Ndugai, Ditopile watinga Kata ya Hogoro kuomba kura za Magufuli, ‘ CCM pekee ndio italeta maendeleo’,

October 7, 2020

SPIKA wa Bunge na Mbunge mteule wa Jimbo la Kongwa, Dodoma, Job Ndugai akiwa na Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile wameshiriki kampeni za kusaka kura za Mgombea Urais wa chama hicho, Dk John Magufuli katika kijiji cha Chamae kata ya Hogoro wilayani Kongwa.

Viongozi hao wamesema licha ya Spika Ndugai kupita bila kupingwa kwenye Jimbo lake na madiwani 17 kati ya 22 wa kata zake kupita bila kupingwa bado wana wajibu wa kuzunguka kumuombea kura Dk Magufuli ili aweze kuibuka na ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano huo na wananchi wa Chamae, Spika Ndugai amesema Dk Magufuli ni kiongozi mwenye maono aliyeletwa na Mungu ili kuja kuwatumikia watanzania na kuwaletea maendeleo.

Amesema ndani ya miaka mitano ya Dk Magufuli Wilaya ya Kongwa imenufaika na ujenzi wa vituo vinne vya afya, maboresho ya Hospitali ya Wilaya ambayo sasa inaenda kuondoa changamoto ya wananchi kusafiri kwenda Dodoma Mjini jambo ambalo limekua nafuu kwa wananchi kwenye sekta hiyo ya afya.

Amesema ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Chamae unaendelea vizuri lakini pia awamu inayofuata ya uongozi wake watajenga tanki kubwa la kisasa litakaloenda kumaliza changamoto ya maji kwa wakazi wa eneo hilo.

” Siyo afya na maji tu tayari kwenye ilani yetu ya CCM upo mpango wa kujenga barabara ya lami ambayo itatoka pale Kongwa Mnadani itapita hapa kuelekea Wilaya ya Kiteto, wote tunajua barabara hii ikiwa ya lami itachangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa kijiji hiki na kata yetu kwa ujumla.

Sasa kuyatimiza hayo yote ni vema tukampigia kura za kishindo Dk Magufuli ili arudi kuwa Rais wetu, wapinzani wanapiga kelele lakini hata wao wenyewe wanajua kazi kubwa iliyofanywa na Dk Magufuli, mwaka 2015 walisema watafufua shirika la ndege, leo Magufuli kanunua Ndege 11 kwa fedha zetu wenyewe wanaponda wanasema hayo ni maendeleo ya vitu siyo watu, tuwapuuze hawa watu wanatapatapa.

Vijana msivutike na maneno ya wapinzani wanasema wataleta Uhuru, Uhuru upi huo wakati Nyerere alishatuletea? Kazi yao ni kuhamasisha vurugu na matusi, tuachane nao sisi tumpe kura za kishindo Rais wetu Magufuli, ” Amesema Ndugai.

Kwa upande wake Ditopile amesema Spika Ndugai na Rais Magufuli wamefanya mambo makubwa katika Wilaya ya Kongwa kwani wamefanikiwa kusambaza umeme Wilaya nzima na kuifanya Kongwa kuwa Wilaya pekee nchini ambayo kila Kijiji kina umeme.

” Mna Mbunge mwenye kuwapenda na kuwatumikia, kwa kuwa mmempitisha bila kupingwa basi mpeni kura za kishindo Rais Magufuli ili Ndugai akienda kuomba maendeleo Rais Magufuli aseme kweli watu wa Chamae na Kongwa walinipigia kura za kishindo ngoja niwakamilishia kwa haraka awamu ya tatu ya REA ili sasa kila kitongoji kikawe na umeme, niwasihi Oktoba 28 mjitokeze kwa wingi tukampe heshima Rais wetu,” Amesema Ditopile.

 

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *