Kansela Merkel kukutana na kiongozi wa upinzani wa Belarus

October 6, 2020

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anakutana hivi leo na kiongozi wa upinzani wa Belarus, Svetlana Tikhanovskaya kwa mazungumzo binafsi mjini Berlin. 

Akizungumza na gazeti la Der Spiegel kabla ya mkutano huo, kiongozi huyo wa upinzani aliashiria kwamba majadiliano yao yatajumuisha uwezekano wa Kansela Merkel kuwa mpatanishi wa mzozo unaorindima nchini Belarus. 

Kiongozi wa muda mrefu wa Belarus, Alexander Lukashenko, ameendelea kusalia madarakani, licha ya uchaguzi wake wa mwezi Agosti kutokutambuliwa na upinzani na jumuiya ya kimataifa, ikiwemo Ujerumani. 

Svetlana Tikhanovskaya alishika nafasi ya pili kwenye uchaguzi huo, lakini kwa mujibu wa wafuasi wake ni yeye ndiye mshindi halali. 

Msemaji wa Kansela Merkel, Steffen Seibert, amesema kansela huyo ana furaha kukutana na mwanasiasa huyo wa Belarus, huku akirejelea msimamo wa Ujerumani wa kuunga mkono maandamano ya amani dhidi ya serikali nchini Belarus.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *