Mradi wa bomba la mafuta wa Uganda, Tanzania unaiathiri vipi Kenya?

September 17, 2020

Dakika 2 zilizopita

Nchi zote mbili na kampuni husika wametoa dola bilioni kumi na sita, kwa ujenzi na kuboresha miundo msingi

Mradi wa Ujenzi wa bomba la mafuta la Uganda kupitia Kenya umepata pigo kubwa baada ya Uganda kutia saini mkataba wa kiserikali na nchi jirani ya Tanzania, kuidhinisha ujenzi wa bomba kama hilo ambalo litaiwezesha Uganda kusafirisha mafuta ghafi kutoka maeno ya machimbo ya mafuta ufuoni mwa ziwa la Albert hadi bandari ya Tanga katika ufuo wa bahari hindi.

Kwa mujibu wa wadadisi wa masuala ya kibiashara na kiuchumi, tukio hili mbali na kukatiza ujenzi wa bomba nchini Kenya, litaisababisha nchi hiyo kujizatiti kwa kiasi kikubwa kuwavutia washirika jirani katika nchi za Sudani Kusini na uhabeshi katika ujenzi huo.

Patricia Rodriguez kutoka kampuni ya Control Risks, ni mdadisi wa masuala ya kiusalama na kiuchumi katika maeneo ya upeo na Mashariki mwa bara Afrika. Anadokeza kuwa kuwa mkataba baina ya Uganda na Tanzania haumaanishi kuwa nchi hizi mbili na Kenya ni maadui, huku akisistiza kuwa bidhaa nyingi zinazotoka ng’ambo na kuelekea katika nchi ya Uganda bado zitapitia nchini Kenya.

‘ Miundo mbinu ya Kenya kama vile bandari, reli na barabara ndio zitakazosalia kuwa nguzo kubwa ya usafiri wa bidhaa za Uganda, na hata kukiwa mizozo ya kisiasa au kibiashara, bado uhusiano mwema upo.’ Patricia alidokeza.

Lakini huku nchi za Uganda na Tanzania zote zikitazamia kufanya uchaguzi mkuu hivi karibuni, inakisiwa kuwa wawekezaji watapata hali ngumu kuendeleza shughuli zao huku viongozi wa kisiasa wakijishughulisha pakubwa na chaguzi.

Hata hivyo, kufuatia kutiwa saini mkataba wa kiserikali na Rais Museveni wa Uganda na John Magufuli wa Tanzania, ujenzi wa bomba lenyewe unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu, huku dola bilioni 3.5 za Marekani zikitazamiwa kutumiwa kujenga kilomita 1,445 la bomba hilo.

Ramani ya maeneo utakapopita mradi

Kwa upande wake Tanzania inatazamia kupata faida zaidi. Inakadiriwa kuwa nchi ya Uganda itailipa Tanzania dola 12 na senti 20 kwa kila pipa la mafuta linalosafirishwa, hii ikiwa ni pato la dola milioni 2 nukta 6 kila siku kwa nchi hiyo kwa miaka 25. Isitoshe wawekezaji wameahidi kutoa ajira 18,000 kwa vijana kupitia mradi huu.

Wadadisi wengi waliokataa kuongea hadharani walitaja kuwa nchi hizi mbili zimejizatiti pakubwa kuwezesha uwekezaji katika mradi huu, hii ikiwa ni kinyume na mwelekeo wa awali ambao ulikuwa unashinikiza malipo ya malimbikizi ya ushuru kabla ya mradi kuendelea.

Kwa mujibu wa Rais Yoweri Museveni, aliyeongea katika uwanja wa ndege wa Geita, katika wilaya ya Chato alipotia saini mkataba, nchi ya Uganda imefutilia mbali agizo kuwa wawekezaji walipe takribani dola millioni 800 zilizodaiwa kama ushuru.

Badala yake, Museveni alidokeza kuwa nchi zote mbili na kampuni husika wametoa dola bilioni kumi na sita, kwa ujenzi na kuboresha miundo msingi, fedha zinazoangaziwa kama uwekezaji katika kipindi cha miaka ishirini na mitano inayokisiwa kuwa awamu ya kwanza ya kusafirisha mafuta ghafi katika eneo hilo.

Rais Museveni wa Uganda na Rais Magufuli walisaini mkataba wakuanza mradi wa bomba la mafuta ghafi mwezi Mei 2017

Kwa upande wake Rais Magufuli alieleza kuwa ushirikiano huo unaonyesha kuwa nchi hizo mbili zitaendelea kuboresha uhusiano wa kibiashara.

Mbali na hayo, Tanzania inaonekana kuwa na uzoefu na ueledi wa kumudu mabomba ya mali ghafi huku tayari ikiwa ina mabomba yake ya gesi yanayotumika kuwasilisha gesi kutoka machimbo hadi bandarini. Kwa mujibu wa shirika lisilo la kiserikali la kuboresha biashara katika maeneo ya Afrika mashariki almaarufu TradeMark East Africa, Tanzania imeshirikiana na nchi jirani ya Zambia tangu mwaka wa 1968 kusafirisha mafuta ghafi kutoka Bandari ya Dar Es salaam hadi mji wa Ndola, nchini Zambia kupitia bomba la ‘Tazama’ ambapo mafuta hayo husafishwa. Trademark pia inataja mabomba ya Gesi ya Songo Songo hadi Dar es Salaam na lile lingine la Mnazi Bay hadi Dar es Salaam kama kielelezo cha umaahiri wa Tanzania katika shughuli hiyo.

Masuala pia ya usalama yanakisiwa kuchangia pakubwa kutoa msukumo kwa ujenzi kufanyika nchini Tanzania. Hivi karibuni magaidi wa Ashabaab wameonekana kuzidisha makali ya mashambulizi yao katika maeneo ya Lamu nchini Kenya ambapo bomba lilitarajiwa kupitia, na hivyo kuhofisha wawekezaji.

Kwa upande mwingine, huku matarajio sasa yakiwa ni kuanza kwa ujenzi wa bomba hili kupitia Tanzania, mashirika kadha yasiyo ya kiserikali yameeleza kuwa yanashuku kuwa kumekuwa na ukiukaji wa haki za kibinadamu na ulaghai katika shughuli ya kutwaa ardhi ya ujenzi wa bomba na miundo mbinu nyingine husika katika nchi zote mbili.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Oxfam, mradi huu tayari umeathiri jamii za kiasilia huku ardhi, mapato, na mazingira yakizorota pakubwa kwa jamii husika.

Rashid Bunya ni Afisa wa utafiti katika kampuni isiyo ya kiserikali nchi Tanzania ijulikanayo kama ‘Northern Coalition on Extractives and Environment au NCEE. Anadokeza shauku zake kwa manufaa ya mradi huu kwa jamii za asilia.

‘utafiti wetu unadokeza kuwa hasara kwa jamii hizi inatarajiwa kuwa kubwa sana katika siku za usoni’, anasema, ‘huku ikizingatiwa kuwa wengi wao wanaishi katika mazingira yasiyowezesha kujumuishwa kwao katika ratiba ya mipangilio wa kuendeleza mradi huu’.

Ujenzi wa bomba la mafuta

Shirika lingine la uanaharakati, International Federation for Human Rights Aalamaarufu ‘FIDH’ limezindua ripoti yake inayodokeza kuwa shughuli za mafuta zinaathiri pakubwa jamii, haswa wanawake zinapotwaa ardhi kwa shughuli za mafuta, bila kuhusisha jamii yeneywe, bila idhini, na bila kutoa fidia kwa uhakiki.

Maria-Isabel Cubides ni mtafiti katika shirika hili. Anatilia mkazo mtazamo huu.

‘ Jamii na watu ambao mali yao imetwaliwa kwa nguvu wanataka habari itakayowawezesha kufanya uamuzi kwa ujuzi na pia fidia ya kuridhisha kwa mali yao. Miradi ya mafuta inavunja jamii na kuharibu kabisa asili ya kitamaduni ya maeneo hayo.’

Kwa upande wake Kampuni ya mafuta ya Total, ambayo ndio mhusika mkuu wa kibinafsi katika mradi huu imekosoa vikali madai haya ikesema kuwa madai yaliyowasilishwa na mashirika haya ni ya kupotosha, na ya zamani. Inadai kuwa yalitendeka kabla mradi huu kuanza vikamilifu ukijumisha wahusika wa sasa.

Katika taarifa iliyoshapishwa mnamo tarehe 10 mwezi September mwaka huu, Total pia ilikanusha madai kuwa imekiuka maadili ya utendakazi au kukiuka haki za kibinadamu katika maeno ambayo inaendeleza shughuli zake.

Source link

,Dakika 2 zilizopita Chanzo cha picha, HABARI MAELEZO Mradi wa Ujenzi wa bomba la mafuta la Uganda kupitia Kenya umepata…

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *