Hali ya afya ya Trump yachunguzwa baada ya wikendi iliojaa hofu

October 5, 2020

Dakika 6 zilizopita

Trump ndani ya gari lake

Rais wa Marekani Donald Trump anaendelea kupewa uangalizi wa karibu akiwa hospitali ambako anapokea matibabu ya Covid-19.

Kuna tashwishi kuhusu uwezekano wa Bw. Trump kutolewa hospitali – kama walivyokuwa wamesema madaktari wake kwamba huenda akatoka Jumatatu huku maswali yakiibuliwa kuhusu hali yake.

Kiwango cha oksijeni yake kilishuka mara mbili na pia anatiliwa tiba ya steroid. Siku ya Jumapili, aliushangaza umma alipoonekana hadharani akiendeshwa kwenye gari kuwasalimu wafuasi wake, hatua ambayo ilikosolewa vikali.

“Zaidi ya Wamarekani 205,000 wamefariki. Tunataka uongozo. Sio picha na video,” aliandika

Kwenye Twitter yake Hakeem Jeffries, mwenyekiti wa Democrats katika bunge la Wawakilishi. Akiwa amevalia barakoa, rais alipunga mkono kutoka ndani ya gari muda mfupi baada ya kuandika ujumbe kwenye mtandao wake wa Twitter akisema kwamba atafanya “ziara ya kushutukiza”.

Bw.Trump, ambaye amekosolewa kwa jinsi alivyoshughulikia janga la corona, pia alisema amejifunza mengi kuhusu virusi hivyo.

Awali, madaktari wake walisema Bw. Trump anaendelea kupata nafuu na kwamba huenda akatolewa hospitali kufikia Jumatatu.

Dk Sean Conley alisema kiwango cha hewa ya oksijeni cha rais kilishuka mara mbili tangu alipogunduliwa kuwa na virusi vya corona, na ameanza kutumia dawa inayofahamika kama dexamethasone.

Rais aliongezewa oksijeni ya ziada mara moja baada kuthibitishwa kuwa na virusi, alisema Dk Conley, ambaye pia alifafanua mkanganyiko uliosababishwa na taarifa tofauti kuhusu hali ya Bw. Trump.

Katika ujumbe wa Twitter, rais – aliyekuwa amevalia suti, koti na shati bila kufunga tai – alisema: “Nimejifunza mengi kuhusiana na Covid” Nimejifunza kwa kwenda shule haswa.

Hii ni shule halisi. Hii sio shule ya njoo tusome vitabu. Sasa naona na nimeelewa. Ni jambo la kuvutia sana, hivi karibuni nitawafahamisha.”

Kuugua kwa rais, kulikotangazwa hadharani na yeye mwenywe kwenye mtandao wa Twitter mapema Ijumaa, kumevuruga ratiba yake ya kampeni.

Bw.Trump atakabiliana na mpinzani wake wa chama cha Democratic Joe Biden katika uchaguzi wa urais wa Novemba tatu.

Madaktari wake walisema nini?

Akizungumza na wanahabari katika kituo cha kitaifa cha matibabu karibu na Washington DC, Dk Conley alisema kiwango cha hewa ya oksijeni ya Trump kilishuka kwa mara ya kwanza akiwa Ikulu ya White House.

Rais alikuwa na homa kali, alisema, na kuongeza kuwa kiwango cha oksijeni cha mtu mzima kinatakiwa kuwa asilimia 95 au zaidi na chake kilikuwa asilimia 94%.

Rais aliongezewa oksijeni ya ziada “kwa karibu saa moja”, alisema daktari kabla ya kukimbizwa Walter Reed nyakati za jioni. Taarifa hizo tayari zilikuwa zimeangaziwa pakubwa katika vyombo vya habari vya Marekani, lakini uthibitisho wa Dkt. Conley ulikuja baada ya yeye kukataa kujibu maswali mara kadhaa kuhusiana na suala hilo siku ya Jumamosi.

Tukio la pili lilifanyika siku ya Jumamosi, wakati kiwango chake cha oksijeni kilishuka chini ya asilimia 93. Alipoulizwa kuhusu hilo, Dkt. Conley hakusema ikiwa rais aliongezewa hewa ya oksijeni lakini akaongeza, ikiwa hilo, lilifanyika, “ilikuwa kwa kiwango kidogo sana”.

Dkt. Conley alisema, tuliamua kumpatia Bw. Trump dawa ya dexamethasone, ambayo utafiti umeonesha inaimarisha hali ya mgonjwa aliyelazwa hospitali akiwa na ugonjwa wa Covid-19.

Hata hivyo, alikubali kuwa siku iliyotangulia alielezea hali Bw. Trump kwa uangalifu: “Sikutaka kutoa taarifa ambayo itazua hali ya taharuki. Na kwa kufanya hivyo inaonekana kana kwamba tulikuwa tunajaribu kuficha kitu fulani, hali ambacho huenda sio kweli.”

Rais mwenye umri wa miaka 74, a anaorodheshwa miongoni mwa watu waliyo na uzani mkubwa kuliko kiasi, yuko kwenye kundi la watu walio kwenye hatari zaidi kuugua maradhi ya Covid-19.

Siku ya Ijumaa alipewa dawa ambayo inafanyiwa majaribio ambayo inajumuisha mchanganyiko wa dawa inayopatiwa mgonjwa kwa njia ya sindano na pia ameanza kutumia dawa ya remdesivir kwa siku tano.

Dkt Brian Garibaldi, ambaye pia ni mmoja wa kundi la madaktari wanaomtibu alisema: “Anaendelea kupata nafuu, amekuwa mchangamfu na mpango wetu wa leo ni kumshawishi ajaribu kula na kunywa, na ajaribu kutoka kitandani na kutembea mara kwa mara.”

Madaktari wamesema rais hajapatikana na homa tangu siku ya Ijumaa na ini na figo zake zinafanya kazi kama kawaida.

Lakini Dkt. Conley amekataa kujibu maswali ikiwa uchunguzi uliofanyiwa umeonesha ikiwa mapafu yake yameathirika au la.

Source link

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *