Wadau wa TAFICO watakiwa kuja na mapendekezo ya aina ya vifaa vya meli ya uvuvi vitakavyo faa kutumika,

October 2, 2020

 

Wadau wa  Shirika la Uvuvi (TAFICO) wametakiwa kujadili na kurudi na mapendekezo ya aina ya vifaa vya uvuvi, hasa vitakavyotumika katika ujenzi wa meli ya uvuvi itakayomilikiwa na shirika hilo kwa niaba ya serikali.

Agizo hilo lilitolewa jana ( tarehe 01102020) na mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Emmanuel Bulayi  wakati anafungua kikao  cha wadau hao kilichowahusisha washiriki kutoka kampuni za uvuvi, TADB, THA, DMI, FETA, TAFIRI, TASAC, Menejimenti ya TAFICO, Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu na wawakilishi wa Idara ya Uvuvi.

 Bulayi ambaye alimuwakilisha katibu mkuu wa uvuvi  katika kikao hicho cha wadau alisema serikali ya Tanzania ilishatiliana saini na serikali ya Japan mkataba wa kuanza utekelezaji wa programu ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii utakaosaidia ununuaji wa vifaa vya uvuvi ikiwa ni pamoja na meli moja ya uvuvi.

“Kwa kuwa taratibu za awali zilishakamilika ambapo tayari mkandarasi kwa ajili ya kununua vifaa hivyo ameshapatikana CROWN AGENT kutoka Japan, kinachosubiriwa ni sisi kuja na mapendekezo ya aina ya vifaa vya uvuvi tunavyotaka vinunuliwe na mkandarasi huyo,” 

“Serikali katika suala hili imeona ni vema wadau

 wakashirikishwa ili na wao waweze kutoa ushauri wao kutokana na uzoefu walionao ili vifaa hivyo vitakapoagizwa viweze kukidhi mahitaji kama ilivyokusudiwa. Kwahiyo ni muhimu majadiliano haya yatakapokamilika, orodha ya vifaa hivyo iweze kujulikana,” aliongeza Bulayi.

Naye Kaimu Meneja Mkuu TAFICO, Bi. Esther Mulyila alisema lengo la kikao hicho ni kujadili aina ya vifaa vya uvuvi vitakavyonunuliwa kwa ajili ya meli ya uvuvi, majokofu kwa ajili ya kuhifadhia samaki na mtambo wa kuzalishia barafu.

Alisema TAFICO kwa sasa itatekeleza majukumu yake pamoja na miradi 10 yenye thamani ya shilingi bilioni 89.8 itakayokuwa inatekelezwa kwa awamu, ambayo itashirikisha wadau. 

Miradi hiyo imegawanyika katika maeneo matatu, kwanza ni miradi ya uvuvi kwa kutumia meli za aina 3 za uvuvi kwa ajili ya uvuvi wa maeneo matatu ya bahari, mradi wa mtambo wa kuzalisha barafu, mradi wa majokofu ya kuhifadhia samaki, mradi wa viwanda vya uchakataji samaki, miradi ya ukuzaji viumbe maji (uzalishaji wa vifaranga vya samaki, uzalishaji wa vyakula vya samaki, ufugaji wa samaki kwenye vizimba na ufugaji wa samaki kwenye mabwawa). 

Alibainisha kwamba serikali inaendelea na mchakato wa ufufuaji wa shirika lake la TAFICO. Ambapo imepata msaada kutoka serikali ya Japan wa Yen Milioni 200 ambazo ni takriban shilingi za kitanzania Bilioni 4.2 kupitia programu ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii.

Mulyila alivitaja baadhi ya vifaa vitakavyonunuliwa kupitia programu hiyo kuwa ni meli moja ya uvuvi, majokofu ya kuhifadhia samaki na mtambo wa kuzalisha barafu.

  Alisema kwaupande wake serikali ya Japan itanunua, itasafirisha, itasimika mitambo katika eneo la Ras Mkwavi na kufundisha juu ya matumizi ya mitambo hiyo.

Madhumuni ya kikao hicho yalikuwa ni kujadili vigezo mbalimbali vitakavyowezesha kupatikana mapendekezo ya aina ya vifaa vya uvuvi vya TAFICO vitakavyo nunuliwa kupitia ufadhili wa nchi ya Japan.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *