Uchaguzi Tanzania 2020: Fahamu umuhimu wa uchaguzi wa Tanzania ndani na nje ya nchi

September 8, 2020

Dakika 5 zilizopita

Wafuasi wa chama cha CCM

Jicho la ulimwengu lipo Tanzania wakati huu ikielekea katika uchaguzi mkuu. Vyama vya kisiasa kile tawala na vile vya upinzani, vinaendelea kuchuana kwa sera katika majukwaa. Vijembe, kebehi, vituko pia vinashuhudiwa kila uchao katika majukwaa hayo. Hadi ikifika tarehe 28 Oktoba Watanzania watakuwa yameshayasikia mengi.

Joto linazidi kupanda kwani nje ya majukwaa ya kampeni kuna pingamizi dhidi ya wagombea wa nafasi mbali mbali. Bado pingamizi hazijatolewa hukumu na Tume ya Uchaguzi (NEC). Kipi kitatokea baada ya pingamizi kujibiwa? Hilo ni swali la kusubiri na kuona.

Ukiacha hilo, uchaguzi huu una umuhimu wake kwa vyama vinavyoshiriki. Pia una umuhimu hadi katika jumuiya ya Afrika Mashariki. Siasa, dhulma, uhuru, maendeleo, mivutano ni baadhi ya mambo machache kati ya mengi yaliyofunika simulizi za uchaguzi huu katika majukwaa ya ndani ya kampeni na yale majukwaa ya kimataifa.

Kwanini uchaguzi huu ni muhimu kwa vyama vya upinzani?

Mwanzoni mwa mwezi huu, Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW) limezitwika lawama mamlaka nchini Tanzania kwa kuongezeka ukandamizaji dhidi ya vyama vya upinzani na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuelekea ya uchaguzi mkuu.

Ripoti ya HRW sio ya kwanza ya aina hiyo. Katika kipindi cha miaka mitano ripoti nyingi za mashirika mbali mbali zimetoka zikielezea kuzorota kwa uhuru wa kisiasa, vyombo vya habari, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na uhuru wa mtu mmoja mmoja kutoa maoni katika mitandao ya kijamii.

Kwa kuzingatia hali ya kisiasa ilivyokuwa katika kipindi cha miaka mitano iliopita, nimemuuliza mchambuzi wa siasa, Aikande Clement Kwayu, juu ya umuhimu wa uchaguzi huu kwa vyama vya upinzani.

“Uchaguzi huu ni fursa muhimu kwa upinzani kuonesha kwamba bado upo, una nguvu na wala haujafa licha ya kubinywa tangu 2016 chini ya mfumo uitwao wa vyama vingi”.

Uchaguzi tanzania 2020

Rikodi mbaya ya uhuru wa kisiasa na kutoa maoni katika miaka mitano ya Rais Magufuli itachangia uchaguzi wa Oktoba kufuatiliwa kwa jicho la karibu zaidi na jumuiya ya kimataifa. Jinsi utakavyofanyika utatoa taswira kuhusu kule Tanzania inakoelekea katika kipindi chengine cha miaka mitano.

Kwanini uchaguzi huu ni muhimu kwa CCM?

“Tutatumia sana dola kubaki madarakani”, kauli ya Dkt. Bashiru Ally, katibu mkuu wa CCM, aliyoitoa mwezi Machi mwaka huu wakati akizungumza katika moja ya runinga nchini. Aliweka wazi azma ya chama chake kuendelea kuingoza Tanzania. Huku akivishangaa vyama vikongwe na vya ukombozi barani Afrika vilivyoshika hatamu kisha vikaondoshwa madarakani.

Wakati ndoto za wale wasioridhika na utawala wa miongo minne wa CCM tangu kiasisiwe ni kukiona chama hicho kikidondoshwa kutoka madarakani ili chama kingine kishike hatamu. Ndoto hiyo haiakisi kabisa fikra za wanachama na viongozi wa CCM wanaotaka kukiona chama chao kikiendelea kubaki kilipo.

Kauli za viongozi hao wawapo majukwaani, zinaashiria wazi kwamba wamepania kushinda kwa kishindo katika uchaguzi huu. Wanataka wingi wa kura katika nafasi ya Urais. Pia wingi wa wabunge na wawakilishi katika majimbo.

Kwanini CCM imekusudia kubeba ushindi mkubwa katika uchaguzi huu? Ni swali nililomuuliza Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mchambuzi wa masuala ya siasa na elimu, Faraja Kristomus:

“Moja, ni kuonesha umma kuwa Rais Magufuli ni kipenzi cha wengi kwa sababu ya utendaji wake. Pia, kuwa na ushindi mkubwa ni mbinu ya kutengeneza uhalali wa kushinda tena katika uchaguzi wa 2025 katika sura kuwa Watanzania bado wana imani na chama cha hicho”.

Kristomus amefafanua sababu ya tatu kwa kusema, “ushindi mkubwa pia ni mbinu ya kujisafisha na tuhuma kuwa CCM ilinunua wapinzani. Ushindi huo utasaidia kusadikisha zile kauli za walio hama kwamba walifanya hivyo kwa kuvutiwa na sera na utendaji wa Rais Magufuli”.

Machache kati ya mengi yanayopigiwa debe na chama tawala panapohusika utendaji wa Rais Magufuli, hutaja namna alivyoimarisha miundo mbinu, usafiri wa anga na bahari, vita dhidi ya ufisadi na uzembe kwa watumishi wa umma. Hivyo wanaona upo umuhimu wa yeye kuiongoza nchi kwa muhula wa pili ili aendeleze harakati zake za ujenzi wa Tanzania ya viwanda.

Sura ya uchaguzi wa Tanzania nje ya mipaka

Rais Magufuli wa Tanzania na mwenzake wa Kenya Uhuru kenyatta

Maelezo ya picha,

Rais Magufuli wa Tanzania na mwenzake wa Kenya Uhuru kenyatta

Tanzania ni muasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliofufuliwa 1999 ikiwa sasa na wanachama sita badala ya watatu, Tanzania ikiwa ndiyo kubwa miongoni mwa wanachama. Tokea uhuru wake imekuwa na umuhimu kisiasa katika kanda hiyo hasa ukizingatia mataifa wanachama Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini, yamekumbwa na migogoro na vita na kuiathiri Tanzania, mfano panapohusika na suala la kuwahifadhi wakimbizi.

Baadhi ya migogoro hiyo imezuka kwa watawala kugombea madaraka, kubadilisha mihula yao ya uongozi au raia kuanzisha uasi baada ya kuona mifumo ya kisheria haiwatendei haki. Mchambuzi wa siasa za kimataifa Mohammed Abdulrahman, anaeleza uchaguzi wa Tanzania unatoa picha gani kwa jumuiya hiyo.

“Uchaguzi huu ni mlinganisho wa mchakato wa kasi ya maendeleo ya kisiasa kati ya Tanzania na mataifa mengine ya Afrika Mashariki panapohusika kupatikana Katiba mpya, Tume huru ya uchaguzi, uhuru wa vyombo vya habari na wa kutoa maoni na nafasi sawa kwa vyama vyote vya kisiasa. Utaona Kenya sasa imepiga hatua tokea machafuko ya 2007/2008 baada ya uchaguzi mkuu, wakati kwa upande wa Tanzania kuna kasoro kadhaa na nchi imerudi nyuma katika kipindi hiki cha miaka mitano ilopita”.

Mbali ya hilo uchaguzi huu unafanyika katika kipindi ambacho nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki ziko katika migogoro ya kisiasa na kiuchumi. Rwanda na Uganda zinatuhumiana kuunga mkono makundi ya waasi yanayotishia usalama wa mataifa hayo. Kumekuwa na kuzorota kwa uhusiano wao tangu 2017.

Burundi na Rwanda hazina uhusiano nzuri tangu 2015. Ilianza baada ya Burundi kuituhumu Rwanda kuwa nyuma ya mapinduzi yaliyoshindwa ya kumg’oa madarakani aliyekuwa Rais wa taifa hilo mwendazake Pierre Nkurunziza.

Bendera za mataifa ya Afrika mashariki
Maelezo ya picha,

Bendera za mataifa ya Afrika mashariki

Uhusiano wa Tanzania na Kenya umekumbwa na mtikisiko kutokana na vita vya kibiashara. Mambo yalianza kuharibika tangu Tanzania ilipovichoma moto vifaranga vya kuku kutoka Kenya na kuishikilia mifugo ya ng’ombe kutoka taifa hilo. Janga la corona nalo limezusha msigano mpya wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.

Ukubwa wa taifa la Tanzania na nguvu yake katika jumuiya, kunatoa matarajio kwa baadhi, ya kupatikana serikali itakayo kuja kuimarisha uhusiano kati ya wanachama na kuzipatia ufumbuzi sintofahamu zinazoendelea. Kwani kuelewana ni nguzo muhimuu ya kujenga uhusiano bora wa kibiashara na kisiasa kuelekea maendeleo ya kweli.

Source link

,Dakika 5 zilizopita Jicho la ulimwengu lipo Tanzania wakati huu ikielekea katika uchaguzi mkuu. Vyama vya kisiasa kile tawala na…

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *