Umoja wa Mataifa waitaka Mali kuheshimu mkataba wa amani,

October 1, 2020

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameitolea wito serikali ya mpito nchini Mali kuheshimu makubaliano ya amani ya mwaka 2015, kwa ajili ya kurejesha utulivu kwenye taifa hilo la magharibi mwa Afrika. 

Wito huo umo kwenye ripoti iliyowasilishwa mbele ya Baraza la Usalama, ambayo inautaja mkataba huo wa amani kama njia pekee ya kuhakikisha mageuzi ya kitaasisi. 

Makubaliano ya amani yalisainiwa na rais aliyeondoshwa madarakani na jeshi, Ibrahim Boubacar Keita, kwa lengo la kuwanyang’anya silaha waasi na kuwaingiza kwenye jeshi la taifa. Hata hivyo, utekelezaji wake umekuwa ukisuwasuwa kwa miaka kadhaa sasa. 

Kundi la wanajeshi lilimuondoa madarakani mwezi uliopita na wiki iliyopita likamtangaza waziri wa zamani wa ulinzi, Bah Ndaw, kuwa rais mpito. 

Tayari Kanali Ndaw amemteuwa waziri wa zamani wa mambo ya kigeni, Mokhtar Ouane, kuwa waziri mkuu. 

Kuteuliwa kwa waziri mkuu huyo kunafunguwa njia ya kuondolewa vikwazo vilivyowekwa na mataifa jirani, wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *