Je itakuwaje ikiwa Trump atakuwa mgonjwa sana,

October 3, 2020

 Ikiwa zimesalia wiki chache tu kabla ya uchaguzi wa urais Marekani, Donald Trump amethibitishwa kuwa na virusi vya corona.

Hilo limezua swali gumu la kipi kitakachotokea ikiwa atashindwa kutekelza majukumu yake.

Je kampeni gani ambayo rais atakosa?

Bwana Trump anahitajika kujitenga kwa siku 10 kuanzia alipopimwa kuthibitisha ikiwa ana ugonjwa wa Covid- 19 yaani Oktoba mosi, kwahiyo bado anaweza kushiriki mdahalo wa pili wa urais uliopangwa kufanyika Oktoba 15.

Mkutano uliopangwa kufanyika Florida Ijumaa ulifutwa.

Bwana Trump ana mikutano mingine iliyopangwa kipindi hiki ambayo sasa hivi itahitajika kuahirishwa au kufutwa.

Je ni kwa hali gani uchaguzi unaweza kucheleweshwa?

Kipindi cha rais Trump kujitenga bila shaka kina athari zake katika kampeni.

Na hivyo basi kuna swali lililoulizwa la ikiwa uchaguzi unaweza kucheleweshwa na je hilo linaweza kutokea vipi?

Uchaguzi wa urais kisheria unafanyika Jumanne baada ya Jumatatu ya kwanza ya Novemba, kila baada ya miaka minne – hivyo basi mwaka huu utafanyika Novemba 3.

Kubadilisha tarehe kutakuwa jukumu la wabunge na wala sio rais.

Pia kutahitaji kuwa na wingi wa kura katika mabunge yote mawili kuuunga mkono kubadilishwa kwa tarehe yoyote ile.

Uwezekano wa hilo ni mdogo, ikizingatiwa kwamba kutahitajika kuungwa mkono na bunge la wawakilishi ambalo linadhibitiwa na chama cha Democratic.

Hata kama utabadilishwa, sheria ya katiba ya Marekani inasema utawala wa rais unakuwa madarakani kwa miaka minne pekee. Hivyo basi, muhula wa rais utafika ukomo wake moja kwa moja Januari 20, 2021.

Na kubadilisha tarehe hii kutahitaji mabadiliko ya katiba. Hilo litahitajika kuidhinishwa na theluthi mbili ya wabunge, kisha robo tatu ya majimbo ya Marekani – hatua ambayo tena ni vigumu kufikiwa.

Je ni kipi kitakachotokea ikiwa rais atakuwa mgonjwa sana?

Ikiwa pengine rais atakuwa mgonjwa sana na kushindwa kutekeleza majukumu yake, katiba ya Marekani inasema hivi:

Marekebisho ya 25 yanaruhusu rais kukabidhi madaraka kwa makamu wake, ambaye kwa sasa ni Mike Pence atakayekuwa ana kaimu.

Ikiwa pengine rais atakuwa mgonjwa sana kiasi cha kushindwa kukabidhi madaraka, baraza la mawaziri na makamu wake wanaweza kumtangaza kwamba ameshindwa kuendelea kutekeleza majukumu na Bwana Pence ataanza kutekeleza majumu hayo.

Ikiwa Bwana Pence pia naye atashindwa kuetekeleza majukumu, chini ya Sheria ya Urithi wa Rais, Nancy Pelosi, spika wa Bunge la Wawakilishi – ambaye ni wa chama cha Democrat – ndiye anayefuata kwa orodha hiyo, ingawa wataalamu wa katiba wanasema uhamishaji wa madaraka wa namna hiyo utasababisha malumbano ya kisheria.

Na ikiwa naye hayuko tayari au hawezi kuendeleza majuku hayo, yatakabidhiwa Seneta mwandamizi wa chama cha Republican, ambaye kwa sasa ni Charles E Grassley, 87. Lakini hatua hiyo vilevile, moja kwa moja itakabiliwa na upinzani wa kisheria.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *