Siasa za Kenya: Fukuto ndani ya chama cha Jubilee, nani anayelengwa?

October 5, 2020

  • Prof. Hezron Mogambi
  • Mhadhiri Chuo Kikuu Nairobi

Dakika 8 zilizopita

Uhuru Kenyatta
Maelezo ya picha,

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Huku vuta nikuvute na tofauti zikiendelea kushuhudiwa katika chama cha Jubilee kinachotawala nchini Kenya, siasa za Kenya zinaonekana kuchukua mkondo mwingine kila wakati.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema hatua hiyo ya chama cha Jubilee inaonyesha wazi kwamba Rais Kenyatta anamlenga naibu wake William Ruto ambaye mara kwa mara amelaumiwa na baadhi ya wanachama wa Jubilee kutomheshimu kiongozi wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Kuna hatua za Rais Kenyatta ambazo zinaelekea kuonesha jambo hili.

Itakumbukwa kwamba tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017 nchini Kenya, rais Kenyatta amekuwa akilenga katika kufikia malengo yake ya maendeleo(ajenda zake tano) na kuonya kuhusu kampeni za mapema.

Hata hivyo, naibu wake William Ruto amekuwa akioneokana akizuru maeneo mbalimbali ya nchi kujipigia debe.

Ni hivi maajuzi tu baada ya mlipuko wa Covid-19 ndipo ziara zake zilipokwamishwa na sheria zinazolenga kuudhibiti ugonjwa huu.

Hatua ya kwanza ni ile ya hivi karibuni ya Rais Kenyatta ya kuitisha mkutano wa maseneta wa chama cha Jubilee katika ikulu ya Nairobi ambapo uongozi wa chama chake cha Jubilee katika bunge la seneti ulibadilishwa.

Kikao hicho kilihudhuriwa na maseneta 20 wa vyama vya Jubilee na KANU huku maseneta 19 wanaogemea upande wa makamu wa rais wakikosa kuhudhuria.

Katika mabadiliko yaliyofanyika katika mkutano huo, wanasiasa wanaonekana kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto akiwemo aliyekuwa kiongozi wa wengi Kipchumba Murkomen na mnadhimu Susan Kihika wamevuliwa nyadhifa zao.

Samuel Poghisio (Pokot Magharibi) ndiye kiongozi mpya wa wengi katika bunge la seneti huku Seneta Irungu Kang’ata(Murang’a) akichukua nafasi kama mnadhimu wa walio wengi katika bunge la Seneti la Kenya na kuchukua nafasi ya seneta Susan Kihika(Nakuru) ambaye anaaminika kuwa karibu na naibu rais William Ruto.

Kufuatia tukio hili, mnadhimu wa seneti Irungu Kangata amewataka maseneta ambao wanamuunga mkono naibu Rais William Ruto na ambao hawakuhudhuria mkutano ulioitishwa na kiongozi wa chama, Rais Uhuru Kenyatta kueleza sababu za kutochuliwa hatua za nidhamu.

Kinachosibiriwa sasa ni kuona hata ambazo chama cha Rais Kenyatta kitawachukulia masenta hao wanaomuunga Bw. Ruto huku duru nyingine zikieleza kuwa huenda wakapoteza nyadhifa zao kama maseneta maana wameteuliwa kwenye bunge la seneti na chama cha Jubilee.

William Ruto
Maelezo ya picha,

Naibu Rais wa Kenya ,William Ruto

Mkutano huu ulifanyika muda mrefu baada ya wabunge wanaoegemea upande wa naibu wa rais William Ruto kumtaka rais kuandaa mkutano wa viongozi wote wa chama hicho ili kuzungumzia masuala muhimu ya kitaifa.

Chama cha Jubilee hakijafanya mkutano rasmi tangu mwaka 2017 baada tu ya uchaguzi mkuu nchini Kenya

Wabunge wanaolengwa kulingana na duru za kuaminika ni wabunge wanaotoka katika eneo la Mlima Kenya (na ambao wanamuunga mkono naibu Rais William Ruto), shehemu ambayo Rais Kenyatta alipata kura nyingi na ambayo ndiyo ngome yake kisiasa.

Duru nyingine zinaeleza kuwa kuna mazungumzo yanayoendelea kati ya chama cha Jubilee na vyama vya upizani kuunda muungano

Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema kuwa mipango na mazungumzo yanaendelea yenye nia ya kuungana na chama cha Jubilee kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao huku kukiwa na tetesi kwamba kiongozi wa chama cha upinzani Raila Odinga na chama chake cha ODM huenda pia akashiriki muungano kama huo.

Mazungumzo ya Jubilee na Upinzani

Tangu walipoingia hatamu ya pili katika uongozi wa Kenya, kumekuwepo na tofauti kati ya viongozi hawa wawili kuhusiana na siasa na maendeleo nchini Kenya.

Huku Naibu Rais William Ruto akionekana kulenga sana siasa za mwaka wa 2022 nchini Kenya na kuanza kampeini zake mapema ili kurithi kiti hicho kutoka kwa Rais Kenyatta, Rais Kenyatta amekuwa akimsuta na wanasiasa wanamuunga mkono kuhusiana na hali hii “ya kulenga siasa tu kila mara badala ya kufanya kazi na maendeleao kwa Wakenya.”

Tofauti kati ya Rais Kenyatta na naibu wake zilianza kuchipuka baada ya uchunguzi mkuu wa mwaka wa 2017 ambao uliokuwa mchuano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Baadaye, Rais Uhuru alipoapishwa na kuingia ofisini, waliamua kuzika tofauti zao na kukutana mnamo Machi 9, 2018 na kuorodhesha ajenda tisa ambazo walisema ndizo zilizowafanya kuanza kufanya kazi pamoja kwa minajili ya kuboresha Kenya na siasa zake.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Naibu Rais , William Rutto
Maelezo ya picha,

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Naibu Rais , William Rutto

Hali hii ya suhirikiano baina ya serikali ya Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga imepelekea baadhi ya watu kueleza kuwa upinzani umelemazwa nchini Kenya jambo ambalo hata naibu Rais William Ruto amekuwa akilitaja.

Aidha, ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ilianza kuleta mtafaruku katika uhusiano kati ya Rais Kenyatta na naibu wake, William Ruto. Wanasiasa wanaomuunga mkono bwana Ruto walianza kuonekana kupinga utaratibu mzima wa jopo la maridhiano (BBI) pamoja na jinsi ya kutekeleza mapendekezo yake.

Hili limebainika wazi kwani Naibu Rais hakuhudhuria mikutano iliyofanyika kuhusu mchakato wa BBI ahata ingawa akisema kuwa alikuwa anaunga mkono mchakato huo. Mnamo October 17, 2019, akiongea katika hafla ya kuzindua barabara muhimu jijini Nairobi Rais Uhuru Kenyatta alizungumzia suala hili na kuwasuta wanaomuunga mkono naibu wake, William Ruto.

“Wanasema ati BBI ni ya kutafutia Uhuru kazi. Mimi sitaki kazi, nimechoka. Eeeh, BBI ni ya kuhakikisha ya kwamba hakuna Mkenya hatamwaga damu tena katika nchi yetu kwa sababu ya siasa. Tuko pamoja?”

Hatua za sasa na zile zitakazofuata kutoka kwa Rais Kenyatta zenye nia ya kuimarisha usimamizi wake katika chama cha Jubilee zinaonyesha ari yake ya kurejesha uthabiti katika uongozi wake na ajenda zake za kimaendeleo.

Hata hivyo, joto la kisiasa linavyoendelea kupanda na siasa za uchaguzi wa mwaka wa 2022 kuchacha, Virusi vya Corona vinaendelea kusambaa nchini, hali ya kuichumi inaendelea kudorora, ukosefu wa chakula unazidi kuwa mbaya, mafuriko yanaendelea kuwaua watu na uvamizi wa viwavi unalemaza uwezo wa Wakenya kujitegemea.

Source link

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *