Rais Ndayishimiye wa Burundi atuwa Tanzania

September 19, 2020

Serikali ya Burundi imeihakikishia Jumuiya ya Afrika mashariki kuwa nchi yao iko salama na inawakaribisha wawekezaji katika sekta mbalimbali kwenda kufanya biashara na nchi hiyo ambayo imekuwa katika machafuko ya kisiasa na kikabila kwa Zaidi ya muongo mmoja.

Hayo yamebainishwa na Rais wa Burundi Everist Ndayishimiye ambaye yuko nchini Tanzania kwa ziara ya siku moja ambapo anakutana na Rais Dr. John Magufuli katika mji wa Kigoma magharibi mwa Tanzania.

Rais Ndayishimiye amebainisha kuwa baada ya kumalizika uchaguzi uliofanyika kidemokrasia, serikali yake ilikaa na pande zote za kisiasa na kukubaliana kuhakikisha nchi haiendelezi migogoro, sambamba na kufuta dhana za makabila ya watusi na wahutu na kukubaliana kuwa Burundi ina kabila moja tu ambalo ni warundi.

Sisi ni warundi, tunazungumza lugha moja, hakuna sababu ya kuendelea kutambua makundi ya wahutu na watutsi kama makabila, kabila yetu ni warundi na lugha yetu ni Kirundi, Wazungu walitumia ukabila kutugawanya ili kututawala, sasa tunajitambua kama taifa huru” amesema Rais Ndayishimiye

Aidha Burundi kupitia kwa Rais wake imeishukuru Tanzania kwa kuendelea kuwahifadhi wakimbizi wa Burundi sambamba na kuwapatia Uraia wale waliopenda kubaki Tanzania baada ya kuishi kwa miaka 40 ambapo Tanzania ilitoa vyeti vya uraia kwa wakimbizi wapatao laki moja na sitini elfu waliokuwa katika kambi na makazi ya Mishambo, Katumba na Ulyankuru katika mikoa ya Katavi na Tabora.

Amepongeza pia kuwepo kwa mkakati wa kuunganisha Burundi na mfumo wa usafiri wa Anga, majini na nchi kavu kwa njia ya reli inayotarajiwa kujengwa kutoka Uvinza Tanzania hadi makao makuu ya nchi ya Burundi -Gitega.

Präsident John Magufuli aus Tansania (Getty Images/AFP/M. Spatari)

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli

Akihutubia wananchi wa mji wa Kigoma Rais Ndayishimiye amesema kuwa Tanzania ni Mzazi wa Burundi na kwamba undugu uliopo ni wa kihistoria na inatakiwa uanze kutumika katika ukuzaji wa uchumi na usalama kwa pande zote mbili, huku akisisitiza watanzania kuwaamini warundi.

Mahusiano ya Tanzania na Burundi

Kwa upande Rais John Magufuli amebainisha kuwa, mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania yamekuwa zaidi huku akitaja kuwa thamani ya biashara kati ya Tanzania na Burundi yameongezeka kutoka bilioni 115.15 mwaka 2016 hadi kufikia bilioni 201 mwaka 2020.

Ameongeza kuwa kituo cha uwekezaji cha taifa kimesajiri miradi 16 kutoka Burundi yenye thamani ya shilingi Bilioni 29 na kwamba makampuni makubwa 10 kutoka Tanzania yamefungua matawi nchini Burundi.

Kutokana na Burundi kutokuunganishwa na bahari, Tanzania imekuwa kitovu cha kiuchumi kwa nchi za maziwa makuu ambapo Burundi pekee hupitisha zaidi ya tani 481,000 kutoka bandari ya Dar es salaam kwenda nchini humo.

Miradi

Rais Magufuli amebainisha kuwa, Tanzania imekubaliana na Burundi kujenga mtambo wa kisasa wa kuchenjua madini pamoja na Burundi kuuza madini yake katika soko la madini la mkoani Kigoma.

Tanzania imetaja pia kuanzishwa kwa miradi ya kimkakati kujenga Reli ya kisasa kutoka Uvinza hadi Gitega-Burundi, kuboresha usafiri katika ziwa Tanganyika kwa kununua Meli mpya mbili na kukarabati Meli kongwe ya MV Liemba yenye umri wa zaidi ya miaka 100.

Hii ni ziara ya kwanza kwa Rais Ndayishimiye kusafiri nje ya nchi tangu alipoapishwa kuwa Rais wa jamhuri ya Burundi mwezi July mwaka huu

Mwandishi: Prosper Kwigize

Mhariri:Yusuf Saumu

 

Source link

,Serikali ya Burundi imeihakikishia Jumuiya ya Afrika mashariki kuwa nchi yao iko salama na inawakaribisha wawekezaji katika sekta mbalimbali kwenda…

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *