Wakulima Bonde la Ruvu kutumia Matrekta,

October 8, 2020

Na Omary Mngindo, Mlandizi

WAKULIMA katika bonde la Mto Ruvu Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, wanataraji kunufaika na kilimo cha mpunga kwa kutumia matrekta pamoja na pembejeo mbalimbali.

Hayo yameelezwa na mgombea ubunge jimboni hapa Michael Mwakamo, akizungumza na wakazi wa Madimla Kata ya Kilangalanga, ambapo alisema kuwa tayari ameshaanza kazi ya kibunge, kwa kutafuta taasisi ambayo itawalimia wananchi wanaojihusisha na sekta hiyo.

“Nimezungumza na watu wapo tayari kuja kutusaidia katika kilimo kwenye bonde la Mto Ruvu, sitaki kubahatisha walichoniambia ni kwamba bonde la Ruvu linaweza kuzalisha zaidi, ila nihakikishe nadhibiti mifugo, na kila kwenye eka kumi, tano watalima bure,” alisema Mwakamo.

Aliongeza kwamba watu hao wapo tayari kuja kuweka taasisi itayokuwa inajihusisha na masuala mbalimbali inayohusiana na kilimo, kwa lengo la kuhakikisha sekta hiyo inarudi katika hadhi yake ya miaka ya 70 mpaka 90.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Kibaha Vijijini Ludovick Remy alisema kuwa, katika eneo la Kwala linakwenda kuwa Mji Mdogo kutokana na uwepo wa Bandari Kavu, sanjali na ujenzi wa ghara litalokuwa linahifadhia mizigo inayotokea nchi mbalimbali.

“Kazi yote imefanyika ndani ya miaka mitano ya Serikali inayoongozwa na Dkt. John Magufuli, hiyo ni kielelezo tosha kwamba mgombea urais anatosha kuongezewa miaka mitano mingine ili amalizie kazi sanjali na kuanzisha miradi mingine ya kimaendeleo,” alisema Remy.

Nae mgombea udiwani katani hapo Mwajuma Denge anayetetea nafasi hiyo alisema kwamba, ndani ya Kijiji cha Madimla kuna changamoto ya kukosekana kwa zahanati, hivyo mpango uliopo ni kuhakikisha inapatikana ili kuwaondolea adha wakazi hao.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *