Jinsi ya kuepuka kupotezewa muda kwenye mapenzi,

October 12, 2020

 

Raha  ya uhusiano wa mapenzi ni kumpata mwenza sahihi na kwa wakati muafaka. Unapopishana na muda, unachelewesha maendeleo yako maana mapenzi ni chachu ya maendeleo. Ili uingie kwenye familia, inakupasa uingie katika muda sahihi na mtu sahihi. Kinyume chake utaishia kuchezewa, ukija kushtuka umri unakuwa si rafiki.

Utaingia kwenye uhusiano na mtu ili mradi tu na wewe uwe na mtu. Kwa sababu tu unataka na wewe uwe na familia. Lakini kama ungeingia mapema, pengine ungekuwa mbali katika mipango yako. Wengi sana wanajuta kupoteza muda. Wanalia kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye si sahihi. Ukitaka kufanikiwa kwenye uhusiano, hakikisha unampata mtu sahihi na katika muda muafaka.

Ukisikiliza simulizi za wanaume wengi kwa sasa, watakuambia wamechoka kuishi maisha ya ubachela. Wanataka kuwa na wenza wao ili kwa namna moja au nyingine, washirikiane katika kutengeneza maisha na wapate maendeleo kabla uzee haujawanyemelea.

Wanakiri kwamba kwa kuishia maisha ya ubachela, wanajikuta wakiwa kwenye matumizi makubwa ya fedha yasiyokuwa ya lazima. Wanalazimika kutumia fedha nyingi kwa kununua vyakula hotelini, kuwapeleka wanawake baa, gesti au hoteli pamoja na mambo mengine mengi ya starehe.

Kifupi inafika wakati wanayachoka hayo maisha. Wanayaona hayana tija katika suala zima la maendeleo. Hapo ndipo wanawasaka wenzi wa maisha kwa udi na uvumba. Bahati mbaya sana, wakati wakiwa wanawasaka wenzi, wanakutana na changamoto ya kupata watu sahihi.

Mwanaume anakuwa yuko tayari kuingia kwenye uhusiano lakini mwanamke anakuwa bado. Anataka kuula ujana na yupo katika kile kiwango cha ‘kunguru hafugiki’. Mwanaume hata afanye nini, yeye si wa kutulizwa akatulia.

Si wanaume pekee, hata wanawake nao wanakutana na matatizo kama hayo. Unakuta mwanamke yupo tayari kwa lolote, amechoshwa na maisha ya kuhangaika na dunia, anataka kuingia kwenye uhusiano wenye tija lakini wapi. Anaambulia patupu maana kila anayekutana naye, hana huo mpango.

Huu ndio ulimwengu ulivyo. Mwanaume aliye tayari, anahaha kumpata mwanamke aliye tayari bila mafanikio Vivyo hivyo mwanamke aliye tayari, naye anahangaika kila uchwao kumsaka mtu ambaye atakuwa baba wa watoto wake lakini naye anapishana naye.

Usikurupuke
Linapokuja suala la kumsaka mwenzi wa maisha, hupaswi kukurupuka. Unapaswa kufanya tathimini ya kina ili uweze kumpata yule ambaye ni sahihi. Usiendeshwe na tamaa ya mwili. Kwamba huyu mrefu, huyu mfupi huyu ana hiki, tazama mahitaji sahihi ya mtu unayemtaka.

Unayetaka kuingia naye kwenye uhusiano, ana tabia njema? Ana hofu ya Mungu? Hofu ya Mungu, ni chachu ya mafanikio yoyote duniani. Mwenye hofu ya Mungu ana tabia njema. Mwenye hofu ya Mungu ni mvumilivu. Ana hekima, ana busara na anaweza kusamehe pale inapobidi.

Mwenye hofu ya Mungu si mtu wa visasi. Si mtu wa kukaa na chuki au kuwa na kinyongo. Anapoombwa msamaha wa jambo alilokosewa, akasema amesamehe basi ujue limeisha. Hutalisikia tena!

Muda ni kitu cha thamani
Tunashauriwa tusipoteze muda. Pale unapoona upo na mtu sahihi, mwenye malengo sahihi tunapaswa kupashikilia. Muda haumsubiri mtu. Usiseme eti utaingia kwenye ndoa baadaye, safari ya ndoa inaanza na uchumba. Hakikisha unaujenga kwa muda muafaka na uweze kuingia na mtu sahihi.

Kuchelewa kuingia, wakati mwingine ni kujikuta unaingia na mtu ambaye si sahihi. Utajikuta umeingia kwa sababu tu unaona umri unakutupa mkono. Yeyote atakaye-jitokeza ni halali yako. Tengeneza njia sahihi katika muda sahihi.,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *