Je kuna athari gani kwaTundu Lissu kusimamishwa kufanya kampeni

October 5, 2020

Dakika 8 zilizopita

Mgombea wa urais kupitia Chadema Tundu Lissu

Katika uchaguzi ambao hadi sasa ni vigumu kufahamu kwa hakika ni asilimia ngapi ya wapiga kura watampigia mgombea Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, au wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli, ni vigumu kupima athari za kusimamishwa kwa kampeni za mgombea yeyote.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010 na 2015, taasisi za kitafiti kama vile Twaweza na IPSOS zilikuwa zikitoa matokeo ya kura za maoni kuhusu wagombea na vyama vilivyokuwa vikishiriki katika chaguzi hizo. Mara nyingi matokeo yalikuwa yakipokewa kwa hisia tofauti na wafuasi wa vyama husika; kila chama kikitaka chenyewe kionekane ndiyo kinaongoza; lakini ukweli ni kuwa mara nyingi tafiti na matokeo yalikuwa yakikaribiana na ukweli.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, taasisi ya Twaweza ilifanya utafiti uliompa aliyekuwa mgombea Urais wa CCM, Magufuli ushindi wa karibu asilimia 60 ya kura zote na matokeo halisi ya NEC yalipotoka, yalikaribiana kabisa na ukweli huo.

Tafiti zilikuwa na faida mbili; mosi kueleza ni mgombea au chama kipi kinapewa nafasi nzuri zaidi lakini pili ni masuala yapi yanapewa nafasi zaidi na washindani.

Katika kufanya uchambuzi, ingekuwa rahisi kujua nani angeathirika na kwa namna gani kwa kukosekana kwake kwenye kampeni na kama aina ya ujumbe anaosambaza unahitaji mikutano ya hadhara au kampeni za kawaida kufika kwa wapiga kura wake.

Baada ya kutungwa kwa sheria tofauti zinazodhibiti utoaji wa taarifa za kitafiti, taasisi ambazo zingekuwa zinafanya kazi hiyo kwenye uchaguzi huu sasa hazifanyi hivyo tena.

Matokeo yake ni kwamba uchaguzi huu umekosa taarifa na nyenzo muhimu za kufanya utafiti kwenye suala kama hili la kusimamishwa kwa Lissu.

NEC na Chadema

Taarifa ya kusimamishwa kwa kampeni za Lissu kwa muda wa siku saba zilitolewa na NEC kwa madai kwamba mgombea huyo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema, alikiuka taratibu za uchaguzi.

Uamuzi huo unadaiwa kukubaliwa kwenye Kamati ya Maadili ya NEC inayoundwa na vyama vyote 15 vilivyosimamisha wagombea urais katika uchaguzi huu. Kwa mujibu wa NEC, vyama 12 vilikubaliana na adhabu hiyo kwa Lissu na vitatu havikukubali.

Kosa la Lissu, kwa mujibu wa NEC, lilikuwa ni kutoa taarifa zisizo sahihi kwenye mikutano yake ya kampeni kuwa CCM imewaita Dodoma wakurugenzi wote wa halmashauri zilizopo nchini kwa ajili ya kupanga mikakati ya kukipa chama tawala ushindi katika uchaguzi huu.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, wakurugenzi wa halmashauri ndiyo wasimamizi wakuu wa chaguzi zinazofanyika na Lissu alisema alikuwa na taarifa kuwa wasimamizi hao walikuwa wameitwa Dodoma kwa kazi hiyo.

NEC ilisema taarifa hizo hazikuwa za kweli na ndiyo ikawa chanzo cha adhabu hiyo.

Hata hivyo, kupitia mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliielezea adhabu hiyo ya NEC kwa mgombea wao kama mwendelezo tu wa vitendo vya tume hiyo kukipendelea chama tawala cha CCM katka uchaguzi huu.

Mbowe alisema ingawa wamekubaliana na adhabu hiyo kwa mgombea wao, watafanya kila wanaloweza kuhakikisha mgombea huyo anaendelea na shughuli zake nyingine za kijamii ambazo hazina uhusiano na kampeni kwa vile ana majukumu mengi kutokana na nafasi yake kama Makamu Mwenyekiti wa Chadema.

Mtindo wa kampeni wa Lissu

Ingawa uchaguzi huu una wagombea 15 wa nafasi ya urais, ni Lissu na Magufuli pekee ndiyo ambao wameonekana kuchuana kwa kufanya mikutano mingi na katika maeneo mengi hapa nchini.

Tayari Lissu amezunguka katika kanda zote nne za Tanzania; Kusini, Kaskazini, Mashariki, Kati na Magharibi; akizunguka karibu katika maeneo yote yenye wafuasi wa kutosha wa chama hicho – akifanikiwa pia kwenda Zanzibar alikotangaza hadharani uamuzi wa kumuunga mkono mgombea Urais wa visiwa hivyo kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Seif Shariff Hamad.

Kabla hajarejea Tanzania baada ya kumaliza matibabu yake nchini Ubelgiji, yaliyochukua takribani miaka mitatu kutokana na shambulizi dhidi ya maisha yake lililofanywa na watu ambao bado hawajajulikana Septemba mwaka 2017, kulikuwa na wasiwasi kwamba huenda Lissu amepoteza silaha yake kubwa zaidi katka maisha yake ya siasa na uanaharakati; uwezo wa kujieleza.

Katika mwezi wa kwanza wa kampeni, Lissu ameonyesha kwamba hajapoteza hata kidogo uwezo wake wa kujieleza na kupambanua mambo magumu kwa lugha rahisi. Kabla hajarejea, ilikuwa ikisemwa kwamba kurejea kwake ndiyo kungebadili mchezo na kusema kweli upepo wa kisiasa nchini umebadilika tangu kurudi kwake.

Hoja zake zimegawanyika kutokana na aliko. Akienda katika eneo kwenye shida za wakulima, atajikita kwenye kero za wakulima, kwa wavuvi atazungumzia uvuvi na sasa Lissu anajua hata nguo za kuvaa katika siku ambazo wazee wa Pwani na Waislamu huvaa siku za Ijumaa.

Na ingawa watu wengi wanamfahamu kama mtetezi wa masuala ya haki na mjuzi wa masuala ya sheria, L9ssu hajakaa mbali katika masuala ya uchumi na uhusiano wa kimataifa.

Lissu pia amejipambanua kwa kufanya mikutano ya mtandaoni (Webinar) na vituo vya luninga na redio vya nje ya nchi; eneo lingine ambalo limempa utofauti miongoni mwa washindani wake katika uchaguzi wa mwaka huu.

Athari za kusimamishwa kampeni

Kampeni rasmi za uchaguzi zinampa mgombea fursa mbili adhimu; muda wa kukutana na kushawishi wapiga kura na kupata fursa ya kutangazwa na vyombo vya habari. Katka kipindi cha miaka minne iliyopita, kilio kikubwa cha vyama vya sasa vya upinzani Tanzania kilikuwa ni kukosekana kwa fursa hizi mbili.

Hatua ya mgombea kukutana na wapiga kura wake na faida mbili kubwa; kusimika nguvu pale ilipo na kupata fursa ya kutongoza wapiga kura ambao bado hawajaamua wamchague nani katika uchaguz huu.

Kuna tofauti moja kubwa kati ya Lissu na aliyekuwa mgombea Urais wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Edward Lowassa. Lissu ni mgombea ambaye ni rahisi kukubalika kwa wana Chadema lakini watu wengi wanaopenda CCM na vyama vingine wanaweza kuwa na shida naye kwa sababu ya ulimi wake mkali. Kwa hyo kuna kundi kubwa la watu ambao bado hawajaamua kama Lissu atawafaa au bado.

Lowassa alikuwa na bahati ya kukubalika na watu wa CCM, wa Chadema kwa sababu ya kuwa mgombea wake na kwa sababu hakuwa machachari na mwenye ulimi mkali kama wa Lissu, hakupata taabu sana kuwavuta kwake wale waliokuwa hawajafanya uamuzi wa nani watamchagua.

Kwa hiyo, pigo kubwa kwa Lissu katika hatua hii ya NEC liko zaidi katika kukosa kuongeza idadi ya wapiga kura ambao hadi sasa wanasubiri kutongozwa na mmoja wa watu wanaotaka kuwa vongozi wa Tanzana baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Kuna athari pia katika kukosa fursa ya kuandikwa na vyombo vya habari na kuchangamsha washabiki wake. Mazingra aliyopitia Lissu ni ya kipekee sana kiasi kwamba wako watu ambao wanahitaji kumwona au kumshika – kama ilivyokuwa kwa Tomaso wa kwenye Biblia, la kuamini kwamba yu mzima na anaweza kutimza majukumu yake vizuri.

Mgombea Urais wa CCM, Rais Magufuli, alikuwa amepanga kupumzika kufanya kampeni kwa muda wa wiki moja na kama Lissu angekuwa barabarani, ina maana angepata muda mkubwa wa kuwa hewani peke yake kwa takriban wiki moja.

Uamuzi huu wa kusimamshwa kwa kampeni zake utamnyima fursa hiyo ambayo bila shaka angeweza kuitumia vizuri. Hata hivyo, haonekani kwamba Tundu ni aina ya wanasiasa ambao wanaweza kukaa kimya kwa muda wa wiki moja.

Tundu Lissu

Kuna uwezekano chama chake kikaandaa mambo na matukio ambayo si ya kikampeni kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, lakini yatampa fursa ya kusikilizwa, kuona au kutazamwa na wapiga kura.

Lissu anaweza kuhojiwa na vyombo vya habari kuhusu masuala tofauti kama mwanasheria, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, mbunge mstaafu na Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).

Pamoja na kusimamishwa kwa kampeni zake, Lissu bado hakatazwi kuongoza vikao vya chama chake, kukutana na watu katika matukio ya kijamii na mambo mengine mengi ambayo anaweza kuamua kujihusisha nayo.

Jambo moja ambalo liko wazi katika wakati wa kampeni ni kwamba kila jambo linalofanywa na mgombea ni kampeni. Ni vigumu sana kumtofautisha mgombea na kampeni za uchaguzi katika mambo ya kibinafsi anayoweza kuyafanya.

Ndiyo sababu, Mbowe aliwaamba waandishi wa habari kwamba pamoja na kusimamishwa kwa kampeni rasmi za urais, Lissu ana kazi nyingi za kufanya kwa wadhifa wake kama Makamu Mwenyekiti wa Chadema.

Kama ningekuwa mcheza kamari, ningesema tutarajie jambo moja au mawili la kusisimua kutokea, kabla Lissu hajamaliza siku zake za kusimamishwa kupanda majukwaani kufanya siasa.

Yeye, tayari, ameshajua atafanya nini. Kama lilivyo jina lake, atatafuta tundu lilipo katika kibano hiki kwa ajili ya kugeuza kuwa fursa ya kisasa.

Source link

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *