CCM Bagamoyo yamshukuru Magufuli,

October 15, 2020

Na Omary Mngindo, Fukayosi

CHAMA Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kimemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa kukipatia Kijiji cha Mkenge Kata ya Fukayosi ekali 100 kutoka Hifadhi ya Ranchi ya Taifa NARCO.

Rais Magufuli ambaye aliziagiza Hifadhi zote nchini kuvipatia ardhi vijiji vinavyozunguka hifadhi hizo kwa lengo la kutumika kwa shughuli za kimaendeleo ikiwemo kilimo, Kijiji cha Mkenge kinachokaliwa na jamii za wakulima na wafugaji nacho kimenufaika na mpango huo kwa kupatiwa eka 100.

Pamoja na juhudi hizo za Rais Magufuli kupitia Hifadhi hiyo ya kukipatia Kijiji hicho ardhi hiyo, chama hicho kupitia Mwenyekiti wake Abdul Sharifu amemuomba mgombea Ubunge Jimbo la Bagamoyo Muharami Mkenge awasilishe ombi kwa Rais Magufuli la kukiongezea ardhi nyingine kutokana na muingiliano wa wakulima na wafugaji.

“Mgombea wetu wa Ubunge Muharami Mkenge nadhani umesikia kilio cha ufinyu wa ardhi unaokikabili Kijiji cha Mkenge, kwaniaba ya wana-Mkenge tukuombe utufikishie ombi kwa mgombea wetu wa urais Dkt. John Magufuli ili atuongezee ardhi kwani eka 100 tuliyopewa ni kidogo ukilinganisha na idadi ya wakazi,” alisema Sharifu.

Kwa upande wake Mkenge alisema kuwa amepokea ombi hilo na kueleza kwamba, Dkt. Magufuli atakapofika wilayani Bagamoyo atamuelezea suala hilo, ikiwemo la eneo la Hifadhi ya Msitu la Kikoka lililopo Kijiji cha Kidomole ambalo kwa miaka mingi limekuwa halitumiki.

“Mbali ya eneo la NARCO pia nitamuwasilishia ombi la kupatiwa eneo la Kikoka lililopo hapa Kidomole ili liweze kutumika na Kijiji, wa-Tanzania tuna imani kubwa na Rais wetu ambae kwa sasa anakiombea kura chama chetu ni kiongozi msikivu hivyo atayapokea maombi yetu,” alisema Mkenge.

Awali Meneja wa Kampeni wa mgombea huyo Yahya Msonde alisema kuwa wa-Tanzania wana kila sababu ya kuwachagua wagombea wanaotokea CCM kwani ilani yao inatekelezeka ukilinganisha na vyama vingine.

“Mfano mfupi ni Rais wetu Magufuli katika kipindi chake cha miaka mitano iliyopia ameziba mianya ya fedha zilizokuwa zinapotea zilizotumika kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali,” alisema Msonde.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *