Putin kuipa Belarus mkopo wa dola bilioni 1.5

September 14, 2020

Rais wa wa Urusi, Vladmir Putin amesema Urusi imekubali kutoa mkopo wa dola bilioni 1.5 kwa Belarus, lakini watu wa Belarus wana jukumu la kuutatua mzozo wao wenyewe bila ya kuingiliwa na mataifa ya kigeni, huku akibainisha kuwa nchi hizo mbili zitaendelea kushirikiana katika masuala ya ulinzi.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akizungumza na Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko ambaye yuko ziarani kwenye mji wa Sochi, kujaribu kutafuta msaada wa Putin ili kuyamaliza maandamano makubwa yaliyodumu kwa wiki kadhaa nchini humo kumshinikiza ajiuzulu, ikiwa ni siku moja baada ya zaidi ya watu 100,000 kuandamana kwenye mitaa ya mji wa Minsk.

Ushirikiano wa ulinzi

”Tumekubaliana kwamba katika wakati huu mgumu Urusi itaipatia Belarus mkopo wa dola bilioni 1.5. Na tutalitimiza hili. Kama tunavyojua kwa sasa, mawaziri wetu wa fedha wanalifanyia kazi suala hili kitaalamu. Tutaendelea kushirikiana katika nyanja ya ulinzi pia. Hapa ushirikiano wetu ni mkubwa na umejikita katika maeneo nyeti,” alifafanua Putin.

Mbali na kutangaza msaada huo wa fedha ambao Putin amesema Waziri Mkuu wa Urusi, Mikhail Mishustin alikubaliana na Belarus katika ziara yake ya hivi karibuni kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, kiongozi huyo wa Urusi ameashiria kumuunga mkono Lukashenko katika njia nyingine, akisema ushirikiano wa ulinzi utaendelea kati ya nchi hizo mbili. Mashirika ya habari ya Urusi yameripoti kuwa Urusi leo imepeleka kikosi maalum kinachotumia parachuti kwa ajili ya mazoezi ya pamoja. Putin amesisitiza kuwa kikosi hicho ambacho tayari kimewasili Belarus kitaondoka nchini humo baada ya mazoezi kumalizika.

Belarus Minsk | Proteste & Verhaftungen (picture-alliance/AP Photo)

Wananchi wa Belarus wakiandamana

Putin pia amesema ana uhakika Lukashenko atautatua mzozo wa kisiasa wa Belarus na analiunga mkono pendekezo la Lukashenko la kufanya mageuzi ya katiba akisema ni lenye busara na limetolewa kwa muda muafaka. Hata hivyo, pendekezo hilo la Lukashenko limetupiliwa mbali na upinzani ambao wamedai ni njama yake ya kuendelea kubakia madarakani baada ya uchaguzi ambao wanadai uligubikwa na udanganyifu.

Mwanzoni mwa mazungumzo yao, Putin amempongeza Lukashenko kwa kuchaguliwa tena na ameahidi kuwapeleka polisi wa Urusi nchini Belarus, iwapo maadanamano ya umma yatageuka na kuwa ya ghasia, huku akisisitiza hakuna haya ya kufanya hivyo kwa sasa. Amesema Belarus ni mshirika wao wa karibu na bila shaka watatimiza majukumu yao.

Lukashenko amesema maandamano hayo yanachochewa na mataifa ya Magharibi na ameiweka hatma yake mikononi mwa Urusi akiomba msaada wa kiuchumi na kijeshi. Polisi wamesema watu 774 walikamatwa wakati wa maandamano ya jana. Upinzani una hofu kwamba Lukashenko anaweza kujaribu kuuza uhuru wa Belarus kwa msaada wa Putin.

Tangu uchaguzi wa Agosti 9, takriban viongozi wote wakuu wa upinzani nchini Belarus wamefungwa gerezani, wamefukuzwa au wamelazimishwa kukimbilia uhamishoni. Sviatlana Tsikhanouskaya, mgombea wa upinzani katika uchaguzi huo, ambaye wafuasi wake wanasema ndiye mshindi halali wa uchaguzi huo, amesema hakuna makubaliano yaliyofikiwa kati ya Lukashenko na Putin yatakuwa halali. Sviatlana amesema chochote watakachokubaliana katika kikao cha Sochi hakitakuwa na uzito wowote kisheria na kitarekebishwa na uongozi mpya.

(AFP, AP, Reuters)

 

Source link

,Rais wa wa Urusi, Vladmir Putin amesema Urusi imekubali kutoa mkopo wa dola bilioni 1.5 kwa Belarus, lakini watu wa…

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *