Migodi Ya Tril 4.6/- Kuajiri Watu 2,000,

August 2, 2021

 

SERIKALI imetoa leseni mbili kubwa za uchimbaji wa madini ya dhahabu na madini adimu zenye thamani ya uwekezaji wa dola za Marekani milioni 200 ambazo ni sawa na Sh trilioni 4.6 za Tanzania.

Msemaji Mkuu wa Serikali, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Gerson Msigwa alisema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa serikali katika kipindi cha robo ya mwisho wa mwaka wa fedha 2020/2021.

Alisema Juni, mwaka huu serikali ilitoa leseni mbili kubwa za uchimbaji madini ikiwamo ya uchimbaji dhahabu katika mgodi wa Nyanzaga, Segerema mkoani Mwanza.

Alisema mgodi huo ni uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani milioni 100 sawa na Sh trilioni 2.3 za Tanzania.

“Uwekezaji katika mgodi wa Nyanzaga ni mkubwa na niseme tu huu ndio mgodi mkubwa kuliko yote nchini wa dhahabu na hata katika ukanda wetu, unakwenda pia kufungua fursa za ajira zaidi ya 1,000 za moja kwa moja na zile za mikataba,” alisema Msigwa.

Alisema leseni ya pili iliyotolewa ni ya uchimbaji wa madini adimu mkoani Songwe na uwekezaji huo ni wa zaidi ya dola za Marekani milioni 100 ambazo ni sawa na Sh trilioni 2.3.

Msigwa alisema mgodi huo utatoa fursa za ajira na pia utakuwa na mahitaji makubwa ya tindikali kwa ajili ya kusafisha madini hayo hivyo ni fursa nzuri ya wazalishaji wa tindikali nchini kujipanga kuangalia jinsi ya kuongea malighafi hiyo.

Alisema katika hatua nyingine, kiwanda cha kusafisha madini hayo adimu kitajengwa nchini mara baada ya madini hayo yatakapoanza kuchimbwa ili yasafishiwe hapa nchini kuyaongezea thamani.

Msigwa alisema hayo yote ni faida za maboresho kwenye sekta ya madini nchini kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita na mapato yameongeka kutoka Sh bilioni 191 hadi Sh bilioni 583 kwa sasa.

Kuhusu mradi wa Nickel wa Kabanga, alisema maandalizi ya uchimbaji yanaanza na utakuwa na mafanikio kwa serikali kwani tayari sheria ya madini ipo na inanufaisha nchi.

Kuhusu mradi wa Mchuchuma, Msigwa alisema mwekezaji ameshapatikana ila hajaanza kuchimba na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kuwa hoja za mwekezaji ziangaliwe na kama ana uwezo wa kuchimba achimbe kama hawezi atafutwe mwekezaji mwingine.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *