Wakili: Ndoa ya kudhaniwa ni ndoa kama nyinginezo,

October 3, 2020

 

Wakili Edson Kilatu akiwa katika kipindi cha SuperBreakfast cha East Africa Radio amesema kuwa kumekuwapo na kasumba kwa baadhi ya wanaume kuishi na wanawake kwa zaidi ya miaka miwili na kuwaacha huku wakioa wanawake wengine licha ya ahadi kedekede wanazokuwa wametoa hapo awali.

Ameitaja hatua hiyo kuwa ni kosa kisheria kutokana na sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 160 kutambua ndoa dhaniwa, ambayo uhalali wake hufikiwa pale wenza wanapokuwa wameishi kwa miaka miwili pamoja katika mazingira yanayowafanya kuonekana na kudhihirika kama mke na mme.

“Sheria yetu ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 160 inatambua ndoa ya kudhaniwa (Presumption of marriage), sheria hii inamlinda mwanamke au mwanaume ambaye amekaa na mwenza wake kwa miaka 2, na yawepo mazingira ambayo hata majirani na watu wanaowazunguka waone na kujiridhisha kuwa wahusika ni mke na mume” Wakili msomi, Edson Kilatu.

Aidha Kilatu ameongeza kuwa  katika mazingira ambayo mmoja kati ya wenza husika hayupo tayari kuikubali ndoa dhaniwa, sheria inamruhusu  kuthibitishia mamlaka husika juu ya mazingira ambayo yataweza kutoa picha halisi.

”Mwenye jukumu la kuithibitishia Mahakama kuwa ndoa ya kudhaniwa haipo ni yule mwenza anayekataa kuwa hakukuwapo uhusiano wa mke na mume katika kipindi chote ambacho aliishi na mwanamke au mwanaume husika” ameongeza Kilatu.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *