Taasisi ya Chem Chem yatoa Gari Vilima Vitatu kupeleka Wanafunzi Shule na kuwarudisha majumbani,

October 2, 2020

Na John Walter- Babati.

Mwekezaji wa sekta ya Utalii kutoka Taasisi ya Chemchem iliyopo wilayani Babati mkoa wa Manyara, ametoa basi lenye thamani ya sh 200 milioni kwa  Kijiji cha Vilima Vitatu  kwa ajili ya kuwasafirisha kila siku wanafunzi wa kijiji hicho kwenda na kurudi katika Shule ya  Sekondari  ya Kata ya NKaiti  ili kupambana na tatizo na Utoro.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa  gari  hilo  kwa viongozi wa kijiji hicho  kilichopo ndani ya jumuiya ya uhifadhi wanyamapori ya Burunge mkuu  wa wilaya ya Babati Lazaro Twange alimshukuru Mwekezaji huyo kwa kujitolea kusaidia kijiji huku akiwataka wananchi na wanafunzi watakaotumia gari hilo kulitunza ili liweze kudumu.

Mkurugenzi mkuu wa Chemchem Nicolas Francois  alimkabidhi funguo za gari hilo Mkuu wa Babati ,Lazaro Twange  katika hafla iliyofanyika kijijini hapo Oktoba Mosi mwaka huu.

Francois alisema lengo la msaada huo ni kuboresha elimu katika kijiji hicho kilichopo kata ya Nkaiti  kwa kuwapunguzia adha wanafunzi kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 10  kwenda shule na kurudi.

Akizungumzia msaada huo, Mkurugenzi wa Chemchem Nicolas Francois alisema wametoa msaada huo ili kusaidia kukuza elimu  katika kijiji hicho hasa kutokana na kuwa na mchango mzuri wa kukuza sekta ya Utalii.

“Msaada huu,kutokana na mapato ya watalii wanaokuja hapa hivyo kama mkiendelea kutunza mazingira,kupambana na ujangili, tutaendelea kupokea watalii na kupata fedha za kuchangia maendeleo” alisema Francois

Francois  alisema gari hilo ambalo limenunuliwa nchini Japan hadi kufika katika kijiji hicho na kufanyiwa taratibu zote limegharimu kiasi cha shilingi Milioni  200 na ni gari la pili kutolewa baada ya gari walilolitoa  mwaka 2016  kuharibika  na kurejeshwa kwao.

Afisa elimu sekondari wilaya ya Babati, Paulina Mpare alisema umbali mrefu ni chanzo cha wanafunzi wengi kukatisha ndoto zao kwa kurubuniwa na wenye vyombo vya moto hususani boda boda.

“Kama Msimamizi wa idara ya Elimu nimekutana na tatizo kubwa la utoro kwa wanafunzi , walikuwa hawafiki shuleni kwa wakati  na mara nyingi  wakifika wanakuwa wamechoka , hata suala la ufunishaji luilikuwa ni tatizio” alisema Mpare

Alisema kutolewa basi hilo kutasaidia  kupunguza  vikwazo vilivyokuwa vikiwakuta wanafunzi hao, kuondoa utoro na mimba za Utotoni kwani sasa watasafiri kwa wakati kwenda shule na kurejea majumbani.

Afisa maendeleo wa taasisi ya Chemchem Walter Pallangyo alisema licha ya kutoa gari, Taasisi ya Chem chem itakuwa ikilifanyia matengenezo pamoja na  kumlipa mshahara dereva huku  kijiji kikichangia mafuta pekee.

Mwenyekiti wa kijiji cha vilima vitatu Abubakary Msuya alipongeza msaada huo na kuahidi  kusimamia gari hilo na kuhimiza  wananchi kulitunza basi hilo na kuchangia mafuta.

 

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *