Mfumo wa ufugaji wa kisasa waweza kuchagia baa kama COVID-19

September 18, 2020

Hii ni kwa sababu ya matumizi ya dawa za kuua bakteria ambazo hutumika kwa wingi kwa wanyama wanaofugwa kwa sababu ya mayai, maziwa na nyama. Kulingana na ripoti ya shirika hilo la ulinzi wa wanyama, matumizi ya muda mrefu ya dawa za kuuwa wadudu huenda yakazifanya kuwa sugu, kwa sababu ya utegemezi mkubwa wa dawa hizo katika ufugaji wa wanyama.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2020 imebaini kuwa

mbinu za kisasa za kilimo na ufugaji zinazofanana na mifumo ya viwandani, zina mchango mkubwa kwenye kusambaza magonjwa ya kuambukiza kati ya wanyama na binadamu kama vile homa ya nguruwe, homa ya mafua ya ndege na virusi vya Nipah.

Dokta Victor Yamo, meneja wa kampeni za kilimo katika shirika la World Animal Protection linalolinda maslahi ya wanyama anasema kwa mantiki hii ipo haja ya kutathmini upya mifumo ya kisasa ya kilimo na ufugaji wa wanyama. Utafiti wa mifumo ya kilimo na kufuga wanyama wa chakula umebaini kuwa vijidudu na bakteria vinaendelea kuwa sugu na dawa zinashindwa kuviua.

Hayo yamekuwa dhahiri Brazil, Uhispania, Thailand, Marekani na barani Afrika. Vijidudu hivyo ambavyo havisikii dawa vinawatatiza matabibu wanapowahudumia wagonjwa wanaohitaji dawa za kuua bakteria. Hilo linaweza kuchangia na kusababisha janga la kiafya kote ulimwenguni. Utafiti uliofanyika Wuhan umebaini kuwa kilichochangia kutokea kwa karibu nusu ya vifo vyote vilivyotokana na COVID-19 ni maambukizi ya pili ya bakteria na wagonjwa walipewa dawa kuziua.

Dr. Jan Schmidt-Borbach - Tierarzt (World Animal Protection)

Dokta Jan Schmidt-Borbach wa shirika la World Animal Protection

Kwa upande wake Shirika la Afya Uliwenguni, WHO linatahadharisha kuwa huenda ikafikia wakati baadhi ya vijidudu vikawa sugu kwa dawa zote kwa sababu ya matumizi ya kupindukia. Hivyo itakuwa vigumu kwa magonjwa ya kawaida kutibiwa.

Profesa Sam Kariuki ni mkurugenzi wa kitengo cha Utafiti na Maendeleo kwenye taasisi ya utafiti wa tiba Kenya, KEMRI ambaye amehusika na utafiti wa bakteria kwa muda mrefu anasema wakulima na wafugaji wa wanyama wa chakula wanakutana na changamoto nyingi kutokana na hilo.

Hata hivyo, suluhu ipo kwenye kupunguza msongamano kwenye mabanda ya wanyama na mashubaka ya samaki ili wawe kwenye mazingira yanayofanana na yale ya kaiwaida maishani. Hilo litaipunguza haja ya kutumia dawa za kuua bakteria na vijidudu kwani kinga yao itaimarika, kama ambavyo alifanya Joy Mdivo ni mkaazi hapa jijini Nairobi na mfugaji wa samaki aina ya kambare.

Utafiti mwengine uliofadhiliwa na WHO umeonyesha kuwa mbinu za kupunguza msongamano wa wanyama wa chakula wanaofugwa na kuimarisha kinga zao zinaupunguza kwa 24% uwezekano wa vijidudu visivyosikia dawa kuwafikia binadamu kupitia chakula.

 

Source link

,Hii ni kwa sababu ya matumizi ya dawa za kuua bakteria ambazo hutumika kwa wingi kwa wanyama wanaofugwa kwa sababu…

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *