Uchaguzi Tanzania 2020: Changamoto na fursa kwa CCM na upinzani

October 16, 2020

  • Na Ezekiel Kamwaga
  • Mchambuzi

Dakika 2 zilizopita

Mwanamke akipiga kura Tanzania 2005

Maelezo ya picha,

Mwanamke akipiga kura Tanzania 2005

BARANI Afrika, mara nyingi, ni vigumu kwa vyama vya upinzani kushinda uchaguzi ulioandaliwa na chama tawala. Ni vigumu zaidi kushinda uchaguzi ambao mmoja wa washindani ni Rais aliye madarakani.

Haya ndiyo mazingira ambayo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT Wazalendo na vyama vingine vya upinzani vinakwenda kukutana nayo katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliopangwa kufanyika Jumatano ya Oktoba 28 mwaka huu.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeitawala Tanzania tangu Uhuru na ni miongoni mwa vyama vichache vilivyokuwa vya Ukombozi ambavyo vimebaki madarakani pamoja na changamoto na upepo wa mabadiliko ya kidemokrasia uliotokea katika nchi nyingi za Afrika.

Pamoja na ukweli huo kuhusu demokrasia ya Afrika, kuna mifano pia ya vyama vilivyofanikiwa kukitoa madarakani chama kilichokuwa kimeshika dola; mifano ikiwa katika nchi kama Malawi, Nigeria, Ghana, Cape Verde, Kenya na Zambia.

Kwa sababu hiyo, suala la upinzani kushinda katika uchaguzi wa mwaka huu si jambo ambalo mtu anaweza kuapa kwa miungu yote kwamba halitawezekana.

Mfumo wa Uchaguzi

Wanachama wa CCM

Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani unaofanyika katika muda wa chini ya wiki mbili zijazo, husimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC) kwa upande wa Muungano na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa upande wa Tanzania Visiwani.

NEC huongozwa na Mwenyekiti ambaye huteuliwa kwenye wadhifa huo na Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye katika uchaguzi huu naye ni mgombea.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, ambaye ndiye hasa msimamizi wa shughuli za uchaguzi naye huteuliwa kutoka miongoni mwa watumishi wa umma. Naye huteuliwa pia na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uchaguzi pia husimamiwa na wasimamizi wa uchaguzi ambao wengi wao ni waajiriwa wa serikali ambayo mkuu wake ni Rais John Magufuli ambaye ndiye mgombea urais wa CCM katika uchaguzi huu.

Tatizo kubwa la Afrika, na la Tanzania katika muktadha wa makala hii, ni kwamba mfumo huu wa uchaguzi wa namna hii una faida kubwa kwa mgombea aliye madarakani – hata kama ni kweli kwamba duniani kote mgombea aliye madarakani ni vigumu kushindwa uchaguzi.

Ndiyo sababu, kuna wanaoamini kwamba itakuwa vigumu sana kwa upinzani kuibuka mshindi endapo mfumo huu wa uchaguzi wa Tanzania hautafumuliwa.

Wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, kulifanyika mchakato wa kutaka kuunda Katiba Mpya ya Tanzania ambao mojawapo ya mapendekezo muhimu katika Katiba Pendekezwa, ilikuwa kwamba iundwe Tume Huru ya Uchaguzi. Kwa bahati mbaya, Katiba Pendekezwa ilikataliwa na uchaguzi huu utafanyika katika mazingira yaleyale ya mwaka 2015 na miaka mingi nyuma.

Taarifa za kitafiti katika taasisi za kimataifa zinazotazama uchaguzi wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika zinazochagua viongozi wake mwaka huu, zinaeleza kwamba suala kubwa katika uchaguzi huu si kwamba ni itikadi au mgombea yupi anapendwa zaidi bali ni kama kutakuwa na uchaguzi kwa maana ya uchaguzi ifikapo Oktoba 28.

Muungano wa wapinzani

Wafuasi wa chama cha upinzani nchini Tanzania

Maelezo ya picha,

Wafuasi wa chama cha upinzani nchini Tanzania

Uchaguzi wa mwaka huu unafuatia ule wa mwaka 2015 ambao vyama vya upinzani viliweka rekodi ya kupata asilimia karibu 40 ya kura zote zilizopigwa. Kama kuna jambo lililojidhihiri katika uchaguzi ule lilikuwa kwamba kuna mamilioni ya Watanzania ambao wanaamini katika mabadiliko.

Siri kubwa ya mafanikio ya upinzani mwaka 2015 ilikuwa kuwa na mgombea mmoja; Edward Lowassa, wa Chadema aliyeungwa mkono na vyama vya upinzani vinne vilivyoshirikiana kumnadi kwa pamoja nchi nzima.

Lowassa pia hakuwa mgombea wa kawaida. Yeye alikuwa mwanasiasa mashuhuri aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na mwenye mtandao wa wafuasi karibu nchi nzima. Faida nyingine ya Lowassa ilikuwa kwamba alitoka katika Chama Cha Mapinduzi na hivyo kulikuwa na wana CCM waliompigia kura kwa sababu walikuwa naye tangu angali chama hicho.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, upinzani una wagombea wawili; Tundu Lissu wa Chadema na Benard Membe wa ACT Wazalendo. Ingawa wawili hawa hawafanani kwa mvuto na wafuasi, uwepo wa wawili hawa katika sanduku la kura ni ushahidi kuwa wapinzani hawakuwa tayari kwa ushirikiano mwaka huu.

Miezi michache kabla ya uchaguzi huu, viongozi mashuhuri wa upinzani kama Zitto Kabwe na Maalim Seif Shariff Hamad wa ACT Wazalendo, walikuwa wakizungumzia umuhimu wa wapinzani kuwa na mgombea mmoja.

Zitto alikwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba katika ziara zake zote mikoani, alijifunza kwamba kilio kikubwa cha wananchi ni kwa upinzani kuungana na kusimamisha mgombea mmoja.

Anza mapema Vs mgombea nyota

Rais John Pombe Magufuli

Visiwani Zanzibar, kuna uwezekano mkubwa wa Maalim Seif kushinda uchaguzi kuliko Lissu kwenye uchaguzi wa Jamhuri kwa sababu moja kubwa; Maalim ameanza mapema.

Kuna sababu nyingi zinazomfanya Maalim Seif awe mgombea tishio Zanzibar na mojawapo ya sababu hizo ni ukweli kwamba huwa anaanza mapema. Wazanzibari walijua mapema kwamba Maalim atawania 1995, 2000, 2010 na hata mwaka huu walijua atagombea.

Nguvu ya Lowassa ya mwaka 2015 ilisababishwa na ukweli kwamba ilijulikana miaka mitano nyuma kwamba atawania urais. Ilijulikana mapema kwamba Lazarus Chakwera wa Malawi atawania urais wa Malawi mwaka huu na Muhammadu Buhari ilijulikana atawania urais na Goodluck Jonathan miaka mitatu kabla ya uchaguzi.

Raila Odinga wa Kenya anajulikana kwamba atawania urais wa Kenya uchaguzi ujao na hivyo ana faida ya kuanza mapema hata kama hatashinda uchaguzi ujao. Uzoefu wa chaguzi za Afrika unaonyesha kwamba washindi wanaoshinda huwa wameanza harakati mapema.

Adama Barrow wa Gambia ni mfano wa tofauti kwa sababu ya mazingira ya taifa hilo lakini kwa kawaida ni muhimu kwa mshindani kuanza na kujulikana mapema.

Lissu wa Chadema ni mgombea mashuhuri na maarufu lakini hakukuwa na uhakika kama hata atarejea nchini kwa uchaguzi wa mwaka huu. Tukio la kushambuliwa kwake mwaka 2017 nusura lihitimishe maisha yake ya hapa duniani, ya kisiasa na maisha na kurejea kwake ni kama maajabu tu.

Kama Lissu angekuwa nchini na ikajulikana kwamba atawania urais mwaka huu na angekuwa ameanza harakati mapema, huenda picha ingekuwa tofauti kidogo. Mshindani wake, Magufuli, ilijulikana miaka mitano iliyopita kwamba mwaka huu atawania tena nafasi hiyo.

Pamoja na ukweli huu, kilichotokea Gambia kwa Barrow ni somo la peke yake katika siasa za karibuni za Afrika. Baada ya miaka zaidi ya 20 ya utawala wa Yahya Jammeh, kiongozi huyu wa upinzani alikuja kushinda katika uchaguzi wakati karibu watafiti wote wakiwa hawampi nafasi katika kura za maoni.

Barrow alikuja baadaye baada ya karibu wagombea wote mashuhuri wa upinzani kuwa wamefungwa jela na Jammeh. Nyota ya Barrow ikawaka kwa sababu wale wote waliokuwa wakitaka mabadiliko walikubaliana kuwa watampigia kura mwanasiasa huyo mgeni.

Ingawa ameingia kwenye kampeni akiwa amechelewa, Lissu ni maarufu kuliko Barrow alivyokuwa kwa Wagambia wengi. Tukio la kushambuliwa kwake kwa risasi lilimtoa kutoka kuwa mwanasiasa machachari wa upinzani na kuwa mshidani halisi wa Rais Magufuli kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Kwa hiyo, ingawa kuchelewa kuanza inaweza kuwa ni hasara kiujumla, lakini kuna mazingira yamewahi kutokea hapa Afrika ambapo kuchelewa ikawa faida badala ya hasara.

Kama Adama Barrow angewahi kuingia kwenye kinyang’anyiro, huenda naye angekuwa ameishia jela kama ilivyokuwa kwa vinara wenzake wa upinzani.

Wapiga kura

Hakuna utafiti uliowahi kufanyika kueleza ni kwa sababu gani hutokea hivyo, lakini kihistoria, Watanzania huwa hawajitokezi kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi ambao Rais aliye madarakani huwa pia ni mgombea.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwisho wa Tanzania ambao Rais aliye madarakani aligombea, Jakaya Kikwete, – mwaka 2010, idadi ya wapiga kura waliojitokeza ilikuwa ni asilimia takribani 40 tu ya wapiga kura wote waliokuwa wameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Kitakwimu, katika nyakati za uchaguzi, vyama vya upinzani huwa na nafasi zaidi wakati idadi kubwa ya watu waliojiandikisha kupiga kura wanapojitokeza kupiga kura. Idadi ikiwa ndogo, kama ambavyo imekuwa kawaida kwa Watanzania wakati Rais aliye madarakani anapogombea, maana yake ni kwamba CCM itafaidika.

Hata hivyo, bado kuna uwezekano wa watu kujitokeza kwa wingi kupiga kura endapo kutatokea sababu ya kipekee ya kufanya hivyo. Kama wafuasi wa vyama vya upinzani wataona kwamba suala la kupiga kura mwaka huu ni la kufa au kupona kwa sababu yoyote inayoweza kujitokeza kati ya sasa na Oktoba 28, wapiga kura wanaweza kuwa wengi na hiyo ikawa na faida kwa wapinzani.

Rekodi zilizopo zinatuonyesha kwamba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 ambapo Benjamin Mkapa alikuwa akiomba awamu ya pili ya kuwa Rais, idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ilikuwa zaidi ya asilimia 70; ingawa wakati huo hakuwa na upinzani mkali kutoka vyama mbadala.

Kuhusu Lissu

Tundu Lissu

Kama upinzani utashinda katika uchaguzi huu, mgombea pekee mwenye nafasi hiyo ni Lissu wa Chadema. Hata hivyo, Lissu ana nakisi ambayo Lowassa hakuwa nayo mwaka 2015.

Katika hadithi za kisiasa za Kitanzania, kauli moja mashuhuri ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambayo imekuwa ikinukuliwa sana na wanasiasa ni ile iliyotabiri kwamba upinzani halisi Tanzania utatokea ndani ya chama tawala cha CCM.

Mojawapo ya tafsiri ya kauli hiyo ni kama pale ambapo Lowassa alihama kutoka CCM kwenda Chadema mwaka 2015 au Augustine Mrema alipohama kutoka CCM kwenda NCCR Mageuzi mwaka 1995. Kuhama kwao kuliendana na kuhama kwa baadhi ya wana CCM.

Kupitia Imani hiyo, huwa inaaminika kwamba ni lazima CCM ipasuke kwanza ndiyo upinzani upate nafasi. Kama ilivyokuwa nchini Kenya kwamba ilibidi chama tawala cha KANU kivunjike vipande ndipo upinzani ulipopata hasa nafasi ya kushinda uchaguzi.

Tundu Lissu hajawahi kuwa mwana CCM. Kimsingi, kutokana na kauli zake za nyuma dhidi ya chama tawala na wafuasi wake, wapo wana CCM ambao hawawezi kumpigia Lissu kura kuwa Rais wa Tanzania. Lowassa alipata kura zote za wapinzani jumlisha na za wana CCM walioamini atakuwa kiongozi mzuri.

Nakisi ya kisiasa aliyonayo Lissu ni kwamba yeye ni aina ya wanasiasa ambao ama unampenda sana au humpendi. Katika uchaguzi huu, anaweza kupata kura za kutosha kutoka kwa wapinzani lakini akapata taabu kupata kura za wana CCM na wale ambao bado hawajaamua wampigie kura nani hadi sasa.

Hata hivyo, kuna namna moja ambayo Lissu anaweza kufaidika nayo; kama Watanzania wataamua kumpa kura za huruma kutokana na madhila aliyopitia katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita au kama wakiamua kupiga kura za hasira dhidi ya chama tawala.

Kura za hasira zinaweza kusababishwa na makundi mbalimbali ya Watanzania ambao kwa namna moja au nyingine maisha yao yameathiriwa katika namna hasi na serikali ya Rais Magufuli. Hili ni kundi ambalo kwa sasa ama halijaamua kama liingie kupiga kura au la. Kunaweza pia kuwa na wana CCM wanaoona kwamba hawajafaidika na utawala wa sasa kama ilivyokuwa huko nyuma.

Kupita bila kupingwa

Hata kabla ya siku ya kupiga kura kufika, tayari CCM ina uhakika wa kupata viti vya Ubunge takribani 20 katika majimbo tofauti hapa nchini. Kwa uzoefu wa miaka ya nyuma, wapinzani hawatakuwa na uwezo wa kuweka mkazo na kulinda kura katika maeneo ambako hawatakuwa na wagombea.

Uchaguzi huu umeshuhudia wagombea wa upinzani katika majimbo kadhaa ya uchaguzi wakiondolewa katika kinyang’anyiro kwa sababu za kiufundi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hadi sasa, wapinzani wamedai kwamba hizo ni rafu na ndiyo matokeo ya kuwa na tume ya uchaguzi isiyo huru.

Kama hali ikibaki hivi hadi Oktoba 28, maana yake ni kwamba CCM itaingia katika uchaguzi ikiwa na uhakika wa kura zaidi ya milioni moja katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu; kabla hata upigaji kura haujaanza. Hakuna chama kingine cha sasa kinachoweza kusema kina uhakika wa namna hii kwenye uchaguzi huu zaidi ya chama tawala.

Kuna uwezekano pia, kwamba kitendo hiki cha wabunge kupita bila kupingwa kinaweza kuwaunganisha wafuasi wa upinzani na kuamua kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura za urais.

Kwamba wawe na dhamira ya kusema kwamba wamekosa wabunge lakini wampe mgombea urais wa upinzani kura za kutosha kuweza kushinda uchaguzi.

Hii inafanana na hoja ile ya kura za huruma na hasira. Inaweza kuwa faida ya wazi kwa chama tawala, lakini inaweza kuwa faida iliyojificha kwa vyama vya upinzani.

Source link

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *