New Zealand: Jacinda Ardern ashinda kwa kishindo,

October 17, 2020

Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika leo Jumamosi. Ushindi huo unakipa chama chake cha Labour nafasi ya kuunda serikali bila ya kuvishirikisha vyama vingine.

Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern ameshinda kwa kishindo uchaguzi mkuu uliofanyika leo na kupata wingi wa viti bungeni utakaomwezesha kutekeleza mpango wake wa mageuzi.

Baada ya kuhesabiwa theluthi mbili ya kura zote, chama cha Waziri Mkuu Adern cha Labour kimepata asilimia 49.2 ya kura zote, huku kikitarajiwa kupata viti 64 katika bunge la New Zealand lenye viti 120.  

Hakuna kiongozi mwingine aliyeweza kupata ushindi mkubwa kiasi hicho tangu New Zealand ilipoidhinisha mfumo wa uchaguzi unaozingatia uwiano wa uwakilishi wa kivyama mwaka 1996. Kukosa ushindi wa moja kwa moja kumevilazimisha vyama vilivyoongoza katika kura tangu wakati huo, kuunda serikali zinazovishirikisha vyama kadhaa vingine.

Upinzani wanyoosha mikono

Hata kabla ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu kura, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Judith Collins amekwishampigia simu Waziri Mkuu Ardern, akikubali kushindwa.

Chama cha kihafidhina cha National Party cha Judith Collins kinatazamiwa kuambulia viti 35 bungeni, hayo yakiwa matokeo mabaya zaidi kwa chama hicho kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita.

”Hongera kwa ushindi wako, kwa sababu naamini ni ushindi mkubwa kwa chama cha Labour. Imekuwa kampeni ngumu sana,” amesema Bi Collins mbele ya umati mjini Auckland.

Ushindi huu wa Bi Jacinda Ardern ni mkubwa kuliko ilivyokuwa imetabiriwa katika uchunguzi wa maoni ya wapigakura, na wa juu zaidi kwa chama cha Labour tangu mwaka 1946.

Rais wa chama cha Labour Claire Szabo amesifu kampeni iliyofanywa na Ardern, mwanasiasa mchangamfu ambaye amesababisha wimbi la ushabiki kwa chama hicho alipochukua uongozi wake mwaka 2017, wakati huo chama hicho kikiwa kinaburura mkia katika chunguzi za maoni.

Szabo amesema ”bila shaka yoyote uongozi mahiri wa Jacinda Ardern umetoa mchango mkubwa katika maendeleo mazuri chamani.”

Ushindi uliotokana na kuyakabili majaribu

Jacinda Ardern alikuwa ameupachika uchaguzi huu jina la ”Uchaguzi wa Covid” na juhudi zake zilikuwa kunadi mafanikio ya serikali yake katika kusimamisha maambukizi ya ugonjwa huo. New Zealand yenye wakazi milioni tano, imekwisharekodi vifo 25 tu kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *