Kenya inaelekea kwa wimbi la pili la virusi vya corona,

October 18, 2020

 

Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe amethibitisha kuwa watu 685 wameambukizwa virusi vya corona ndani ya saa 24 huku idadi jumla ya walioambukizwa kufikia sasa ikiwa 44,881.

Akiwa anatoa taarifa kuhusu ugonjwa wa virusi nchini humo, Waziri Kagwe amesema kuwa maambukizi ya sasa hivi yameongezeka kwa asilimia 12 ikilinganishwa na asilimia 4 wakati Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alipotangaza kulegezwa kwa masharti kidogo na kufunguliwa kwa uchumi.

Watu 635 ni raia wa Kenya huku 50 wakiwa raia wa kigeni.

“Kati ya walioambukizwa, 456 ni wanaume huku 229 wakiwa wanawake mdogo kabisa akiwa na umri wa mwaka mmoja na wa umri wa juu akiwa na miaka 99,” Kagwe amesema.

Kagwe pia amesema kuna wasiwasi kuhusiana na idadi ya wanaopelekwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi ambayo sasa hivi imefikiwa wagonjwa 28.

“Kwa muelekeo huu, bila shaka Kenya inaelekea kwa wimbi la pili la virusi vya corona”, Waziri Kagwe amesema.

Bwana Kagwe ameweka wazi kwamba ikiwa wananchi watashindwa kufuatilia kanuni zilizowekwa kukabiliana na virusi vya corona hali huenda ikawa mbaya zaidi.

Idadi ya leo ni ya juu tangu kuanza kuonekana kana kwamba maambukizi ya virusi hivyo yameanza kushuka nchini Kenya.

Aidha, watu zaidi 7 wamethibitishwa kufariki duniani na kuongeza kwamba vifo vingi vimetokea kwa watu wenye umri zaidi ya 58 ingawa walio na umri wa miaka ya 20 na 30 pia wamefariki dunia.

Hadi kufikia sasa, idadi ya waliofariki dunia imefikia 832.

Kulingana na waziri, wagonjwa 105 wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kupona.

Bwana Mutahi Kagwe amesisitiza kuwa huenda Kenya ikajikuta kwenye janga iwapo wananchi hawatachukua tahadhari.

Aidha, amewasihi viongozi ikiwemo wanasiasa kuonesha ushirikiano katika kukabiliana na ugonjwa wa corona na kuwakosoa kwa mikutano ya kisiasi inayoendeshwa bila kuhakikisha hatua zilizowekwa na wizara ya afya zinatekezwa.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *