Majaribio ya chanjo ya COVID-19 yaidhinishwa Kenya

September 10, 2020

Majaribio hayo yataongozwa na taasisi ya utafiti wa tiba KEMRI na kuwashirikishwa watalaam na wahudumu 400 wa afya walioko kwenye kaunti za Mombasa na Kilifi. Maeneo ya pwani ndiyo yaliyokuwa ya mwanzo kuripoti maambukizi ya COVID-19 nchini Kenya. Bodi ya dawa na sumu ya Kenya ilichapisha kwenye mtandao wake mwanzoni mwa wiki hii kuwa serikali imeitoa ridhaa kwa chanjo hiyo kufanyiwa majaribio. Kwenye taarifa yake, Katibu mwandamizi katika wizara ya afya, Rashid Aman alithibitisha taarifa hizo. Soma zaidi: Kagwe: Hakuna fedha ya COVID-19 iliyotafunwa Kenya

Hatua itakayofuatia ni ya tume ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi, NACOSTI kuitoa ridhaa yake ijapokuwa uamuzi wa serikali kuu ndio wa mwisho. Ifahamike kuwa Kenya ni nchi ya pili baada ya Afrika Kusini kwenye eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara kufanya majaribio ya chanjo ya COVID-19. Afrika Kusini ilianza mwezi Juni majaribio ya chanjo hiyo hiyo iliyotengezwa na chuo kikuu cha Oxford cha Uingereza. Kwa upande mwengine, kampuni ya madawa ya AstraZeneca iliyoshirikiana na chuo kikuu cha Oxford kuiandaa chanjo hiyo ilibainisha kuwa majaribio yalisitishwa kwa muda ili kuipa kamati maalum muda wa kutathmini usalama wake.

Kenia Corona-Pandemie (picture-alliance/AP Photo/B. Inganga)

Matayarisho hayo yatawashirikisha wahudumu na wataalam wa afya

Hii ni baada ya mtu mmoja wa Uingereza aliyejitolea kufanyiwa majaribio kuanza kuonesha dalili za ugonjwa ambao haufahamiki na kupata madhara ambayo hayakutarajiwa.

Kwa hapa Kenya, azma ya majaribio hayo ni kutathmini usalama wa chanjo yenyewe, uwezo wa kumlinda mhusika na utendaji wake haswa kwa watu wazima walioambukizwa na virusi vya COVID 19. Washiriki watapewa dozi moja ya chanjo na kufuatiliwa kwa muda wa miezi 12. Kenya inasisitiza kuwa majaribio hayo ni muhimu ukizingatia kuwa maambukizi ya virusi vya corona yamechukua mkondo tofauti barani Afrika ikilinganishwa na kwengine.

Soma zaidi: Madaktari wa Nairobi waanza mgomo

Yote hayo yakiendelea, utafiti wa matumizi ya dawa ya chloroquine/hydroxychloroquine kwa watu wazima kupambana na COVID-19 umepata ridhaa. Utafiti huo ujulikanao kama COPCOV utaongozwa na taasisi ya utafiti wa utabibu KEMRI kwenye vituo vyake vya Kilifi, Mombasa, Nairobi na Kisumu na utwashirikisha wahudumu 1,600 wa afya. Kwengineko ulimwenguni washiriki waliolengwa ni alfu 40.

Hata hivyo, baadhi ya wataalam wanashikilia kuwa dawa ya chloroquine/hydroxychloroquin haina uwezo wa kupambana na COVID 19. Hospitali ya rufaa na mafunzo ya Chuo Kikuu cha Kenyatta inasubiria ridhaa ya kutumia majimaji ya damu kufanyia utafiti wa kupambana na COVID-19.

Hata hivyo, masharti ya kawaida ya kuchangia damu lazima yafuatwe. Itakumbukwa kuwa bodi ya dawa na sumu ya Kenya imeshaidhinisha majaribio ya pili ya dawa ya yabisi kavu yanayofadhiliwa na Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO kwa wagonjwa walioambuziwa virusi vya corona

Thelma Mwadzaya, DW Nairobi

Source link

,Majaribio hayo yataongozwa na taasisi ya utafiti wa tiba KEMRI na kuwashirikishwa watalaam na wahudumu 400 wa afya walioko kwenye…

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *