Mkuu wa Wilaya ya Newala ataka mikatati ya kuimarisha na kuendeleza ushirika,

October 2, 2020

 

Mkuu wa Wilaya ya Newala Mkoani Mtwara Mhe. Aziza Mangosongo ametoa wito kwa Viongozi na Watendaji wa Ushirika kushirikiana katika kuhakikisha kuwa Mkulima anapata huduma yenye kuzingatia haki na usahihi wa upimaji wa uzito wa mazao hususani wanapofikisha mazao yao kwenye AMCOS zao na hatimaye katika Maghala Makuu.

Wito huo umetolewa wakati Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw. Charles Malunde alipokuwa katika ziara ya Kikazi Mkoani Mtwara kwa malengo ya kutathmini na kupanga mikakati mbalimbali ya Kiushirika na Maafisa Ushirika pamoja na Viongozi wa Vyama vya Ushirika kwaajili ya maandalizi ya msimu wa Korosho 2020/21. 

Mhe. Mangosongo ameshauri Maafisa Ushirika kuhakikisha maandalizi ya msimu yanakamilika vizuri ikiwa ni pamoja na kuangalia Mizani za kupimia mazao ya Wakulima zimepimwa na Wataalamu wa Wakala wa Vipimo ili kujiridhisha kuwa shughuli za msimu zitaendelea vizuri na kuondosha uwezekano wa kujitokeza kwa malalamiko. DC huyo aliongeza kuwa Maafisa Ushirika, Viongozi pamoja na Watendaji wa Vyama watoe taarifa pale dosari zozote zinapojitokeza.

“Niwaombe Maafisa Ushirika na Viongozi wa Ushirika msisite kutoa taarifa pale ambapo kunaweza kukajitokeza jambo lolote litakalo kuwa ni changamoto kwa Wakulima wetu,” alisema DC

Aidha, Naibu Mrajis Malunde akiwa katika Kikao na Maafisa Ushirika pamoja na Viongozi wa Chama Kikuu  cha Ushirika cha Tandahimba Newala (TANECU) Wilayani Newala amewataka Maafisa Ushirika pamoja na Viongozi wa Vyama kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Ushirika na kuzingatia utendaji wenye uadilifu ili kuepusha Changamoto mbalimbali na kutoa huduma bora kwa Wakulima.

Kwa upande wake Mhasibu wa Chama hicho Bw. Rajab Mussa akisoma taarifa ya maandalizi ya Msimu wa Korosho 2020/21 ya Chama hicho ameeleza kuwa Chama hicho kimefanya maandalizi kuhakikisha kuwa kila Chama cha Ushirika cha msingi cha Tandahimba na Newala kinapata mahitaji muhimu na vitendea kazi vinavyohitajika kwa msimu mpya. Mahitaji hayo akitaja ni pamoja na gunia za kuhifadhia Korosho, Kampuni za Usafirishaji wa Korosho, Vitabu vya kumbukumbu, Maghala ya kuhifadhia Korosho.

   

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *