Uchaguzi Tanzania 2020; Je ni changamoto gani zinazowakabili wagombea wa urais Tanzania

September 9, 2020

  • Na Markus Mpangala
  • Mchambuzi Tanzania

Dakika 3 zilizopita

tume ya taifa ya uchaguzi

Wagombea 15 wa vyama vya siasa nchini Tanzania wanashiriki kampeni za kuwania urais zilizozinduliwa Agosti 26 na kunadi sera na vipaumbele vyao kwa wapigakura kuelekea siku ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu wa 2020, lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali binafsi,vyama wanavyoviwakilisha.

Uwezo wa fedha, usawa katika vyombo vya habari, hotuba, fursa, mchakato wa katiba, ajira, hali ya usalama wa viongozi, mitego ya uchochezi, ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wagombea wote, huku watatu kutoka vyama vya ACT Wazalendo,CCM na Chadema wakiwa gumzo kuliko wengine 12 wanaoshiriki uchaguzi huo.

Bernard Membe (ACT Wazalendo) amezindua kampeni zake akiwa mkoani Lindi, wakati John Magufuli (CCM) alizindua jijini Dodoma na Tundu Lissu (Chadema) alizindua katika viwanja vya Mbagala Zakheim jijini Dar es salaam.

Uwezo wa fedha wa vyama

wafuasi wa CCM

Wagombea wa vyama vyote 15 katika kiti cha urais wana uwezo tofauti wa kifedha kufanya kampeni na kuwafikia wapigakura. Uhaba wa fedha ni changamoto zinazowakabili wagombea wa vyama vya upinzani. Ni vigumu kwa vyama hivyo kugharamia matangazo ya runinga moja kwa moja.

Vyama vya upinzani haviwezi kugharamia safari za waandishi kutoka vyombo vya habari mbalimbali mfano runinga,redio na magazeti waweze kuripoti habari zao. Mathalani, Chadema wameweka matangazo mitandaoni kuomba harambee kwa wanachama na watanzania kumchangia mgombea wao Tundu Lissu ikiwa ni njia ya kutunisha mfuko wa fedha za kampeni za chama hicho.

Hali hiyo ni tofauti na CCM ambacho kimegharamia matangazo ya moja kwa moja kwenye runinga mbalimbali nchini. Pia waandishi kutoka vyombo vya habari mbalimbali wanaripoti taarifa za CCM na mgombea wake kuliko wengine. Pengo hilo limechangiwa na hali duni ya kifedha kwa vyama vya siasa hivyo kutegemea hisani ya wadau wa siasa na utawala bora.

Je hotuba zao zikoje?

Wataalamu wa masuala ya uandishi wa hotuba wanasisitiza vigezo vikuu vitano muhimu; misemo yenye kusisimua zaidi, uwezo wa kushawishi hadhira juu ya jambo, usanifu wa hoja,ubunifu, uwezo wa kutumia lugha kwa ufasaha zikiwemo za nchi ambazo wagombea wanafanya kampeni kama vile Kiswahili, Kiingereza, Kijapan, Kichina, Kijerumani au yoyote inayofahamika kwa hadhira husika.

Aidha, wanasisitiza kuwa wagombea wanatakiwa kuwa na takwimu juu ya maeneo wanayofanya kampeni, mathalani ugonjwa, utamaduni ama lolote linalohusu kijiji,Kata,Tarafa,Wilaya,Mkoa, kanda na kadhalika. Katika eneo hili ndilo wagombea wanatakiwa kubadili upepo wa kisiasa ili uvume upande wao.

Tangu kuzinduliwa kampeni hali imekuwa tofauti katika hatua za mwanzo hizi wagombea wamekuwa wakizungumzia sera zilizoko nje ya Ilani pamoja na kuyumba kutoka kwenye msingi wa kutafuta kura kwa ushawishi wa hoja.

Wafusia wa upinzani nchini Tanzania
Maelezo ya picha,

Wafusia wa upinzani nchini Tanzania

“Changamoto ninayoona ni wagombea wa urais kushindwa kujikita katika Ilani zao. Wagombea wetu hawa wakiwa majukwaani huwa wanahamishwa na upepo na shangwe za watu wanaohudhuria mikutano yao, kiasi cha kusababisha wao kuongea sera nje ya ilani zao, ambayo ndio mwongozo wa chama kuomba kura. Na hii ni kutokana na wananchi kufahamu na kuelewa kuwa ndio maendeleo. Vitu kama vile hospitali,umeme,maji ndio maendeleo yenyewe kwa mtazamo wa wananchi, sasa wagombea wengi wanakutana na changamoto ya kukwepesha hili na isonekane kuwa si maendeleo. Kwenda nje ya ilani imekuwa kwa wagombea wote tuliowaona, si CCM, Chadema, ACT Wazalendo na vingine, hawazungumzi kwa kubaki kwenye mkate wa kuombea kura yaani Ilani,” amesema mwanasiasa mmoja mwandamizi wa CCM.

Miradi ya maendeleo

Waama, serikali ya CCM imetekeleza miradi ya maendeleo lakini inakabiliwa na changamoto ya kujibu swali ni wapi wameyapeleka maisha bora yaliyosimikwa na serikali ya awamu ya nne ya rais Jakaya Kikwete? Kwamba ni namna gani wanahuisha ujenzi wa miradi ya maendeleo na unafuu wa maisha ya wananchi?

Aidha, wagombea wa upinzani nao wanakabiliwa na changamoto ya kueleza ni nini watakifanya zaidi ya hiki wanachokiona kwa serikali ya CCM ambayo imetekeleza miradi ya maendeleo maeneo mbalimbali?

Mtaalamu wa Sayansi ya siasa, Cassian Mbunda, amemwambia mwandishi wa makala haya, “Mgombea wa CCM licha ya miradi mikubwa aliyotekeleza bado anakabiliwa na changamoto kwamba unafuu wa maisha kwa wananchi wa kawaida umepungua sana. Hii ni kwa watu wote mijini na vijijini ukilinganisha na awamu ya nne ya Rais Kikwete. Wagombea wa upinzani kutoka vyama vyaote wanakabiliwa na changamoto kwa kuwa Rais Magufuli ametekeleza miradi ya maendeleo ni rahisi kuielezea au inaonekana kwa urahisi machoni mwa watu. Hii changamoto kubwa kwao kuhimili vishindo lakini uthubutu wa kuomba ridhaa na mwitiko wa wananchi katika mikutano yao ya kampeni ni ishara wanasikilizwa,”

Usawa katika vyombo habari

Uchaguzi huu kwa mara kwanza wagombea wa upinzani wana fursa ndogo kwenye vyombo vya habari. Hakuna usawa katika utoaji wa habari, waathirika wakiwa ni vyama vya upinzani ambao wanakosa fursa za habari zao kutangazwa kwenye runinga, redio hata magazetini.

Vyama hivyo vimetambua changamoto hiyo na kuwekeza katika mitandao ya kijamii. Mitandao hiyo ni nyenzo mbadala ya kuwafikia wapigakura, kwa kufanya ‘Live Streaming’. Uzinduzi wa Ilani ya ACT Wazalendo mkoani Lindi umeoneshwa kupitia mitandao ya kijamii pamoja na kusambaza vipeperushi mbalimbali kuwafikia wapigakura.

Kwa upande wao CCM wametaweala zaidi kwenye vyombo vya habari, lakini hawaonekani kuwa nguvu kwenye mitandao ya kijamii licha ya kufanya jitihada za kutumia nyenzo hizo. CCM wamehodhi sehemu kubwa ya habari za kampeni za uchaguzi kwenye vyombo vya habari, huku wananchi wakiona hali hiyo na kuwafanya waanze kujieleza ni kwa namna pengo hili limejitokeza.

Mchakato wa katiba

Ilani ya CCM 2015-2020 inatamka kuendelezwa mchakato wa katiba mpya, lakini kwa kipindi cha miaka mitano Rais Magufuli hakuendeleza suala hilo kinyume cha matarajio ya sengi. Akizungumza wakati wa kufungua Bunge la 11 mwaka 2015, Magufuli aliahidi kuendeleza mchakato wa Katiba mpya. Hata hivyo, kwa sasa anaomba ridhaa ya kuchaguliwa kuongoza ngwe ya pili anakabiliwa na changamoto ya kuwaambia watanzania ni nini kilichotokea hadi mchakato wa katiba mpya ukaota mbawa.

Kwa upande wao wagombea wa upinzani Tundu Lissu anaungana na Bernard Membe ambao ilani zao zimebainisha juu ya kuendelezwa mchakato wa Katiba mpya. Changamoto inayowakabili kueleza namna gani katiba iliyopo ni kikwazo cha ustawi wa taifa hilo na kwa vipi Katiba mpya itakuwa mwarobaini wa kutokomeza maisha duni nchini humo.

Tundu lissu

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti uliofanywa na Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Twaweza nchini Tanzania ya mwaka 2017, ilionesha kuwa asilimia 67 ya watanzania wanataka Katiba mpya, huku asilimia 57 walisema toleo la mwisho la rasimu ya Katiba ya Tume ya Marekebisho ya Katiba mpya chini ya Uenyekiti Jaji Joseph Sinde Warioba lipigiwe kura na wananchi. Asilimia 48 walisema Katiba mpya haiwezi kupatikana ndani ya miaka mitatu.

Hali ya usalama wa viongozi

Chama tawala CCM kiliunda serikali mwaka 2015 baada ya kushinda kiti cha urais. Katika kipindi cha miaka mitano (2015-2015) limetokea tukio la kushambuliwa kwa risasi aliyekuwa Mbunge wa Singida mashariki na Mnadhimu wa Kambi ya upinzani Bungeni, Tundu Lissu, ambalo lilipaswa kuiamsha serikali na kuchukua hatua madhubuti ya kuimarisha usalama wa raia wake. Hata hivyo hakuna taarifa rasmi kutoka mamlaka juu ya kushambuliwa mwanasiasa huyo angalau kwa sasa. Mgombea wa CCM anatarajiwa kukabiliwa na changamoto ya kutoa majibu ya maswali ya kushambuliwa kwa mwanasiasa huyo kwa vile alikuwa madarakani akiwajibika kuongoza raia wote kwa haki.

Naye Tundu Lissu ni mgombea wa urais anaibua mjadala juu ya usalama wa viongozi. Changamoto hiyo inawakabili pia wagombea wa vyama vingine kuhakikisha wanaweka wazi sera za usalama wa raia na viongozi wao na nini watakifanya mara baada ya kushinda na kuunda serikali.

Mitego ya uchochezi

Je, mgombea atazungumza nini? Hilo ndilo swali linalowakabili washauri na wataalamu wa siasa kwenye mikutano ya kampeni ya uchaguzi mkuu mwaka huu. Miongoni mwa changamoto zinazowakabili wagombea wawili wakuu wa kiti cha urais John Magufuli na Tundu Lissu ni kuzungumza nje ya mwongozo wa hotuba. Aghalabu hotuba za Tundu Lissu zimekabiliwa na changamoto za uanaharakati. Kimsingi ameelemewa katika harakati. Hali kadhalika hotuba za Magufuli zimekuwa na sera nje ya Ilani ya chama, lugha kali zinazochangia kutovutia wasikilizaji, hasa namna ya kutamka na kuzungumza.

rais John Pombe mgufuli

Tukirejea mkutano wa kampeni wa CCM wa Septemba mosi mwaka huu uliofanyika Ikungi mkoani Singida tathmini inaonesha kuwa mgombea wa chama hicho alieleza suala la mwanasiasa mmoja kupewa kazi nyingine hivyo aachane na ndoto za urais, nalo lilikuwa nje ya hisia za wapigakura katika muktadha wa mahitaji afya,elimu,barabara,ajira na maisha bora kwa ujumla. Hivyo alikuwa nje ya mguso wa mioyo ya wapogakura.

Septemba mosi, mwaka huu kwenye viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, Tundu Lissu alionesha anavyokabiliwa na changamoto ya kuwasiliana na wapigakura. Alizungumzia suala la wakoloni wa Ujerumani kujenga reli (Tazara,Kati,Tanga-Arusha),viwanja vya ndege,bandari ya Mwanza, Kigoma, pamoja na Ikulu.

Kama tulivyoona awali mgombea anavyotakiwa kufahamu cha kuzungumza katika eneo analofanya kampeni, Lissu alitakiwa kuzungumzia uchumi wa wananchi wa Mwanza ambao ni uvuvi, biashara na kilimo. Alitakiwa kueleza namna gani atawezesha vijana wa eneo hilo katika uchumi, ikizigatiwa si wote watapata fursa ya kusoma ilani ya chama chake. Ni aina ya wagombea ambao wanahitaji timu mahiri ya washauri kwa lengo la kuwaongoza na kuwasaidia kuwa bora zaidi.

Membe

Mgombea wa ACT Wazalendo, Bernard Membe ambaye ni mwanadiplomasia, wakati wa kuzindua kampeni zake mkoani Lindi amekuwa mtulivu katika hotuba zake na anateua maneno ya kuzungumza, si mgombea wa kutoa mashambulizi wala hoja za haiba badala yake amejikita kwenye masuala muhimu ya wananchi,

Hitimisho la hoja hii ni kwamba wagombea wote wanatakiwa kuwa na lugha ya kuunganisha taifa ili kuepuka uchochezi. Lugha ambayo ni changamoto kwao, kwani ndiyo msingi wa kampeni kuonesha kuwa wao ni wanapenda umoja ambao na mshikamano miongoni mwa wananchi, bila kuwagawa wala kuchochea ghadhabu. Ni changamoto.

Ajira, uchumi na biashara

Ilani ya CCM kipengele cha 8(f) inasema kuzalisha ajira milioni 8. Ilani ya ACT wazalendo imesema itazalisha ajira milioni 10, hali kadhalika Chadema. Membe akiwa Lindi alizungumzia suala la zao la Korosho ambalo ni changamoto kubwa kwa wakulima kutolipwa fedha na Kangomba (ambao ni sawa na madalali) kuzuiwa kujihusisha na biashara hiyo.

Katika hoja hii mgombea wa CCM anakabiliwa na kibarua kigumu kuelezea sakata la biashara ya zao la korosho. Mgombea wa CCM, anatakiwa kuwaeleza wananchi wa Lindi ni namna gani atarekebisha dosari zilizojitokeza ama anatumia mfumo upi kuhakikisha wananchi wananufaika na juhudi zao za kilimo cha korosha.

Chadema wanakabiliwa na changamoto ya kueleza zaidi kipengele cha 4(g) kuhusu kilimo hususani kwa wananchi wa mikoa ya kusini wanaotegemea zao la korosho, baada ya kushindwa kufafanua kwenye mkutano wao jijini Mwanza.

Source link

,Na Markus Mpangala Mchambuzi Tanzania Dakika 3 zilizopita Wagombea 15 wa vyama vya siasa nchini Tanzania wanashiriki kampeni za kuwania…

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *