanawachukuliwa kuwa wa tabaka la chini kabisa.

Wanawake hawa ambao ni karibu asilimia 16 ya idadi ya wanawake nchini India, wanakabiliana na “mzigo mara tatu” wa ubaguzi wa kijinsia, kunyanyapaliwa na ukosefu wa mahitaji ya msingi.

“Wanawake wa Dalit wanatoka katika kundi linalonyanyaswa zaidi duniani,” alisema daktari Suraj Yengde, mwandishi wa kitabu cha ‘Caste Matters’.

“Ni muathirika wa utamaduni, na unyanyasaji wa taasisi, ndani na nje. Na hili linajitokeza katika dhuluma ambazo wanawake wa Dalit wamekuwa wakizipitia miaka nenda rudi.”

Matokeo ya ubakaji uliotokea hivi karibuni na mauaji ya mwanawake wa Hathras, huko Uttar Pradesh, yanayosemekana kutekelezwa na wanaume wa tabaka la juu, kulionesha hali inayoshuhudiwa pale mwanamke wa Dalit anaposhambuliwa:

Polisi wamerekodi malalamishi kwa kasi ya polepole; wachunguzi huchukua muda mrefu; maafisa huanza kushuku ikiwa kweli ubakaji umetokea; kuna dhana kwamba hilo halina uhusiano wowote na tabaka; na mamlaka huonekana kuunga mkono tabaka la juu ambao ndio watendaji wa dhuluma hizo.

Hata baadhi ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na wanahabari wa tabaka la juu, huhoji kwanini dhuluma za kingono zinahusishwa na tabaka.

Kwa maneno mengine, jimbo na sehemu ya jamii nchini India hupanga njama ya kutotilia maanani au kuondoa uhusiano kati ya dhuluma za kingono na mfumo wa matabaka kuanzia na wanaochukuliwa kuwa watawala.

Dalit women

Maelezo ya picha,

Inakadiri kwamba kuna wanawake milioni 80 wa Dalit kote nchini India

Baada ya kilichodaiwa kuwa ubakaji wiki iliyopita, serikali ya Utta Pradesh, ambayo inatawaliwa na mwanasiasa wa tabaka wa juu wa chama tawala cha BJP, kwa haraka sana walichoma mwili wa mwathirika usiku wa manane, na kukataza vyombo vya habari na wanasiasa wa upinzani kutembelea kijiji cha waathirika na familia, na kuzua wasiwasi kuwa wanataka kuuficha ukweli.

Katika hatua ambayo haijawahi kutokea hapo kabla, serikali ilichukua hatua ya kutafuta shirika la binafsi la uhusiano mwema ili kuendeleza ajenda yake kwamba tukio hilo halikuwa ubakaji.

Wanawake wa Dalit kote katika maeneo ya vijijini ya India wamekuwa waathirika wa dhuluma za kingono tangu walipoanza kujitambua.

Katika maeneo hayo, ardhi nyingi, rasilimali na nguvu katika jamii ni vya matabaka ya juu na ya wastani.

Licha ya sheria ya mwaka 1989 yakuzuia ukatili dhidi ya jamii, hakuna kilichofanywa kupunguza madhila kama hayo dhidi ya wanawake wa Dalit.

Waliendelea kunyanyapaliwa, kunyanyaswa, kushambuliwa, kubakwa na kuuawa kwa kupewa adhabu kali.

Wanawake 10 wa Delit walibakwa kila siku nchini India mwaka jana, kulingana na idadi rasmi iliyotolewa.

Jimbo la Kaskazini mwa Uttar Pradesh ndio linaloongoza kwa idadi ya juu ya matukio dhidi ya wanawake pamoja na idadi ya juu ya visa dhidi ya unyanyasaji ya kingono kwa wasichana.

Majimbo matatu – Uttar Pradesh, Bihar na Rajasthan – yaliripoti zaidi ya nusu ya matukio ya ukatili dhidi ya wanawake wa Dalit.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2006 kuhusu wanawake wa Dalit katika majimbo manne kote nchini India kuangalia aina ya dhuluma ambazo wamekumbana nazo, asilimia 54 wameshambuliwa kimwili; asilimia 46 wamenyanyaswa kingono; asilimia 43 wamekabiliana na dhuluma za ndani ya nyumba; asilimia 23 wamebakwa’ na asilimia 62 wametukanwa kwa maneno.

Indian activists protest against an alleged gang rape of a 19 years old Dalit woman in Uttar Pradesh state, in Bhopal,

Maelezo ya picha,

Kumekuwa na maandamano kote nchini humo yanayopinga ubakaji wa msichana wa Dalit mwenye umri wa miaka, 19.

Na wanawake wa Dalit ndio wanaopitia dhuluma zote zinazotekelezwa na matabaka mengine likiwemo la kwao.

Kituo cha kundi la kutetea haki za wanawake wa Dalit kilitathmini matukio 100 ya dhuluma za kingono dhidi ya wanawake na wasichana wa Dalit katika maeneo 16 nchini India kati ya mwaka 2004 na 2013.

Kituo hicho kilibaini kwamba asilimia 46 ya waathirika walikuwa na umri wa chini ya miaka 18 na asilimi 85 walikuwa cha chini ya miaka 30. Waliotekeleza dhuluma hizo walitoka katika matabaka 36 tofauti tofauti ikiwemo tabaka la Dalit.

Moja ya sababu kwanini Wadalit – hususani wanawake – wanapitia matukio chungu nzima ya unyanyasaji ni kwamba wameanza kuzungumza na kujitetea.

Mabadiliko ya historia ya dhuluma dhidi ya wanawake wa Dalit nchini India ni mwaka 2006, pale watu wanne wa familia ya Dalit – mwanamke, binti yake, 17, na vijana wake wawili – walipouawa kinyama na kundi la wanaume wa tabaka la juu baada ya kutokea kwa mgogoro wa umiliki wa ardhi.

Mgogoro huo ulitokea katika kijiji kinachofahamika kama Khairlanji jimbo la Maharashtra na ulianza na wanawake wawili waliokwenda kufungua kesi polisi juu ya mzozo wa kipande cha ardhi wakilalamikia watu wa tabaka la juu katika kijiji chao.

“Tukio hilo lilichochea dhamira ya Wadalit na kuanza kuangazia mateso ya kijamii hiyo na unyanyapaa ambao wamekuwa wakiupitia,” amesema mwanahistoria Uma Chakravarti.

Tabaka la juu limetingishwa na madai ya Wadalit ambayo yamekuwa yakiongezeka na kutaka kulipiza kisasi.

Katika kesi ya Hathras iliyofanyika majuma kadhaa yaliopita, taarifa zilionesha kwamba familia za waathirika wamekuwa na mzozo kwa kipindi cha miongo miwili na familia ya tabaka la juu.

Kote nchini humo, mabadiliko ya kijamii yanawapeleka wasichana Wadalit shuleni na kushinikiza wanawake wa Dalit na makundi ya kutetea haki za wanawake kupaza sauti zao.

“Ikiwa ni jambo geni kabisa, wanawake walio uongozini hukusanya malalamishi yao na kupambana bila usaidizi kutoka kwa yeyote,” amesema Dkt Yengde.

Wanawake wa Dalit wameamua kupigana haki yao. Na inaonekana ukosoaji umekuwa wa juu kuliko wakati mwingine wowote.

“Awali, vita hivyo havikuwa vinaonekana wala kuripotiwa,” amesema Manjula Pradeep, kiongozi wa Dalit ambaye ni mwanaharakati. “Sasa tunajua kile kinachoendelea.

Tuko imara zaidi na wenye kujiamini. Sasa vita vikubwa ni kutukumbusha mipaka yetu.”

Source link

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *