Jeshi la Tanzania lakana madai kuwa linahusika na mzozo Msumbiji

September 7, 2020

Dakika 2 zilizopita

kundi la Islamic State lilidai kwamba lilitibua shambulio kutoka kwa wanajeshi wa Msumbiji wakishirikiana na wenzao wa Tanzania

Jeshi la Tanzania limekana madai kwamba limekuwa likihusika katika mzozo wa kivita unaoendelea nchini Msumbiji.

Akizungumza na BBC kwa njia ya simu msemaji wa jeshi hilo Luteni kanali Juma Sipe amesema kwamba habari hizo ni uvumi uliozagaa katika vyombo vya habari na kwamba hazina ukweli wowote.

Matamshi yake yanajiri kufuatia madai ya kundi la Islamic State kwamba liliwauwa wanajeshi 20 wa Tanzania wakati lilipokuwa likijaribu kufanya mashambulizi kaskazini mwa Msumbiji.

Katika taarifa yake ya tarehe 5 mwezi Septemba kundi hilo la Islamic State lilidai kwamba lilitibua shambulio kutoka kwa wanajeshi wa Msumbiji wakishirikiana na wenzao wa Tanzania karibu na eneo la Mocimboa da Pria katika mkoa wa Cabo Delgado.

Katika ripoti hiyo wapiganaji hao wa Islamic State wanadai kwamba wapiganaji wao waliwajeruhi wanajeshi wa Tanzania wakati wa makabiliano hayo katika eneo hilo, na kuongezea kwamba walifanikiwa kukamata silaha kadhaa mbali na magari manne ya kivita.

Lakini akijibu taarifa hizo msemaji wa Jeshi la Tanzania Luteni Kanli Juma Sipe amesema kwamba hadi kufikia sasa wanajeshi wa Tanzania hawajawahi kuvuka mpaka na kuingia Msumbiji.

”Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania limesikitishwa mno na taarifa hizo na kwa ujumla ni kwamba hatukutarajia kabisa kwamba jambo hilo lingeweza kuzungumziwa kwasbabu Tanzania haina wanajeshi ambao wamevuka mpaka na kuingia Msumbiji”, alisema bwana Sipe.

”Hadi kufikia sasa tunakalia maeneo yetu ya utendaji ambayo hayahusiani kabisa na operesheni zozote za Msumbiji”, alisema Luteni Sipe.

Aidha afisa huyo wa jeshi ameongezea kwamba wanajeshi wa Tanzania hawana ushirikiano wowote wa kijeshi na Msumbiji na kusisitiza kwamba hakuna mwanajeshi wa taifa hilo aliyevuka na kuingia taifa hilo.

Ramani

Bwana Sipe ametaja madai yanayotolewa na kundi la Islamic State kuwa propaganda zinazolenga kulipatia umaarufu kundi hilo.

”Kwa jumla ni kwamba utendaji wa jeshi la Tanzania upo katika maeneo yake ya kawaida kabisa katika kutekeleza ulinzi wa mipaka yake na operesheni zake hazihusiani kivyovyote vile na harakati zinazoendelea nchini Msumbiji.

Tarehe 12 mwezi Agosti 2020 Msumbiji ilinukuliwa ikisema kwamba vikosi vyake vinapigana kurejesha udhibiti wa bandari muhimu ya Mocimboa da Praia, baada ya taarifa kadhaa kudai kwamba bandari hiyo ilikuwa imetekwa na wanamgambo wa Islamic State .

Mji huo uko karibu na miradi ya gesi asili yenye thamani ya dola bilioni 60.

Je ni nini kinachoendelea Msumbiji?

Jeshi la Msumbiji lilisema kuwa hatua imechukuliwa kukabiliana na kundi hilo ambalo limekuwa likitumia wenyeji kama ngao yao.

Hatua hiyo inafuatia mapigano ya siku kadhaa ya kutaka kuchukua udhibiti wa bandari hiyo iliyo kwenye eneo lililona utajiri mkubwa wa gesi eneo la kaskazini.

Mwandishi wa BBC Africa Andrew Harding alisema kuwa kutekwa kwa bandari hiyo ni pigo kubwa kwa jeshi la Msumbiji, ambalo lina wakati mgumu kudhibiti ukuaji wa makundi ya waasi katika eneo hilo la utajiri wa mafuta la Cabo Delgado.

Bandari ya Mocimboa da Praia inatumiwa kwa uwasilishaji wa mizigo kwa miradi ya eneo la pwani takribani umbali wa kilomita 60 (maili 40), ambayo inaendelezwa na kampuni kubwa za mafuta duniani ikiwemo Total.

Wanamgambo – wenye kuhusishwa na kundi la Islamic State -wamekuwa wakiteka miji kadhaa ya kaskazini katika miezi ya hivi karibuni, na kulazimisha maelfu ya watu kutoroka makazi yao.

Baadhi ya kampuni kubwa duniani za nishati sasa zinataka ulinzi zaidi wakati zinajitayarisha kuanza kuzalisha mafuta katika visima vilivyo pwani ya Msumbiji.

Aidha, serikali imetafuta usaidizi kutoka kwa wanakandarasi wa usalama wa kimataifa. Lakini hadi kufikia sasa Msumbiji inaonekana haiko tayari kugeukia nchi jirani kutafuta usaidizi wa kijeshi.

Source link

,Dakika 2 zilizopita Chanzo cha picha, AFP Jeshi la Tanzania limekana madai kwamba limekuwa likihusika katika mzozo wa kivita unaoendelea…

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *