Ditopile amuwashia moto Salum Mwalimu wa Chadema, ‘Magufuli amekuza uchumi wetu’,

October 9, 2020

 

TUMEPIGA hatua! Ndiyo kauli ambayo Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile aliyowaambia wananachi wa kata ya Ngomai wilayani Kongwa alipoenda kuomba kura za Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli.

Akizungumza na wananchi wa kata hiyo, Ditopile amesema miaka mitano ya Dk Magufuli imekua bora na ya kukumbukwa kwa namna alivyofanya mambo makubwa kwa muda mfupi jambo ambalo limewafanya hata raia wa Nchi jirani kutamani wangekua na Rais kama Magufuli.

Amesema miaka ya Dk Magufuli imesaidia kukuza uchumi wa Nchi kwa jinsi alivyoweka mazingira bora ya kibiashara, kusimamia nidhamu ya ukusanyaji wa mapato bila kuweka matabaka jambo ambalo limefanya mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato TRA kufikia Sh Trilioni 1.8 kutoka Bilioni 800 kwa mwezi mwaka 2015.

Amemshangaa Mgombea Mwenza wa Urais wa Chadema, Salum Mwalimu kwa jinsi alivyowahadaa wananchi wa Kariakoo alipofanya mkutano wake akisema biashara zimekufa ilihali watu waliohudhuria mkutano wake wengi ni wafanyabiashara wa Kariakoo.

” Mgombea Mwenza wa Chadema alikua Kariakoo kawakusanya wafanyabiashara anasema Serikali Mbaya Biashara zimekufa wakati hapo yupo na wafanyabiashara mzima kweli huyu? Biashara zilizoanzishwa kipindi cha Magufuli ni zaidi ya 147,818, ukusanyaji wa mapato umepanda kutoka Bilioni 800 kwa mwaka 2015 hadi Trilioni 1.8 mwaka huu, mapato yatapandaje kama biashara ni mbaya? Tuwapuuze.

Hakuna nyakati Soko la Kariakoo limejaa wafanyabiashara kama kipindi hiko cha Magufuli, siyo wa madukani hadi machinga, Rais Magufuli kupitia vitambulisho vile vya wajasiriamali amesaidia vijana wengi kujiajiri na leo ukienda Kariakoo hakuna hata sehemu ya kuweka miguu kwa jinsi vijana wa kitanzania walivyojiajiri, hizi zote ni jitihada za Magufuli kutuinua wanyonge.

Mipango yetu kama Nchi ilikua kufikia uchumi wa kati 2025 lakini Magufuli katufikisha mwaka 2020, miaka mitano kabla, leo hii kila mtanzania analipa kodi anavyostahili tofauti na nyuma wanyonge ndio walikua wanalipa peke yao, chini ya Magufuli hakuna rushwa na kila mmoja analipa kodi na nidhamu ya ukusanyaji wa mapato ndio imetusaidia leo kujenga vituo vya afya, hospitali na kusomesha watoto wetu bure, hakuna kama Magufuli,” Amesema Ditopile.

Amesema wapinzani wanatapatapa kwa sababu hawana Sera wala hawaoneshi kwenye ilani yao watafanya nini zaidi ya kutishia kila siku kuingia barabarani kufanya maandamano badala ya kuwaeleza wananchi watawafanyia vitu gani vya maendeleo.

Ditopile amesema miaka mitano ya Dk Magufuli Wilaya ya Kongwa imefanikiwa kuwa Wilaya ya kwanza Tanzania ambayo vijiji vyake vyote vimefikiwa na umeme lakini pia akisaidia upatikanaji wa vituo vinne vya afya kama alivyoahidi pamoja na kuifanyia maboresho makubwa Hospitali ya Wilaya ambayo imegharimu zaidi ya Sh Bilioni Moja na kuondoa adha ya wananchi wa Kongwa kuwalazimu kwenda hadi Dodoma Mjini.

” Ndugu zangu kwa mambo ambayo Dk Magufuli na Mbunge wenu Spika Ndugai wamefanya kwa miaka mitano hapa mnapaswa kabisa kwenda kumpigia Rais Magufuli kura nyingi za heshima ili tuzidi kumfanya atutumikie kwa upendo zaidi,” Amesema Ditopile.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *