“Dereva Aliwajibu Abiria Wasimfundishe Kazi”- DC Gondwe Afunguka

October 5, 2020

 

Mkuu wa wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe, amewaasa madereva kuzingatia sheria za barabarani na kwamba hata ajali iliyotokea hii leo na kupelekea vifo vya watu 5, chanzo chake ni uzembe wa dereva, kwani abiria walimsisitiza kuhusu kasi yake ya gari akawajibu kwamba wasimfundishe kazi.

Kushoto ni daladala iliyopata ajali Chang’ombe na kulia ni Mkuu wa wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Oktoba 5, 2020, wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital ambapo amesema mpaka sasa dereva hajulikani alipo kwani mara baada ya ajali hiyo alitoweka kusikojulikana.

“Niwape pole familia ambazo wamepoteza wapendwa wao, ambapo mpaka sasa hivi wamefariki 5 na majeruhi 10, inaonekana ni uzembe wa madereva maana wakati wanatoka Buza abiria walikuwa wanamuambia apunguze mwendo na alipofika kwenye mataa taa nyekundu ilikua imewaka, abiria wakamkumbusha lakini akawaambiwa wasimfundishe kazi”, amesema DC Gondwe.

Aidha Gondwe ameongeza kuwa, “Dereva yeye kakimbia na serikali ina mkono mrefu tutamfikia, nitoe wito kwa madereva wa dalaladala wamebeba uhai wa watu, mali zinatafutwa, uhai wa mtu ukipotea hauwezi kurejea kwa hiyo wafuate sheria ili kuokoa maisha”.

Ajali hiyo iliyohusisha daladala na lori imetokea leo Oktoba 5, 2020, katika eneo la Chang’ombe jijini Dar es Salaam, majira ya saa 10:00 alfajiri.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *