Maandamano Ufaransa kuonyesha umoja kushtumu kisa cha mwalimu aliyechinjwa,

October 18, 2020

 

Maandamano yanatarajiwa kufanyika katika miji kadhaa nchini Ufaransa leo, kuonyesha mshikamano dhidi ya kisa cha kuchinjwa kwa mwalimu aliyewaonyesha wanafunzi vibonzo vya Mtume Mohammed. 

Kisa cha mwalimu huyo wa historia Samuel Paty kukatwa kichwa nje ya shule viungani mwa mji wa Paris Ijumaa iliyopita, kimeibua ghadhabu nchini Ufaransa na kukumbusha wimbi la machafuko ya Waislamu wenye itikadi kali ya mwaka 2015, ambayo pia yalichochewa na kuchapishwa kwa vibonzo vya Mtume Mohammed kwenye jarida la Charlie Hebdo. 

Akiwataka waandamanaji kujitokeza kwa wingi, waziri wa Elimu wa Ufaransa Jean-Michel Blanquer ameliambia kituo cha televisheni cha France 2 kwamba ni muhimu kuonyesha umoja na mshikamano wa kitaifa dhidi ya kisa hicho. 

Maandamano hayo yanapaswa kufanyika eneo la Place de la Republique mjini Paris, ambako mnamo mwaka 2015, takriban watu milioni 1.5 waliandamana kushtumu shambulizi lililofanywa na Waislamu wenye itikadi kali, waliokuwa na bunduki katika ofisi ya jarida la Charlie Hebdo. 

Maandamano mengine yanatarajiwa kufanyika Lyon, Toulouse, Strasbourg, Nantes, Marseille, Lille na Bordeaux.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *