Lebanon na Israel kujadiliana kuhusu mpaka wa baharini,

October 13, 2020

 

Lebanon na Israel, ambazo kimsingi bado ziko katika hali ya vita kufautia mzozo wa miongo kadhaa, zitafanya mazungumzo kushughulikia mgogoro wa muda mrefu juu ya mpaka wa baharini katika eneo la bahari ya Mediterania.

Eneo hilo linalogombaniwa  lina uwezekano wa kuwa na hifadhi kubwa ya nishati ya gesi. 

Mazungumzo  hayo  ambayo  Marekani  ndio mpatanishi  yanafuatia miaka  mitatu ya  diplomasia ya kina inayofanywa  na  Marekani  na yametangazwa  chini  ya  mwezi mmoja  baada  ya  Marekani kuongeza  shinikizo  dhidi  ya  washirika  wa  kisiasa  wa  kundi  la Lebanon la  Hezbollah  linaloungwa  mkono  na  Iran.

Mazungumzo  hayo  pia  yanakuja  baada  ya  Umoja  wa  Falme za Kiarabu  na  Bahrain  kukubali kurejesha  uhusiano kamili  na  Israel, chini  ya makubaliano  ya  upatanishi  wa  Marekani, ambayo yamewavuta  baadhi  ya  washirika  wa karibu  wa  Marekani  katika mashariki  ya  kati kujiweka kando na  Iran.

Hezbollah , ambayo ilipigana  vita  vya  wiki  tano  na  Israel  mwaka 2006, imesema  mazungumzo  hayo  si ishara ya  kuleta  amani  na adui wake  huyo  wa  muda  mrefu. Waziri  wa  nishati wa Israel pia amesema  matarajio katika  mazungumzo  ya  kesho  Jumatano ni lazima yaangalie hali  halisi.

Majadiliano ya amani 

“Hatuzungumzi juu  ya  majadiliano ya  amani na  kurejesha uhusiano, badala  yake  ni jaribio la  kutatua mzozo  wa  kiufundi na kiuchumi  ambao kwa  miaka  kumi umechelewesha hatua  za maendeleo za  maliasili  ya  baharini,” waziri Yuval Steinitz ameandika  katika  ukurasa  wa  Twitter. Spika wa bunge  la Lebanon Nabih Berri amesema juhudi za Marekani ni muhimu kwa ajili ya mazungumzo hayo.

“Marekani  ina nia  ya kuweka juhudi zake zote na  pande hizo  mbili kusaidia  kujenga  hali bora na yenye uwezo wa  kuleta  mafanikio kati ya  pande hizo mbili  ili  kulinda  mazungumzo  na  kuyafikisha mwisho  kwa mafanikio haraka  iwezekanavyo.”

Hata  hivyo, waziri wa  mambo  ya  kigeni  wa  Marekani Mike Pompeo ameueleza  uamuzi  huo  wa kuendelea  na  mazungumzo hayo  kuwa  ni  wa  kihistoria, na  kusema  Marekani ina  matumaini makubwa  kwa  mazungumzo tofauti baadaye kuhusiana  na kutokubaliana  juu  ya  mpaka  wa ardhini wa  nchi  hizo  mbili.

Mkutano wa  kesho Jumatano utasimamiwa na  ujumbe  wa  kulinda amani  wa  Umoja  wa  Mataifa  UNIFIL, ambao  umekuwa  ukiangalia mzozo huo  wa  mpaka  wa  ardhini  tangu  kuondoka  kwa  jeshi  la Israel  kutoka Lebanon  kusini  mwaka  2000, na  kufikisha  mwisho miaka  22  ya  kulikalia  eneo  hilo.

Chanzo  katika kitengo  cha  usalama  nchini  Lebanon kimesema pande  hizo  mbili zitakutana katika  chumba hicho  hicho  katika kituo  cha  UNIFIL kusini  mwa  Lebanon , lakini watafanya mazungumzo  yao  kupitia mpatanishi.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *