Kyrgyzstan yatangaza hali ya dharura.

October 9, 2020

Hatua hiyo inafuatia siku kadhaa za machafuko kufuatia uchaguzi unaozozaniwa. Huku hayo yakiendelea, rais wa zamani wa taifa hilo Almazbek Atambayev amenusurika kwenye jaribio la kuuawa hii leo.

Mwandishi wa habari wa shirika la habari la Reuters amesema kumesikika milio ya risasi na kushuhudiwa waandamanaji kutoka makundi hayo ya upinzani wakirushiana mawe na chupa pamoja na kutupiana maneno.

Ofisi ya Jeenbekov imetoa tangazo hilo la hali ya dharura ambayo pia imejumuisha amri ya kutotoka nje na vikwazo vikali vya kiusalama ambavyo kwa pamoja vitaanza kutekelezwa kuanzia saa mbili usiku wa leo hadi saa mbili asubuhi hadi ifikapo Oktoba 21.

Agizo hilo la rais hata hivyo halikufafanua ni wanajeshi wangapi watapelekwa lakini ilisema wataelekezwa kutumia magari ya kijeshi, kutengeneza vituo vya ukaguzi na kuzuia mapigano ya watu waliojihami kwa silaha.

Kirgsitan Porteste gegen die Parlamenstwahlen (Elaman Karymshakov/Sputnik/dpa/picture-alliance)

Serikali imeagiza kupelekwa wanajeshi katika mji mkuu wa taifa hilo kupambana na machafuko ya wenye silaha.

Mapema, rais alisema alikuwa tayari kujiuzulu pale baraza jipya la mawaziri litakapokuwa limechaguliwa.

Taifa hilo limeshuhudia mzozo wa kimamlaka, huku makundi ya upinzani yakivutana miongoni mwao tangu yalipodhibiti majengo ya serikali na kulazimisha kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa bunge uliofanyika siku ya Jumapili.

Urusi imeielezea hali hiyo ya Kyrgyzstan inayopakana na China na ambayo pia ina kambi ya wanajeshi wa Urusi kuwa ni ya “vurugu na machafuko matupu”.

Mzozo huo unatoa mtihani kwenye mamlaka ya ikulu ya Kremlin kuelekea kuzitengeneza siasa za eneo hilo lililokuwa na ushawishi kwenye uliokuwa Muungano wa Kisovieti wakati ambapo mapígano yamepozuka kati ya Armenia na Azerbaijan huku Belarus nayo ikiwa imegubikwa na maandamano.

Upinzani umegawanyika kati ya vyama 11 vinavyowakilisha maslahi ya kikabila katika taifa hili ambalo tayari limeshuhudia marais wawili wakiondolewa tangu mwaka 2005.

Maafisa waliojitangaza waachia ngazi.

Wagombea wa upande wa upinzani wanaowania nafasi ya uwaziri mkuu Omurbek babanov na Tilek Toktogaziyev wamekubaliana kuunganisha nguvu hii leo, huku Toktogaziyev akikubali kuwa msaidizi wa Babanov. Walikuwa wanaungwa mkono na vyama vinne, hii ikiwa ni kulingana na tovuti ya habari ya 24.kz.

Kirgisistan: Proteste für Sadyr Zhaparov in Bishek
(Nezir Aliyev/AA/picture-alliance)

Upinzani uliogawanyika umeendelea kuandamana mitaani katika mji mkuu Bishkek nchini humo.

Hata hivyo baadhi ya vyama vya siasa bado havijaonyesha msimamo wao.

Washirika wa Jeenekov walishinda ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa bunge siku ya Jumapili baada ya matokeo rasmi ya uchaguzi ambayo tayari yamefutwa. Washirika hao wamekuwa hawajitokezi sana wakati vyama vya upinzani vikiingia mitaani kuandamana. waangalizi wa magharibi wamesema uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa kura. 

Hadi sasa, maafisa wa zamani waliounga mkono uasi huo wamekuwa wakividhibiti vikosi vya usalama. Hii leo, viongozi wa mpito waliojiteua kwenye wizara ya mambo ya ndani na usalama wa taifa waliondoka kwenye majengo na kukabidhi uongozi kwa wasaidizi wao. Idara hizo mbili za serikali zimesema hatua hiyo ilikuwa inalenga kuhakikisha kwamba vikosi vya usalama havifungamani kisiasa.

Huku hayo yakiendelea, rais wa zamani wa taifa hilo Almazbek Atambayev amenusurika katika jaribio la kuuawa katika mji mkuu Bishkek wakati gari lake liliposhambuliwa kwa risasi, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la Urusi, RIA lililomnukuu msaidizi wake.

Soma Zaidi: Uchaguzi Kyrgystan

Mashirika: RTRE.

 

Source link

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *