Ditopile: Watanzania tumuenzi Mwl Nyerere kwa kumchagua Dk Magufuli Oktoba 28,

October 14, 2020

IKIWA leo ni kumbukumbu ya miaka 21 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwl Julius Nyerere, Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile amemfananisha Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli na Mwl Nyerere kutokana na aina yake ya utendaji kazi katika kuwatumikia watanzania.

Kauli hiyo ameitoa leo mkoani Dodoma katika Kata ya Majereko wilayani Chamwino alipoenda kushiriki kampeni za CCM ambapo amemuombea kura za Urais Dk Magufuli, kura za mgombea  ubunge wa Chamwino, Deo Ndejembi na Diwani wa kata hiyo, Mussa Omary.

Akizungumza na wananchi hao, Ditopile amesema kwa miaka mitano ya uongozi wake, Dk Magufuli ameyaishi mawazo, fikra na ndoto za Mwl Nyerere za kuwaletea maendeleo watanzania hasa Uhuru wa kiuchumi jambo ambalo amelitimiza kwa kiwango kikubwa.

” Wakati Mwl Nyerere na wenzake wakiichukua Nchi hii kutoka kwa wakoloni alisema tuna maadui watatu ambao ni Ujinga, Maradhi na Maskini, leo Magufuli anauondoa ujinga kwa kutupatia elimu bila malipo kuanzia shule za Msingi hadi kidato cha nne, yote hayo ni kutekeleza malengo ya Baba wa Taifa.

Magufuli anapambana na Maradhi kwa kasi kubwa, miaka mitano tumeshuhudia ujenzi wa vituo vya afya 484 nchi nzima, Hospitali za Wilaya 71 hii ni miaka mitano tu, tukimpa miaka mitano mingine ataenda kumaliza Kabisa changamoto zilizopo kwenye sekta ya afya,” Amesema Ditopile.

Amesema katika kukabiliana na umaskini, Dk Magufuli amehamisha ujenzi wa viwanda vingi ili kutoa fursa ya ajira sambamba na kutoa vitambulisho vya wajasiriamali kwa Sh 20,000 mwaka mzima jambo ambalo limefanya ongezeko kubwa la vijana wanaojiajiri huku pia akipiga marufuku wafanyabiashara hao wadogo kusumbuliwa na badala yake wafanye biashara sehemu yoyote ilimradi hawavunji sheria na wana kitambulisho.

Amewaomba wananchi wa kata hiyo kuchagua mafiga matatu yanayotokana na CCM kwa maana ya Rais Magufuli, Mbunge Ndejembi na Diwani Omary ili waweze kushirikiana kuleta maendeleo kwa kasi zaidi.

” Tunaposema Magufuli ameyaishi maono ya Mwl Nyerere tunamaanisha, leo Madini tunafunaika nayo wenyewe, hatuibiwi tena kama zamani, tumeona jana alivyopokea gawio kutoka sekta ya madini Sh Bilioni 100 kutoka kwa kampuni ya Twiga, hii ni kuonesha sasa watanzania wananufaika na rasilimali zao,” Amesema Ditopile.

Amesema kama ilivyokua kwa Baba wa Taifa katika kusimamia uadilifu serikalini, kusimamia nidhamu kwa watumishi wa umma ndivyo ambavyo kwa miaka mitano ya Dk Magufuli ilivyokua jambo ambalo kwa miaka mingi lililkua limepotea.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *