Kituo cha Afya cha Bukoli chakabidhiwa ambulance ya Milioni 32,

October 1, 2020

Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Rafiki Surgical Mission kutoka Australia wametoa msaada wa gari la wagonjwa lenye gharama ya Milioni 32 kuhudumia wagonjwa katika kituo cha Afya cha Bukoli na maeneo jirani Wilayani Geita.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya gari hilo katika Kituo cha Bukoli Wilayani Geita, Makamu Rais anayeshughulikia Mahusiano na Maendeleo endelevu, Simon Shayo amesema msaada wa gari hilo umetolewa kwa wakati muafaka na utasaidia kutatua changamoto za usafiri kwa wagonjwa mahututi katika Kata hiyo ya Bukoli na maeneo ya jirani.

“Halmashauri ya Wilaya ya Geita iliomba msaada wa gari la wagonjwa kutoka GGML ili kuwasaidia wagonjwa katika jamii ya watu wa Bukoli ambao waliokuwa na changamoto kubwa kila ilipobidi kusafirisha wagonjwa kwa ajili matibabu makubwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Geita ambayo ipo wastani wa kilomita 35 kutoka kijiji cha Bukoli” Shayo

Kwa karibu miaka 20 sasa, mbali na kutoa msaada wa vifaa tiba, Geita Gold Mining Limited kwa kushirikiana na Rafiki Surgical Mission  wameongeza wigo wa matibabu kwa watoto na watu wazima mkoani Geita  ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya midomo sungura na migongo wazi kwa kuwapatia matibabu ya upasuaji bure.

Shayo amesema GGML imefadhili miradi mbalimbali ya afya Wilayani Geita ikiwemo ukarabati wa Hospitali ya Rufaa mkoani Geita na ujenzi wa vituo vipya vya afya katika Vijiji vya Nyamalembo, Nyakahongola, Kasota na  Kakubiro ambapo miradi yote hiyo kwa pamoja iligharimu Shilingi bilioni moja na milioni mia nane (1.8bn) za Kitanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ali Kidwaka, amesema Serikali inatambua mchango wa GGML katika kutatua changamoto ya huduma za afya katika halmashauri ya wilaya na kwengineko mkoani Geita na kuwaomba washirika wengine waliopo katika Wilaya ya Geita kushirikiana na Serikali kwa lengo hilo hilo.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *