Baba’ke Amber Rutty Amwangukia JPM!

October 3, 2020

BABA wa msanii anayechipukia Bongo, Rutifya Abubakary ‘Amber Rutty’, Mzee Abubakary Abdul Milenga, amemwangukia laivu Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’, kufuatia hukumu ya miaka mitano jela au faini ya shilingi milioni tatu.

Baba huyo wa Amber Rutty amefunguka kuwa, alipatwa na simanzi kubwa mara tu baada ya kufikishiwa habari kwamba, Amber Rutty alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar.

Mzee huyo amesema kuwa, kama mwanaye huyo atakwenda jela kwa muda huo, basi maisha yake yote yatakuwa ya maumivu. Baba wa Amber Rutty ambaye anaishi Bomba-Mbili wilayani Songea, Ruvuma alisema kuwa, alipopata taarifa hiyo aliishiwa nguvu na hakuweza kula chochote na hadi sasa bado hajakaa sawa.

 

“Tangu nimepata taarifa ya hukumu ya mwanangu, sitaki kuficha hata kidogo, sikuweza kula, ninaweza nikanywa chai nusu kikombe tu basi, maana ninamfikiria sana mtoto wangu kwa janga ambalo amekutana nalo na mimi ni mzee sasa, ninamsaidiaje jamani…”

Anasema baba huyo akimuomba JPM amuonee huruma. Baba huyo aliendelea kusema kuwa, hadi juzi (Jumamosi) alikuwa hajui hatma ya mtoto wake, ukizingatia yeye hana mbele wala nyuma na hajui atapata wapi pesa ya kumdhamini kwa sababu hawezi kufanya kazi yoyote ili apate pesa ya kumsaidia.

“Mimi hali yangu ni mbaya kiuchumi, lakini sina uwezo wa kuweza kumsaidia chochote kwa sababu hata mimi shilingi 5000, ninaitafuta kwa shida mno na siipati, je, milioni tatu nitaimudu mimi?”

Alijihoji baba huyo kwa uchungu mno. Baba huyo aliongeza kuwa, kwa sasa anatafuta nauli ya kwenda jijini Dar kwa ajili ya kumlilia Rais Magufuli ili atoe msamaha kwa mwanaye huyo, maana kama atakaa jela, akitoka hawezi kumkuta akiwa hai.

“Kwa hali yangu hii niliyonayo, ninajitahidi kutafuta nauli niende Dar kumlilia Magufuli ili amsamehe mwanangu, maana sina jinsi ya kufanya na ukweli mwanangu akienda jela, atakapotoka atakuta nimetangulia mbele ya haki,” anasema mzee huyo kwa uchungu.

Mzee Abubakary alimuomba yeyote yule ambaye ana uwezo wa kumsaidia mtoto wake pesa za faini, ajitokeze kumsaidia ili mwanaye awe huru, kwani ameshajifunza vya kutosha, hivyo wamsaidie kupitia namba; 0659 978 777.

Amber Rutty na mumewe, Said Mtopea, walihukumiwa kwa kosa la kujirekodi picha zisizokuwa za maadili, ambazo zilisambaa mitandaoni yapata miaka mitatu iliyopita, ambapo kwa pamoja wanatakiwa kutoa faini ya shilingi milioni sita au kwenda jela miaka mitano.

Mwingine aliyehukumiwa na wawili hao, ni James Delicios ambaye anatakiwa kulipa faini ya shilingi milioni tano au kwenda jela miaka mitano ambaye tayari ameshalipa pesa hizo na kuachiwa huru.

,

Article Categories:
Habari

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *