Kampuni 21 za nunua korosho RUNALI, bosi wa CBT na DC watema cheche,

October 12, 2020

Na Ahmad Mmow, Lindi. 

 Kampuni 21 zimenunua kilo 2,854,008 za korosho katika chama kikuu cha ushirika cha RUNALI, kupitia mnada wa kwanza kwa msimu wa 2020/2021 uliofanyika kwenye viwanja vya ofisi kuu ya chama cha RUNALI iliyopo mjini Nachingwea. 

Katika mnada huo ambao ulikuwa tofauti na minada ya misimu iliyopita kwa korosho kununuliwa kwa mifumo miwili tofauti ( mtandao kupitia soko la bidhaa,TMX na barua za kawaida ndani ya boksi la zabuni) ilishuhudiwa bei 82 tofauti zilizoombewa na kampuni hizo kununua zao hilo.

 Ambapo kampuni zilizofanikiwa zimenunua kwa bei ya juu ya shilingi 2,555 na bei ya chini shilingi 2,422 kwa kila kilo moja. 

 Korosho zilizonunuliwa zipo katika maghala  yaliyopo katika wilaya za  Nachingwea na Ruangwa. Ambapo katika  ghala la Lipande, wilayani Ruangwa ambalo korosho zake zilinunuliwa kwa bei ya shilingi 2,395 hadi 2,345 lina kilo 580363. 

 Katika ghala Lindi farmes lililopo wilayani Nachingwea ambalo korosho zake zilinunuliwa kwa bei ya shilingi 2,451 hadi shilingi 2,430 lina kilo 779,843.

Wakati katika ghala la Pachani lililopo katika wilaya hiyo ya Nachingwea lina kilo 1,213,102 ambazo zimenunuliwa kwa bei ya shilingi 2,555 hadi 2,422 kwa kila kilo moja. 

 Akizungumza baada ya wakulima kukubali kuuza kwa bei hizo, kaimu mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania ( CBT), Fransis Alfred alisema kumekuwa na upotoshaji wa makusudi unaofanywa na baadhi ya watu kwamba katika msimu huu wa 2020/2021  wakulima wamebebeshwa tozo nyingi na kulipishwa madeni yasiyowahusu. 

Kaimu mkurugenzi huyo wa CBT alisema habari hizo hazina ukweli wowote. Kwani hakuna tozo iliyoongezwa wala deni ambalo wakulima wamebambikiwa kama inavyodaiwa na watu hao wenye nia ya kuwachonisha wananchi na serikali yao. 

 Alisema madeni yanayohusu gharama za uendeshaji katika msimu wa 2018/2019, ikiwamo ya wasafirishaji na vifungasshio (magunia) yalishalipwa. 

” Tarehe kumi na tisa, mwezi wa saba, mwaka huu waziri mkuu katika AMCOS ya Matogolo wilaya ya Tandahimba alikwenda na fedha shilingi bilioni ishirini ambazo zilitumika kulipa madeni yote. Kwahiyo hakuna ukweli wowote kama wakulima wamebebeshwa mzigo na kubambikiwa madeni,” Alfred alisisitiza. 

 Bosi huyo wa CBT alisema wasichokijua wapotoshaji hao ni madeni ya siku za nyuma ambayo hicho kiasi cha shilingi 25 ambacho wanasema watakatwa wakulima katika kila kilo moja ya korosho katika msimu huu ni kwamba fedha hizo zinakatwa na kuchukuliwa kutoka CBT shilingi10 kutoka kwenye shilingi 25 za ushuru wake , Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Kilimo- Naliendele(TARI-Naliendele) shilingi 10 kutoka kwenye ushuru wake wa shilingi 25 na wasafirishaji shilingi 5 kutoka kwenye shilingi 50 ambazo wanalipwa kwa usafirishaji. 

Huku akiweka wazi kwamb punguzo hilo  litatumika kulipia deni la magunia ambayo wapotoshaji wanasema wamebambikiwa wakulima. 

 Alfred alibainisha  kwamba hakuna tozo iliyoongezeka msimu huu. Bali jumla yatozo zote ni shilingi 226.52 ambayo ni jumla ya tozo za msimu uliopita. 

 Alfred alitoa wito kwa wakulima kwakuwaambia kwamba yeyote atayetozwa zaidi ya shilingi 226.52 awasiliane na bodi ya korosho. 

Kwaupande wake mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Hashim Komba alisema korosho ni maisha na uchumi kwa wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara. Kwahiyo zisitumike kwa maslahi ya kisiasa kwa kuwatia hofu, kuwapotosha na kuwajengea chuki baina yao na serikali. 

 Alisema wapo baadhi ya watu wanaotumia korosho kwa maslahi ya kisiasa kwa kuwapandikiza chuki kwamba wanakandamizwa na kulipishwa madeni yasio wahusu. 

Aidha Komba aliwatoa hofu wakulima nakutaka wapuuze uzushi unaosema watakatwa fedha zao kwa ajili ya kuchangia timu ya mpira wa miguu ya Namungo iliyopo wilayani Ruangwa, mkoa wa Lindi.

 Ambayo inashiriki ligi kuu na ikikabilwa na kibarua kigumu cha mashindano ya kimataifa katika ligi ya shirikisho. 

 Alisema hakuna maagizo wala kikao kilichopitisha azimio la kutaka wakulima wa korosho wakatwe ili kuichangia timu hiyo.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *