Fahamu faida za kuchangia damu,

October 1, 2020

Damu ni tiba muhimu kwa afya ya mwanadamu na ni damu ya binadamu pekee ndio inayo tumika. Kumekuwa na ukosefu wa damu katika hospitali zetu. Tatizo hili limechangia vifo vingi ambavyo vimeweza kuzuilika. Hivyo katika kulitatua tatizo la ukosefu wa damu, uchangiaji wa damu wa hiari ndio utakaoweza kuokoa maisha ya mgonjwa.

KWA NINI UJITOLEE KUCHANGIA DAMU?

Hadi sasa hakuna utaalamu wa kuzalisha damu nje ya binadamu. Kwa hiyo, wewe ni miongoni mwa wanaopaswa kujitolea damu. Unapojitolea damu unashiriki kikamilifu kuokoa maisha ya binadamu

Kumbuka: Chupa moja ya damu inaweza kuokoa maisha ya watu watatu

NI MAKUNDI GANI YA WATU WANAOHITAJI KUONGEZEWA DAMU?

Makundi katika jamii yanayohitaji damu mara kwa mara ni:-

Watoto wadogo hasa walio chini ya umri wa miaka mitano.

Majeruhi wa ajali mbalimbali hasa ajali za barabarani.

Wajawazito na wanawake wenye matatizo ya uzazi.

Watu wanaofanyiwa tiba ya upasuaji.

Wale wote wenye magonjwa mbalimbali yanayosababisha upungufu wa damu.

Kumbuka:Inawezekana damu unayochangia ni kwa ajili yako, familia na jamii

SIFA ZA MTU ANAYEWEZA KUCHANGIA DAMU

Mtu yeyote awe mwanamke au mwanamume anaweza kutoa damu kufuatana na sifa zifuatazo:

Asiwe na maradhi kama vile Kisukari, Shinikizo la damu, kifafa, ugonjwa wa ngozi n.k

Asiwe mjamzito au anayenyonyesha.

Asiwe na mwenendo unaoweza kuhatarisha kupata maradhi yanayoambukizwa kwa njia ya damu (kufanya ngono zisizo salama, kutumia dawa za kulevya,ulevi wa kupindukia)

Awe na umri kati ya miaka 18 hadi 65

Uzito wa kilo 50 au zaidi

Asiwe katika tiba yoyote

NI MARA NGAPI MTU ANATAKIWA KUCHANGIA DAMU KWA MWAKA?

Mwanamke anaweza kuchangia kila baada ya miezi minne.

Mwanamume anaweza kuchangia kila baada ya miezi mitatu

Kumbuka: Toa taarifa sahihi unapohojiwa na wataalam wa huduma ya damu Salama.

JE NAWEZA KUAMBUKIZWA VIRUSI VYA UKIMWI WAKATI WA KUCHANGIA DAMU?

Hapana.

Kuchangia damu ni kitendo salama kabisa kwani vifaa vyote vinavyotumikwa ni safi na salama hutumika mara moja kwa mtu mmoja.

JE DAMU YANGU ITAFANYIWA VIPIMO GANI?

Damu itapimwa vipimo vifuatavyo:-

Kiwango cha damu

UKIMWI (VVU)

Kaswende

Homa ya Ini (Hepatitis B na C)

Makundi ya damu.

JE NITAPEWA MAJIBU YA VIPIMO VYA DAMU YANGU?

Ndio

Utapewa majibu yako kupitia mshauri nasaha baada ya kupimwa. Vipimo vyote vya maabara hufanywa kwa usiri wa hali ya juu. Hakuna mtu yeyote atakayeambiwa majibu ya vipimo vyako bila ya idhini yako.

JE NITALIPWA NIKICHANGIA DAMU?

Hapana.

Kuchangia damu ni kitendo cha kibinadamu ambacho hufanywa kwa hiari bila malipo yoyote, kwani damu ina thamani kubwa. Hospitali hazitatoza malipo kwa damu inayotolewa kwa hiari. Wizara ya Ustawi wa Jamii zitagharamia shughuli zote zinazohusu upatikanaji wa damu salama

Kumbuka: Damu ina thamani kubwa. Damu nu UHAI na HAIUZIWI.

JE NAWEZA KUPIMA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI (VVU) KATIKA VITUO VYA MPANGO WA DAMU SALAMA BILA YA KUCHANGIA DAMU?

Mpango wa Taifa wa Damu Salama, sio kituo cha kupima afya za wananchi. Huduma kama hizo zinapatikana katika vituo vya upimaji na ushauri nasaha (VCT) kilicho karibu na wewe, mfano ZANGOC,ANGAZA, Hospitali za Rufaa, Mikoa na Wilaya.

NIFANYE NINI ILI NIWEZE KUWASAIDIA WAGONJWA WANAOHITAJI DAMU HOSPITALINI?

Changia damu leo hujachelewa

Hamasisha ndugu na rafiki zako wachangie damu mara kwa mara.

Wasaidie wafanyakazi wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama kuifikia jamii yako kwa urahisi kwa kuunda na kujiunga kwenye klabu za wanaochangia damu katika eneo lako.

WITO KWA VIONGOZI

Viongozi katika ngazi mbalimbali na watu wote mashuhuri wanatakiwa kutumia Nafasi walizonazo kuhamasisha watu kuchangia damu.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *