Uhusiano kati ya Tanzania na Malawi umekuwa ukigubikwa na mambo makubwa matatu katika kipindi cha miaka 50 iliyopita

October 7, 2020

Saa 4 zilizopita

Rais Chakwera wa Malawi na John Pombe Magufuli wa Tanzania

Maelezo ya picha,

Rais Chakwera wa Malawi na John Pombe Magufuli wa Tanzania

MIEZI mitatu kabla hajaondoka madarakani mwaka 2005, Rais Benjamin Mkapa wa Tanzania alipokea ujumbe wa maandishi kutoka kwa mwenzake, Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi.

Mmoja wa viongozi waandamizi katika serikali ya Awamu ya Nne aliyezungumza na mwandishi wa makala hii kwa masharti ya kutotajwa majina yake, alisema Rais Mutharika alikuwa anapendekeza kwa Mkapa kuhusu kuundwa kwa tume maalumu ya nchi hizo mbili itakayoshughulika na mgogoro wa mpaka baina ya nchi hizo jirani.

Rais Mkapa, kwa busara zake, akaamua kwamba jambo hilo aliache kwa mrithi wake; ambaye aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kwa miaka yote kumi ya utawala wa Awamu ya Tatu, Jakaya Kikwete.

“Hata hivyo, kwa sababu ambazo hazijulikani, wasaidizi wa Kikwete hawakumpa ujumbe huo mpaka takribani miaka mitatu baadaye. Ujumbe ule ukajibiwa kwa maandishi kwenda kwa Mutharika,” alieleza kiongozi huyo.

Lakini, Tanzania nayo haikujibiwa ujumbe huo hadi miaka minne baadaye. Rais Mutharika, wakati huo akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, akaamua kwamba nchi za Kiafrika ziunde chombo cha kushughulika na migogoro ya mipaka. Wataalamu wa Tanzania na Malawi wakakaa na kukubaliana kwenye mambo ya msingi kuhusu mpaka huo.

Hata hivyo, wakati Mutharika alipofariki dunia na nafasi yake kuchukuliwa na Joyce Banda mwaka 2014, serikali mpya ikaanza kuja na mawazo mapya. Katika mojawapo ya vikao vya majadiliano, mmoja wa wajumbe kutoka Malawi alihoji kuwa hao waliokuwa wakijadili mambo makubwa namna hiyo “walipata wapi” mamlaka hayo.

Hiyo ndiyo hadithi ya miaka 15 iliyopita ya uhusiano wa Malawi na Tanzania. Haya ndiyo mazingira ambayo Rais mpya wa Malawi, Lazarus Chakwera, anajikuta nayo wakati wa ziara yake ya kwanza nchini Tanzania inayoanza Oktoba 7, mwaka huu.

Tatizo la miaka 130

Uhusiano baina ya Tanzania umekuwa ukigubikwa na mambo makubwa matatu katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Kwanza ni mgogoro wa mpaka baina ya nchi hizo za Kusini mwa Afrika ambao chanzo chake ni mkataba wa kikoloni baina ya Wajerumani na Waingereza wa mwaka 1890, unaojulikana kwa jina la Heligoland.

Katika mkataba huo, mpaka baina ya Tanzania na Malawi unadaiwa kuanzia linapoishia Ziwa Nyasa kwa upande wa Tanzania – ikimaanisha kuwa ziwa hilo la nane kwa ukubwa duniani, lote ni mali ya Malawi.

Mkataba huo wa kikoloni ni tofauti na Sheria za Kimataifa zinazotambua mpaka wa majini baina ya nchi huanzia katika kina kirefu zaidi cha maji; mara nyingi katikati ya maji – ambayo tafsiri yake inaweza kuwa kwamba nusu ya ziwa linatakiwa liwe Tanzania na nusu nyingine kwa Malawi.

Chakwera

Hili ndilo jambo ambalo viongozi wa juu wa nchi hizi mbili wanatakiwa kulitafutia ufumbuzi wa kudumu na tayari kuna mapendekezo kuwa wananchi wote wanatakiwa waendelee kulitumia kwa pamoja kama ilivyo sasa.

Tatizo la pili la nchi hizi lilihusu zaidi tofauti za kiitikadi na kitabia baina ya viongozi wawili waasisi wa mataifa haya. Viongozi hao ni Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hastings Kamuzu Banda wa Malawi.

Ingawa wote walisomeshwa na Waingereza, walikuwa tofauti kitabia. Nyerere akipenda Ujamaa, Umajumui wa Afrika na Ukombozi. Banda alikuwa muumini wa ubepari aliyeamini kwamba wakoloni walikuwa bado wana umuhimu wa kubaki Afrika.

Kwa sababu hiyo, Banda hakuunga mkono harakati za kupambana na Makaburu wa Afrika Kusini wala wakoloni wa Ureno waliokuwa bado wanashikilia nchi za Msumbiji na Angola.

Kimsingi, Nyerere alipata kusimulia wakati fulani kuwa Banda aliwahi kumueleza kwamba Msumbiji si nchi bali ni eneo ambalo Tanzania na Malawi zinaweza kugawana.

Jambo la tatu ambalo pia lilikuwa chanzo cha migongano ya mara kwa mara baina ya Tanzania na Malawi lilikuwa uamuzi wa taifa hili la Afrika Mashariki kupokea wakosoaji wakuu wa utawala wa Banda.

Mara baada ya Uhuru wa Malawi, kulijitokeza tofauti za wazi baina ya Banda na waliokuwa wapigania Uhuru wenzake kama vile Orton Chirwa na Kanyama Chiume.

Mahasimu hao walikimbilia Tanzania kama wakimbizi wa kisiasa na mtawala huyo Malawi hakuwahi kumsamehe Nyerere na serikali yake kwa kuwapokea wanasiasa hao aliowachukulia kama maadui.

Upande mzuri wa Tanzania na Malawi

Ingawa inaonekana kuna migogoro katika ngazi za juu a serikali na miongoni mwa watawala wa mataifa haya, wananchi wake hawajawahi kuwa na tatizo na uhusiano uliodumu kwa karne nyingi.

Kwa mfano, wazazi wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, walitokea Malawi ambako kuna Waislamu wengi walikwenda katika visiwa hivyo kujifunza Uislamu.

Hadi leo, katika duru za Kiislamu za Malawi, kuna mashekhe mashuhuri na wanazuoni wengine wanaozungumza Kiswahili fasaha kwa sababu walikuja Zanzibar kujifunza dini; wakifunzwa na mwanazuoni wa Kiislamu mashuhuri wa Kizanzibari, Sheikh Saleh Farsy.

Wanasiasa wengine mashuhuri wa Tanzania wakati wa Uhuru kama vile Oscar Kambona, Michael Kamaliza na Askari Kama Alexander Nyirenda – wote walikuwa ama wana wazazi ambao asili yao ni Malawi.

Ingawa lugha mashuhuri ya Wamalawi ni Kichewa, kuna maeneo maarufu yamepewa majina ya Kiswahili; likiwapo soko maarufu lijulikanalo kama Soko la Mataifa.

Maelfu ya Watanzania wanaendesha maisha yao nchini Malawi na vivyo hivyo kwa Wamalawi ambao wanaendesha maisha yao nchini Tanzania.

Katika miji ya mipakani, biashara za mipakani zimeshamiri kiasi kwamba wananchi wa nchi hizo wamezoea zaidi bidhaa kutoka ugenini kuliko zile zinazotengenezwa nchini mwao.

Magufuli na Chakwera

Ziara ya siku tatu ya Chakwera nchini Tanzania inatarajiwa kuzimua upya uhusiano baina ya majirani hao wanachama wa Umoja wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Wawili hawa ni wapya katika ulingo wa siasa za kimataifa na mtindo wao wa kufanya siasa ni kuangalia maslahi zaidi kuliko siasa. Inatarajiwa kuwa majadiliano kuhusu biashara ndiyo yatapewa nafasi zaidi kuliko vitu vingine.

Pamoja na migogoro ya nyuma, Malawi ni mojawapo ya nchi chache duniani ambazo zimepewa ardhi Tanzania kwa sheria ya Bunge katika eneo la Bandari ya Dar es Salaam. Eneo hilo hadi leo linajulikana kwa jina la Malawi Cargo Center.

Huu ni mwanzo mzuri wa biashara kwa sababu Malawi haina bandari na inategemea nchi kama Tanzania kwa ajili ya kusafirisha mizigo yake inayotumia njia ya maji.

Chakwera alipoapishwa kuwa rais wa Malawi

Kwa vyovyote vile, kazi kubwa zaidi ya Magufuli na Chakwera, itakuwa ni kumaliza utata wa suala la mpaka baina ya nchi hizo mbili; suala lililoanzishwa na Mkapa na Mutharika ambao sasa ni marehemu.

Namna pekee ya kuwaenzi marehemu hawa – na huo ndiyo wajibu mkubwa wa viongozi hawa wanaokutana Dar es Salaam wiki hii ni kumaliza mgogoro na kujenga misingi imara ya ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi miongoni mwa wananchi masikini wa nchi hizi mbili.

Source link

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *